Binti Yangu Amezaa Na Mkristo Tumekubali Posa Kwa Sharti Abadili Dini, Sasa Anakataa Tufanyeje?

SWALI

 Assalaal Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh.

BINTI YANGU AMEZAA NA MKIRISTO, TUMEKUBALI  POSA NA KUWA ATABADILI DINI SASA ANAKATAA TUFANYEJE

Ndugu zangu nina mtihani mkubwa naombeni msaada na ushauri mapema.

Tuna binti huko UK anasoma tukakuta ana rafiki kijana Mkiristo. Tukamshauri kuwa ni haramu kuishi na kijana mkiristo na tutam-disown kama ataolewa naye abadili dini. Tukamjulisha na kijana kuwa kama anataka kumuoa binti lazima abadili dini awe Muislamu.  Nimekuwa nawapelekea makala nyingi za dini na msahafu wenye tafsiri niliwapa muda mrefu. Binti akatuambia kijana amekubali kubadili dini lakini bahati mbaya sasa wamezaa mtoto. Kijana akaleta posa na tukaikubali kwa sharti letu la kuwa atamuoa tu akiwa amependa dini yetu na abadili dini awe Muislamu ndoa ifungwe ya Kiislamu. Wazazi ndio tumepanga kuonana kupanga kuhusu harusi mwezi ujao.

 Sasa leo binti ananiambia kuwa anaona kijana hajapenda sana kubadili dini na hataki kumlazimisha. Wamepanga wafungie ndoa huko UK ambapo watapewa cheti cha serekali.

Kufuatana na hukmu ya dini tunatakiwa tum-disown binti kabisa kwa hii tabia haramu?. Je Turudishe posa au tumshawishi abadili wafunge ndoa ya Kiislamu?? Sitaki kumuasi Mwenyezi Mungu kwa makosa ya binti ambaye ni mtu mzima.

Mwenyezi Mungu awabariki na kuzidi kuwaongoza katika kazi hii njema ya kuelimisha umma wa Kiislamu.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

‘Kijana kaleta posa na tukaikubali’ Asli katika uchumba na kupelekea kukubali posa ni kuwa muhimu sana kwa wazazi kumkubalia kwa mtoto wao yule aliyewashauri Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pekee tumkubalie, kama kweli ni katika wenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho na kufuata aliyowapa Muhammmad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuacha na aliyowakataza kama inavyotuelekeza na kutusisitiza Qur-aan kwa kusema:

“ … Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu” Al-Hashr: 7.

Kwani Muhammmad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio dira na kiongozi wa Waumini, yeye ni kiongozi pekee anayewapendelea wafuasi wake kila lenye kheri katika maisha yao yote, ndio akawa yanamhuzunisha yanayowataabisha; anawahangaikia sana, anapata dhiki kwa madhara yanayo wasibu, ana hamu tuongoke, tena basi ni mwingi wa huruma na rehema kwetu Waumini; ushauri wake katika posa ni kuwa tumkubali mtu wa namna moja tu, mtu aliye na muelekeo wa kuweza kwa tawfiki yake ar-Rahmaan kumsaidia katika kumpelekea kutekeleza yenye kutarajiwa kumfikisha Peponi na huyo ni yule aliyekubali kwa ridhaa yake.  Na kuyathibitisha hayo kwa vitendo vyake kuwa kuna Mungu mmoja ambaye Pekee ndiye mwenye haki ya kuabudiwa na huyo ndiye mnayetakiwa kuipokea posa yake sio mshirikina; kwani Mkiristo ni mshirikina bila ya shaka yoyote ile, vyenginevyo ni uharibifu katika ardhi kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Atakapokujieni mtayeridhika na tabia yake na dini yake (kwa posa) basi muozesheni, vyenginevyo itakuwa fitna katika ardhi na ufisadi mkubwa” Imepokelea na Al-Haakim.

Hivyo basi kosa lililotendeka kwanza ni kwenda kinyume na ushauri bali amri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kukubalia posa ya uliyesema, ‘kijana Mkiristo akaleta posa na tukaikubali’, kwa kukubali posa yake mlikuwa mmeridhika na nini? Tabia zake?! Tabia ya kuishi na mtoto wenu na kumzalisha! Dini yake?! Kumshirikisha Allaah kwa kusema kuwa ana mtoto au kuabudu masanamu! Kuna ushirikina zaidi ya huu?! Kipi mlichoridhika nacho?    

Jengine ni kuwa umekwenda kinyume na ushauri bali pia ni amri ya Allaah kwani Ametukataza kuwaoa au kuwaozesha watoto wetu washirikina; kwa kuipokea posa ni kama ushakata shauri la kuwa tayari kumuozesha mtoto wenu kama ulivyosema, ‘Wazazi ndio tumepanga kuonana kupanga kuhusu harusi mwezi ujao’

na Qur-aan inakushauri na kukuamrisha hivi:

“Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Allaah Anaitia kwenye Pepo na maghafira kwa idhini yake…” Al-Baqarah: 221.

