Itikadi Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Kuhusiana Na Qur-aan – 04

 

 

Itikadi Ya Ahlus-Sunnah Kuhusiana Na Qur-aan - 04

 

Je, Qur-aan Imeumbwa?

 

Abuu Rabiy’

 

 

 

 

Hoja Yao Ya Nne:

 

Baadhi ya mapote yaliyopinda wanadalilisha kuwa Allaah Ameyaumba maneno Yake pale Aliposema:

 

فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِيَ مِن شَاطِئِ الْوَادِ الْأَيْمَنِ فِي الْبُقْعَةِ الْمُبَارَكَةِ مِنَ الشَّجَرَةِ أَن يَا مُوسَىٰ إِنِّي أَنَا اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٣٠﴾

Basi alipoufikia, akaitwa kutoka upande wa kulia wa bonde katika sehemu iliyobarikiwa kutoka mtini kwamba: “Ee Muwsaa! Hakika Mimi ni Allaah, Rabb wa walimwengu.”

 

Hoja yao ni kuwa Allaah Ameyaumba Maneno Yake katika mti, na si kuwa Yeye Amezungumza!!

 

 

Majibu Yetu:

 

Kwanza: Allaah Ametumia kitendo: "Nuudiya".

Na kitendo hiki kinajulisha sauti ya juu na kuzungumza. Haiwezekani katika lugha ya Kiarabu useme kuwa:

ناديت فلانا

Naadaytu fulaanan

 

Kwa maana nimemuashiria au kumnong’oneza au kumuandikia barua, kwa sababu kitendo hiki hakijulishi ila kuita kwa sauti.

 

Pili: Inalazimisha kauli ya kusema kuwa:

 

"إِنِّي أَنَا اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ "

"…Hakika Mimi ni Allaah, Rabb wa walimwengu" [Al-Qaswasw: 30]

 

Ule mti ndio uliosema na wala hakusema Allaah!!!

 

Na hii ni jinaayah kubwa sana kusema maneno kama haya asiyekuwa muumba!!!

 

Na ndio maana Imaam Ibn Abil-‘Izz (Allaah Amrehemu) akawalazimisha laazimu hii:

 

”ولو كان هذا الكلام بدا من غير الله لكان قول فرعون: "أنا ربكم الأعلى" - صدقا إذ كل من الكلامين عندهم مخلوق قد قاله غير الله “!

 

Lau yengekuwa haya maneno yamedhihiri kwa asiyekuwa Allaah ingekuwa kauli ya Fir’awn: “Mimi ndie Rabb wenu aliyekuwa juu" - Ingekuwa ni kauli ya kweli kwa sababu maneno yote haya ya sampuli mbili kwao wao yameumbwa hayajasemwa na Allaah!"

 

 

Bali sisi tunaamini kuwa Allaah Anazungumza kwa sauti na herufi na wala Hafanani na kiumbe Chake katika uzungumzaji Wake. AlhamduliLLaah.

 

 

Hoja Yao Ya Tano:

 

Kuitumia athari ya Ibn Mas’uwd (radhi za Allaah ziwe juu yake) ambayo inasema:

 

”ماخلق الله من سماء ولا أرض ولا جنة ولا نار أعظم من آية فى سورة البقرة الله لاإله إلا هو الحي القيوم...“

 

"Hajapatapo Allaah kuumba katika mbingu wala ardhi wala Pepo wala moto kikubwa zaidi kuliko Aayah katika Suwratul-Baqarah... "

 

 

Majibu Yetu:

 

Na’am athari hii imekuja kwa njia mbili:

1. Kutegemezwa kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa haya ni maneno yake.

 

2. Kutegemezwa kwa Ibn Mas’uwd kwa maana kuwa haya ni maneno yake na si maneno ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ama utegemezwaji wa athari hii kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni batili haikuthibiti kwake Hadiyth hii.

