Du'aa Maalumu Au Makhsusi Za Kila Baada Ya Swalaah Ni Swahiyh?
SWALI:
BAADA YA SWALAH YEYOTE HUWA NA TAKA NISOME DUA. SO KWAJILI YA SWALAH YA FARDH NAFUAATA HISNUL MUSLIM PAMOJAA NAA ZIKO DUAA NYENGINE NIMEPEWA NA SHOGA YANGU WA MUSSCAT KAMA DUA YA KUSOMA BAADA YA SWALAH YA ADHUHURI......... MPAKA ISHAA. NA VILE VILE ZIKO DUA NYENGINE HIVI HIVI MKUSANYIKO WA AYAA ZA KURAANI ZINAZO ANZIYA ALLAAHUMMA NA RABBANA JEE NI SAHIHI AU WRONG?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani ndugu yetu katika Imani kwa suala lako hilo. Tufahamu kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia muongozo katika Ibaadah zetu ili ziwe ni zenye kutakabaliwa na Allaah Aliyetukuka.
Miongoni mwa Ibaadah ni du‘aa ambayo tunatakiwa tuwe ni wenye kumuomba Allaah Aliyetukuka. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Du‘aa ni Ibadah” (at-Tirmidhiy).
Hakika ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na adhkaar ambazo alikuwa akizileta baada ya kila Swalah ya faradhi. Baada ya kumaliza Swalah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akileta Istighfaar mara tatu (Astaghfirullah). Kisha akisoma
اللّهُـمَّ أَنْـتَ السَّلامُ ، وَمِـنْكَ السَّلام ، تَبارَكْتَ يا ذا الجَـلالِ وَالإِكْـرام
Allaahumma Antas-salaam wa Minkas-salaam Tabaarakta Yaa dhal Jalaal wal Ikraam
(Ewe Mola! Wewe ndiwe Amani, na amani yatokana Nawe, Umetukuka ewe Mwenye Enzi na Mwenye kustahilki kuheshimika).
Baada ya hapo alikuwa akisoma Ayaatul Kursiy (2: 255), kisha akimsabihi mara 33, akimuhimidi mara 33, akikabiri mara 33 na akitimiza mia kwa kusoma
لا إلهَ إلاّ اللّهُ وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ المُـلْكُ ولهُ الحَمْد، وهوَ على كلّ شَيءٍ قَدير، اللّهُـمَّ لا مانِعَ لِما أَعْطَـيْت، وَلا مُعْطِـيَ لِما مَنَـعْت، وَلا يَنْفَـعُ ذا الجَـدِّ مِنْـكَ الجَـد
Laa ilaaha illa Llaahu Wahdahu laa shariika Lahuu Lahul Mulku wa Lahuul Hamd wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr. Allaahumma laa maani'a limaa A'twayta, wa laa mu'twiya limaa Mana'ta, wa laa yanfa'u dhal jaddu Minkal-jadd
"Hapana apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah hali ya kuwa Peke Yake Hana mshirika, niwake Ufalme, na ni Zake sifa njema, na Yeye ni muweza wa kila kitu. Ee Allaah, hakuna mwenye kukizuia Ulichokitoa, wala mwenye kutoa Ulichokizuia, na wala utajiri wa mtu haumnufaishi mwenye utajiri mbele Yako.”
لا إلهَ إلاّ اللّه, وحدَهُ لا شريكَ لهُ، لهُ الملكُ ولهُ الحَمد، وهوَ على كلّ شيءٍ قدير، لا حَـوْلَ وَلا قـوَّةَ إِلاّ بِاللهِ، لا إلهَ إلاّ اللّـه، وَلا نَعْـبُـدُ إِلاّ إيّـاه, لَهُ النِّعْـمَةُ وَلَهُ الفَضْل وَلَهُ الثَّـناءُ الحَـسَن، لا إلهَ إلاّ اللّهُ مخْلِصـينَ لَـهُ الدِّينَ وَلَوْ كَـرِهَ الكـافِرون
Laa ilaaha illa Llaahu wahdahu laa shariika lahuu lahul Mulku wa lahuul Hamd wa Huwa ‘alaa kulli shay-in Qadiyr, laa hawla wa laa quwwata illa BiLLah, laa ilaah illa-Allaah, wa laa na'budu illa Iyyaahu, Lahun-ni'matu wa Lahul-fadhwl, wa Lahuth-thanaaul-Husn, laa ilaaha illa-Allaahu mukhliswiyna Lahud-diyna wa law karihal-kaafiruun.
“Hapana apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah hali ya kuwa Peke Yake Hana mshirika ni Wake Ufalme, na ni Zake sifa njema, na Yeye juu ya kila kitu ni Mueza, hapana uwezo wala nguvu ila vyote vinatokana na Allaah, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah, wala hatumuabudu ila Yeye, ni Zake neema, na niwake ubora, na nizake sifa nzuri zote, hapana mola apasae kuabudiwa kwahaki ila Allaah hali ya kumtakasia dini yake, ijapokuwa wanachukia makafiri”
Baada ya kuleta adhkaar hizo baadhi ya nyakati unaweza kumuomba lolote unalotaka kutoka kwa Allaah kwa lugha yoyote unayojua na kupenda. Ukitaka kutumia du’aa ambazo zimo ndani ya Qur-aan zinazoanza na Allaahumma au Rabbaana itakuwa ni juu yako kwani hizo zote ni du‘aa nzuri zenye faida kwako na kwa Waislamu wenzio. Pia zipo Hadiyth zinazotutajia du‘aa alizokuwa akiziomba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nasi tunaweza kuzitumia. Lakini sehemu nzuri za kuomba du’aa ni wakati wa kusujudu na wakati umemaliza kusoma tashahhud kabla hujatoa salaam.
Ikiwa unatumia Hiswnul Muslim basi hicho kitabu kitakutosheleza kwani zimo adhkaar nyingi kutoka Hadiyth zilizo madhubuti na barabara, zilizo sahihi. Huna haja ya hivyo vitabu vingine ulivyopewa maana vitabu vingi vya du’aa vilivyoandikwa na watu, si vitabu vya kutegemewa na vingi havina du’aa sahihi kama zilivyo kwenye kitabu cha Hiswnul Muslim. Bonyeza kiungo kifuatacho upate hicho kitabu:
Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)
Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuwafikishie kuweza kufuata Sunnah ya kipenzi chetu, Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Na Allaah Anajua zaidi