Umesema, ‘Tuna binti huko UK anasoma’, katika makosa ambayo yanafanywa tena kwa wingi ni huku Waislamu kutomsikiliza na kushikamana na ushauri wake wanaedai kuwa wanampenda na kumtukuza, Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kumpeleka mtoto wa kike masomoni tena Uingereza ambako hakuna neno haramu katika kamusi la jamii yao, huko ni kumtelekeza na kumuangamiza mtoto, watoto wa kiume hupotea achila mbali wa kike.

Wazazi wenye kipato huonelea ni vyema kuwasomesha mtoto wao nchi za nje (sio vibaya kama kinachotakiwa hakipo katika nchi zao) ila tu wanahitaji waulize nini ametushauri Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu kusafiri mwanamke kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriy amesema: amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Si halali kwa mwanamke (katika riwaya): - Kwa hakika hakai pekee mwanamume na mwanamke isipokuwa yuko Mahram wa huyo mwanamke - , mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho kusafiri safari ya siku tatu na ziada isipokuwa anakuwa pamoja naye baba yake au mtoto wake au mume wake au ndugu yake au Mahram wake” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Hijja, mlango safari ya mwanamke pamoja na Mahram wake Hajj na kwengineko.

Kama katika kesi yetu hii palifuatwa ushauri huu wa kusafiri na kuishi na Mahram wake huko UK, basi kusingekuwepo neno lako la  ‘tukakuta ana rafiki kijana Mkiristo’, haya pengine yasingelitokea; na kubwa zaidi ni kuwa kama tulimuandaa na kumsomesha mapema kuhusu dini yake na kumuelewesha lipi ni halali na lipi ni haraam kabla ya safari yake na kuhakikisha kuwa akili yake ni yenye kuelewa na kufanya kazi sawa sawa na imani ipo katika moyo wake na kuelewa kuwa dini yake ni ya haki na ndio ya kufuatwa na kila mtu, ilikuwa yeye mwenyewe huyo mtoto wenu kama anamtaka na kumpenda kikweli kweli awe baba wa watoto wake; alitarajiwa kama ni Muislamu yeye mwenyewe awe na uwezo wa kumueleza na sio nyinyi kumueleza huyo kijana kama ulivyosema, ‘Tukamshauri kijana’; kama alivyomueleza Ummu Saliym Abu Twalhah alipotaka kumuoa, kisa chake ni sawa sawa na cha mtoto wenu kama anavyosimulia Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa kusema:

“Alileta posa Abu Twalhah kutaka kumuoa Ummu Saliym; Ummu Saliym akamwambia: Wa Llaahi (kwa kula kiapo) haiwezekani kwa mtu kama wewe Abu Twalhah kuoana na mimi, kwani wewe ni kaafir (mkiristo) na mimi ni Muislamu na si halali kwangu kuolewa na wewe; utaposilimu (ukibadili dini na kuwa Muislam) basi huko kusilimu kwako ndio kutakuwa mahari yako kwangu na sitotaka zaidi ya hilo; basi Abu Twalhah alisilimu na ikawa ndio mahari yake; Thaabit amesema: Sikuwahi kusikia kwa mwanamke yeyote aliyewahi kupata mahari bora na mazuri kuliko Ummu Saliym kwani mahari yake yalikuwa Uislam…” Imepokelewa na An Nasaaiy, kitabu cha ndoa ,mlango wa kuolewa kwa sababu ya Uislamu.

Hivyo basi kama mtoto wenu ni Muislam, alitarajiwa kuwa na msimamo kama huu wa Ummu Saliym wa kumueleza kuwa ni muhali bali ni haramu kuolewa na mkiristo na ukisilimu basi huko kusilimu kwako ndio kutakuwa mahari yako kwangu na sitotaka zaidi ya hilo kwani dini kwangu ndio uti wa mgongo wa maisha yangu.

Kisha umesema, ‘Tukamjulisha kijana kuwa kama anataka kumuoa binti lazima abadili dini awe Muislamu. kwa sharti letu la kuwa atamuoa tu akiwa amependa dini yetu na abadili dini awe Muislamu ndoa ifungwe ya Kiislamu’. Asli, haya yalikua yatokee kwa mtoto wenu kama ni Muislamu na yalikuwa yaje kwa njia nzuri ya kumlingania na njia iliyokuwa nzuri ya kumlingania  kwani kwa kijifedhehesha kwake sasa wamezaa mtoto, kutokuwa yeye mwenyewe Muislam na kumthibitishia kivitendo kuwa hakuna haja ya kubadili dini wala kufunga ndoa Kiislamu. Kisha umesema, ‘anaona kijana hajapenda sana kubadili dini na hataki kumlazimisha. Wamepanga wafungie ndoa huko UK ambapo watapewa cheti cha serekali’, hakika huo ndio mchango wa mtoto wenu kumpelekea kijana abakie kama alivyo; kwani kuna usemi sio mzuri lakini hapa ni pahala pake unaosema: “kuna haja gani ya kununua ngo’mbe ikiwa unapata maziwa kwa kawaida kama apatavyo mmiliki wa ngo’mbe,”  na haya ndio aliyokuwa nayo kijana katika akili yake ya nini kubadili dini na ya nini kuoana Kiislamu kwani kila nikitakacho chenye kuitwa maisha ya ndoa baina ya mke na mume ninakipata bila ya kuoa wala kubadili dini na ushahidi wake sasa wamezaa mtoto.