 

Na ama kutegemezwa kwa Ibn Mas’uwd (radhi za Allaah ziwe juu yake), fana’am zimekuja njia nyingi sana za athari hii ikitegemezwa kwake.

 

Na ufupisho ni kuwa kweli kabisa athari hii imethibiti kutoka kwake.

 

Lakini swali la msingi; Je, Wanachuoni waliielewaje hii athari?

 

Anasema Imaam At-Tirmidhiy (Allaah Amrehemu):

 

”حدثنا محمد بن إسماعيل حدثنا الحميدي حدثنا سفيان بن عيينة فى تفسير حديث عبد الله بن مسعود قال: ما خلق الله من سماء ولا أرض أعظم من آية الكرس “

قال سفيان: لأن آية الكرسي كلام الله وكلام الله أعظم من خلق الله ومن السماء والأرض “.

 

"Ametuhadithia Muhammad Ibn Ismaa’iyl (bila shaka huyu ni Imaam Al-Bukhaariy) Amesema: Ametuhadithia Humaydiy (na huyu ni Shaykh katika mashaykh wa Imaam Al-Bukhaariy) Amesema:  Ametuhadithia Sufyaan Ibn 'Uyaynah katika kuitafsiri Hadiyth ya ‘Abdullaah Ibn Mas’uwd (radhi za Allaah ziwe juu yake) amesema:

 

"Hajapatapo Allaah kuumba mbingu wala ardhi kitu kikubwa kuliko Aayatul-Kursiy. Amesema Sufyaan Ibn 'Uyaynah: Kwa sababu Aayatul-Kursiy ni katika maneno Yake Allaah,  na maneno Yake Allaah ni makubwa mno kuliko viumbe Vyake na kuliko mbingu na ardhi."

 

 

Hivi ndivyo walivyofahamu hawa Wanachuoni wakubwa kabisa kuwa uumbaji haukunasibishwa na maneno Yake Allaah. Na wala hapana shaka ikiwa dhati Yake Allaah ni kubwa na tukufu kuliko kitu chochote inalazimisha pia sifa Zake ziwe ni kubwa na tukufu kuliko kitu chochote kwa sababu sifa Zake zinafungamana na dhati Yake. Na maneno kuhusiana na sifa Zake ni kama vile maneno katika dhati Yake" Na wala hapana tofauti!!

 

Ananukulu Imaam Adh-Dhahabiy katika kitabu chake Siyarul A’laami An-Nubalaa mjadala kati ya Imaam Ahmad na wale wanaoona kuwa Qur-aan imeumbwa kwa kudalilisha kwao kwa Hadiyth hii aliwajibu hivi:

 

”إن الخلق واقع ههنا على السماء والأرض وهذه الأشياء لا على القرآن “

 

"Kwamba uumbaji umepatikana huku katika mbingu na ardhi na vitu vingine na si katika Qur-aan."

 

Hivi ndivyo walivyofahamu Wanachuoni wa Ahlus-Sunnah kuhusiana na hii athari, na inatosha kuwa Ijmaa’ yao inathibitisha kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah ambayo hayajaumbwa. Na atakayesema kinyume na hivi twamtaka dalili katika Qur-aan na Sunnah zilizokuwa sahihi.

 

 

Hoja Yao Ya Sita:

 

Qur-aan imesifika na sifa hizi zifuatazo:

1. Imetokezeshwa.

2. Imepambanuliwa.

3. Imejaaliwa na Allaah kuwa ya Kiarabu.

4. Imebarikiwa.

5. Imeteremshwa.

6. Imegaiwa kwa vituo.

7. Imehifadhiwa.

8. Allaah Akitaka Anaweza Kuiondosha yaani iko chini ya uwezo wa Allaah.

9. Ni Nuur.

10. Uongofu.

 

Sifa hizi zote ni sifa za kiumbe, kwani maana ya kiumbe ni kile  kilichokuwa hakipo kisha kikawepo  na hii ndio hali ya Qur-aan na viumbe vingine vyoote.