Umesema, ‘Sitaki kumuasi Mwenyezi Mungu kwa makosa ya binti ambaye ni mtu mzima’.  Kwa hakika tushamuasi Mwenye nguvu na Mwenye adhabu iliyo chungu! Kwani tulitakiwa tujilinde nafsi zetu na ahali zetu (akiwemo huyo mtoto wetu) na Moto wa Jahannam, na kujilinda kwenyewe ni kutekeleza kila litaloweza kwa tawfiki yake Allaah kukupelekea kutokwenda kinyume na amri za Allaah na haya huja kwa kumuelimisha kama ulivyosema Nimekuwa nampelekea makala nyingi za dini na msahafu wenye tafsiri’ yepi halali kwake na yepi haraam na kule kumpeleka UK bila ya Mahram kumechangia yote nako ni kwenda kinyume na amri ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) , hivyo basi mumemtelekeza na kumsukumiza mtoto wenu katika Moto, bila shaka yoyote ile mumeasi na mumekwenda kinyume na mafundisho ya Qur-aan, kwani Qur-aan inasema:

 

“Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa Anayowaamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa” At-Tahriym: 6.

Tunatumai kuwa hii itakuwa funzo kwa wazazi wengine pia wasije kufanya kosa kama hili kwa watoto wao wa kike.

Umesema, ‘Kufuatana na hukmu ya dini tunatakiwa tum-disown binti kabisa kwa hii tabia haramu?’ Nyinyi wazazi mna makosa yenu na mtoto ana yake; na lilio wazi ni kuwa yeye ni mzinifu na zinaa ni haraam katika Uislamu na kama atakuwa anaona na kuitakidi kuwa zinaa ni halali na sio haraam basi atakuwa amehalalisha kilichoharamishwa na Allaah hivyo atakuwa ametoka nje ya duara la Uislamu kwa kuhalalisha aliyoharamisha Allaah; hukumu ya mzinifu kama inavothibitisha Qur-aan ni kupigwa mboko mia (100), hakuna pa kutekelezwa hayo; lakini hayo yatamthibitikia Siku ya Malipo kama hatotubia na kuacha kuzini; Qur-aan inasema:

“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini.” An-Nuur: 2.

 

Umesema tena, ‘Je Turudishe posa,’ kwa hakika ndugu yetu hapo hakuna posa, kwani aliyeleta posa hana haki ya kumuoa mtoto wenu kama mnaamini Allaah na Siku ya Mwisho na kutarajia aliyoyaandaa kwa wenye imani hiyo; kwani mtoto wenu kama ni Muislamu si halali kuolewa na huyo kijana Mkiristo kama ilivyoashiria Qur aaan kwa kusema:

 

“….Wanawake hao (Waumini) si halali kwa hao makafiri, wala hao makafiri hawahalalikii wanawake Waumini. Na wapeni hao wanaume mahari waliyotoa….” al Mumtahinah aya ya 10.

 

Hivyo basi kurudisha posa na kutorudisha hakutosaidia kitu, kwani kilichotakiwa na wote wawili kinapatikana kila wanapotaka; hivyo basi kinachotakikana ni kumuaidhi na kumnasihi kwa kumueleza mtoto wenu kuwa anazini na Allaah Ameiharamisha na kutahadharisha kwa kuikaribia zinaa, yeye analala na kuamka nayo, bali ndio maisha yake, pia kumuelewesha kuwa huenda yeye kwa kumkubalia ayatakayo akawa miongoni au sababu tosha ya kumpelekea huyo Mkiristo kuona kuwa Uislamu si lolote bali ni kama Ukiristo kwani wao kama wanavyodai kuwa ni mafundisho ya dini yao huishi na kuzaa kisha wakaja kufunga ndoa miaka mingi bada ya kupata watoto kama watataka.

 

Kisha ukasema, ‘tumshawishi abadili wafunge ndoa ya Kiislamu??’ Ndoa ya Kiislamu haifungwi isipokuwa baina ya Waumini wawili na hapa hakuna hilo, bali haliruhusiwi kwa muozeshaji kumuozesha Muislam kwa asiye Muislamu hata kama wao wataridhiana na mtoto wako anayaelewa hayo ndio akakutaarifuni kuwa ‘Wamepanga wafungie ndoa huko UK ambapo watapewa cheti cha serekali.’

 

Tunamuombea Allaah (Subhaana wa Ta’ala) Amuongoze mtoto wenu Amuonyeshe haki na atoke katika maasi hayo kabla hayajazidi madhara kwake, na tunawaombea watoto wetu wote wa Kiislamu Allaah Awaongoze katika Njia iliyonyooka. Aamiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share