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Alikuwa Allaah na hakikuwa chochote isipokuwa yeye.

 

Na Allaah ndie alivyojisifu kuwa Yeye ni Kwanza kwani Hana mshirika katika utangu wake si Qur-aan wala chengine.

 

 

Majibu Yetu:

 

 

Bila Shaka mwenye kufuatilia kwa umakini makala zangu ataweza ona nukta ya mzozo kati ya Ahlus-Sunnah na mapote mengine ambayo yamepinda kuhusiana na hii Qur-aan.

 

Kwa sababu wao taswira wanazozijenga kuhusiana na Qur-aan zinatoka kwenye akili zao badala ya kusimama pale ambapo dalili imesimama!

 

Sisi twasema kuwa miongoni mwa sifa za Allaah ni kuzungumza; je, twamaanisha kuwa Allaah Azungumza wakati wote?

 

Yaani akawa Azungumza tu muda wote?

Jawabu: hapana, kuzungumza ni sifa thaabit ya Allaah lakini kumbuka kuwa Allaah Anazungumza Alitakalo muda wowote Autakao. Na ndio maana Alipoamua Kuizungumza Tawraat Aliizungumza na Alipoamua Kuizungumza Zabuwr Aliizungumza na Alipoamua Kuizungumza Injiyl Aliizungumza na Alipoamua kuizungumza Quraan Aliizungumza. Na mfano wa sifa hii ni sifa ya Kuchukia.

Sifa hii ni thaabit kwa Allaah inafungamana na dhati yake na wala hakufananishwi kuchukia Kwake na kiumbe Wake!!

 

Kwa sababu hizi ni dhaati mbili tafauti na kila moja ina majina yake na sifa sake.

Lakini je kuchukia kwake ni moja kwa moja au kwa wakati wote?

Jawabu: hapana anachukia pale ambapo anapoamua kuchukia. Na hili lipo wazi sana kwa mwenye kutaka haki.

Sasa ikiwa ndio hivyo Allaah Aliamua kuizungumza Quraan na Jibriyl (‘Alayhis Salaam) Alimsikia Allaah Akiizungumza hii Qur-aan na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsikia Jibriyl (‘Alayhis Salaam) na Maswahaba (radhi za Allaah ziwe juu yao) walimsikia mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiisoma Qur-aan na walikiri wale waliokuwa mahodari katika lugha ya Kiarabu kuwa hii Qur-aan si mashairi wala ngonjera wala uchawi!

 

Ehe hoja ya kusema kuwa:

"Imetokezeshwa" Ina maana gani mahala hapa?

Je, mwataka kuithibitisha dhati ya Allaah pasina kuwa na sifa?

Au mwataka kusema Allaah Alikuwa pasina kuwa na sifa kisha Akaja kuziumba sifa Zake?

Na kuthibitisha kwenu kuwa Allaah Anazungumza na ilhali maneno Yake Ameyaumba kuna faida gani?

 

Na ndio utaona Maibadhi na mapote mengine yaliyopinda huwa wanaitakidi kuwa hii Qur-aan ilitokezeshwa, kwa maana ilikuwa haipo na kila kilichotokezeshwa basi ni kiumbe!!

 

Hapa pana swali kwa hawa watu:

Je, kuwepo kwake Allaah Alikuwa pasina kuwa na sifa?

Mkisema hapana alikuwa na sifa, swali la pili:

Je, sifa Zake ni kitu kingine ambacho si Yeye au zinafungamana na dhati Yake?

 

Mkisema zinafungamana na dhati Yake kwanini mseme kuwa Qur-aan imeumbwa na wakati ni maneno Yake ambayo Ameyazungumza?

Mkisema sifa Zake ni kitu kingine basi hapo mtakuwa mmeithibitisha dhati pamoja na kitu kingine ambacho ni sifa!!

Na hili litajuwa ni jambo ovu zaidi na mtakuwa mmebatilisha madai yenu yote.

 

 

Ama kauli ya kusema:

"Imepambanuliwa"

 

Naam maneno yake Allaah yapo wazi kabisa tena yana ufasaha wa hali ya juu sana na ndio maana wale waliokuwa mafuswahaa walikiri kuwa huu si uchawi na wala si mashairi na wala haya si maneno ya kawaida!

 

Twawaulizeni hivi:  Ikiwa Allaah Ameuumba huu ufasaha kwa viumbe Wake tena wakawa ni mahodari sana katika fani mbali mbali; je, mlitaka maneno Yake Allaah yawe na mafundo na makongwa hadi ifikie mahala hawa viumbe wayatie dosari?

 

Hayhaat! maneno Yake lazima yawe wazi tena yamepambanuliwa ili msikilizaji akiri kuwa haya ni maneno ya Rabb na wala haina maana kuwa yameumbwa.

 

Kwa sababu mtu anaweza kuwa mfasaha katika maneno yake mpaka akashangaza watu! Na wala watu hawasemi kuwa huu ufasaha Kautengeneza Bali wataishia kusema kuwa hiki ni kipawa.

 

Na Allaah Ana mfano uliokuwa juu zaidi.

 

 

Ama kusema:

"Imebarikiwa"

 

Na’am kwa sababu maneno Yake yametoka kwake Subhaanahu Wa Ta’aalaa, na sote twafahamu kuwa Allaah ni Mtukufu, Allaah ni Mkweli, Allaah ni mwenye Rahmah, Allaah ni Mpole, sasa wategemea maneno Yake Aliyoyazungumza yaweje?

 

Wataka yawe kama ya binadamu ambaye asili yake ni kuidhulumu nafsi yake?

 

Hapana Wa-Allaahi, kama ilivyokuwa dhati Yake Tukufu, na kadhalika maneno Yake Anayoyazungumza lazima yawe Matukufu, na yenye baraka kwa sababu yametoka Kwake kwa kuyasema na wala Hakuyaumba.

 

Hivi jamani kuna mkweli wa maneno zaidi ya Allaah?

Je, kuna maneno yaliyotimia zaidi ya maneno Yake?

 

Jawabu: hapana, na ndio maana Allaah Anasema:

وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّـهِ قِيلًا ﴿١٢٢﴾

… Na nani aliye mkweli zaidi kwa kauli kuliko Allaah? [An-Nisaa: 122]

 

Na ndio maana maneno Yake yakawa mazuri sana kama Alivyokuwa Yeye mwenyewe Mzuri.

 

Kwa hiyo, kudalilisha kwa kuwa maneno Yake yana baraka ndio khalaas yameumbwa hili si kweli labda mje na hoja nyingine.

 

Na hili lipo wazi hata kiakili!

Hivi maneno ya Ibliys yaweza kuwa na baraka na ukweli ndani yake?

Jawabu: hapana, kwa sababu gani?

Kwa sababu Ibliys mwenyewe amelaaniwa amefanywa kuwa dhalili na wala hana thamani, sasa vipi maneno yake yawe na baraka au ukweli au upambanuzi?

 

وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ ۚ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا ﴿٨١﴾

Na sema: “Haki imekuja, na ubatili umetoweka. Hakika ubatili daima ni wenye kutoweka.” [Al-Israa: 81]

 

 

Ama hoja yao kuwa "Imeteremshwa"

 

Neno "Kuteremshwa" ndani ya Qur-aan limekuja katika sampuli mbili:

1. Limefungamanishwa kwa Allaah.

2. Limekuja moja kwa moja bila ya kufungamanishwa kwa Allaah.

 

 

Ama ya kwanza dalili zake:

1. Kauli Yake Allaah:

 

تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّـهِ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ﴿٢﴾

Ni uteremsho wa Kitabu Kutoka kwa Allaah Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote. [Ghaafir: 02]

 

 

2. Kauli Yake Allaah:

وَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَعْلَمُونَ أَنَّهُ مُنَزَّلٌ مِّن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ ۖ فَلَا تَكُونَنَّ مِنَ الْمُمْتَرِينَ ﴿١١٤﴾

 (Sema): “Je, nitafute hakimu ghairi ya Allaah na hali Yeye Ndiye Ambaye Aliyekuteremshieni Kitabu kilichofasiliwa?” Na wale Tuliowapa Kitabu (kabla) wanajua kwamba kimeteremshwa kutoka kwa Rabb wako kwa haki. Basi usijekuwa miongoni mwa wanaotia shaka. [Al-An’aam: 114]

 

3. Kauli Yake Allaah:

تَنزِيلٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿٢﴾

Ni uteremsho kutoka kwa Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu. [Fusw-swilat: 2]

 

Hii ikajulisha kuwa Qur-aan imetoka kwake Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa, tofauti kabisa na kuteremka kwa mvua n.k.

 

Halafu pana tofauti kabisa kati ya kitendo "Anzala" Na "Nazzala"

Na angalia kwa umakini kuwa kitendo kilichotumika katika kuteremshwa kwa Qur-aan "Nazzala".

 

Kitendo ambacho asli ya muweko wake ni kumfanya mfanyaji awe amefanya mara nyingi, na ndio maana Qur-aan haikushushwa kwa mara moja bali iliteremshwa mara nyingi na kitendo chake:

Nazzala Yunazzilu Tanziylan.

 

Na kitendo cha pili ni:

Anzala Yunzilu Inzaalan.

Ambacho asli ya muweko wake kinajulisha mara moja na si mara nyingi.

 

Na nahisi labda tatizo kubwa ni pale Allaah Alipoweka wazi na kubainisha kuwa hii Qur-aan ni Kitabu, hivyo inaweza kuulizwa, sasa hii si inajulisha kuwa imeumbwa?

Jawabu: ni kuwa tatizo ni kitu kimoja, hawa watu waliopinda wakati wanapotetea batili zao huwa hawana uadilifu hata wa kuweza kunukulu!

 

Kwa sababu wanafahamu fika kuwa wakizungumza ukweli na uhalisia wale watu ambao fikra zao hazijafisidika wataweza kufahamu haki na kuifuata!

 

Na ndio maana hata katika uandishi wao huwa wanatumia sana akili kuliko dalili na elimu!

 

Na Mimi nawabishia kama kweli elimu ipo basi iwekeni wazi na acheni kutumia akili na falsafa katika dini.

 

 

Sasa mada:

"KA TA BA" Katika lugha ya Kiarabu mzunguko wake wote unajulisha mkusanyiko.

Na ndio maana unaposema katika lugha ya Kiarabu:

Takattaba Banuu Fulaan

Maana yake: wamekusanyika banuu Fulani.

 

Na kwanini kitabu kama kitabu kimeitwa kitabu?

Kwa sababu ya kukusanyika maneno na herufi katika maudhui ambayo imepangiliwa.

 

Na ndio maana wale majini walipofika kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anasoma Qur-aan walinyamazishana wakiisikiliza hii Qur-aan, na ilipomalizika walikuwa ni waonyaji kwa jamaa zao kwa kuwaambia:

Tumesikia Kitabu ambacho kimeteremshwa baada ya Muwsaa.

 

Kwanini walisema kitabu na ilhali wao waliisikia Qur-aan ikisomwa?

 

Kwa sababu ya mkusanyiko wa maneno na herufi. Na ndio maana unapomwambia mtu kuwa nimehifadhi Qur-aan au Hadiyth (Al-Bukhaariy au Muslim) hashangai hata kidogo!

 

Ehe hoja hapa sasa iko wapi ya kuwa imeumbwa kwa sababu ya kuitwa kitabu?

Au wenzetu mnapohifadhi Qur-aan huwa mnakula karatasi zake pamoja na majalada yake??

 

 

Fuatana na Mimi makala namba tano tukimalizia hoja zao pamoja na majibu.

 

 

 

Share