Je, بسم الله (BismiLLaah) Inahesabika Kuwa Ni Aayah Katika Suwratul Faatihah?
Je, بسم الله (BismiLLaah) Inahesabika Kuwa Ni Aayah Katika Suwratul Faatihah?
SWALI:
Assalamu Aleykum Warahmatullahi Wabarakatu, Swali Langu Ni Hili Katika Suwrah Nyingine Zote Tunapata Kuwa Bismillahi Rahmani Rahim Ndio Utangulizi Au Ndio Ufunguzi Wa Suwrah Lakini Katika Suwrah Faatihah 'bismillahi Rahmani Rahim' Imekuwa Kama Aayah Ya Kwanza Ya Suwrah 'Faatihah' Naomba Ufafanuzi Kutoka Kwenu, Jee Bismillahi Rahmani Rahim Ile Katika Suwrah 'Al-Faatihah' Na Zile Bismillahi Rahmani Rahim Nyingine Katika Zile Suwrah Nyingine Tafauti Yake Ni Nini? Shukran Wa Jazakallah Kher.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Bismillaahi ar-Rahmanir Rahiym katika Suwrah Faatihah na Suwrah nyinginezo. Kuhusu suala hilo kuna tofauti baina ya wanachuoni na kila mmoja ana dalili zake kuhusu hilo:
Mwanzo ni kuwa wanazuoni wamekubaliana kuwa al-basmalah (BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym) iliyopo katika Surawh Naml (27) kuwa ni sehemu ya Aayah katika kauli Yake Aliyetukuka:
إِنَّهُ مِن سُلَيْمَانَ وَإِنَّهُ بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿٣٠﴾
30. Hakika hiyo ni kutoka kwa Sulaymaan, na hakika hiyo (imeanza) Kwa Jina la Allaah, Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu. [An-Naml: 30]
Na haihesabiwi kuwa ni mwanzo wa Aayah ya Suwrah hiyo, na kuisoma mwanzo wa Suwrah hiyo ni Makruuh.
Hata hivyo, wanachuoni wametofautiana kama al-basmalah ni Aayah katika Suwrah Faatihah na katika mwanzo wa kila Suwrah au la? Kauli za wanachuoni katika hilo ni kama zifuatazo:
1. Hiyo ni Aayah katika Suwrah Al-Faatihah na kila Suwrah katika kila Surah isipokuwa Bara’ah (Suwrah Tawbah). Na hiyo Madh-hab ya Imaam Ash-Shaafi'iy, Ath-Thawriy, Ibnul Mubaarak na kundi la wanachuoni.
2. Si Aayah katika Suratul Faatihah wala Surah nyingine yoyote katika Qur-aan. Na hiyo ni kauli ya Imaam Maalik, Al-Awzaa’iy na moja ya riwaya kutoka kwa Imaam Ahmad (Ingawa kuna mashaka kuhusu usahihi wa hiyo riwaya kutoka kwa Imaam Ahmad kama ilivyotajwa katika Al-Muhadhab).
3. Hiyo ni Aayah kamili katika Suwrah Al-Faatihah na si katika Suwrah zingine. Hii ni kauli ya Is-haaq, Abu ‘Ubayd na riwaya moja kutoka kwa Imaam Ahmad.
4. Si Aayah katika Suwrah Al- Faatihah wala mwanzo wa Suwrah nyinginezo, bali ni Aayah kitenganishi baina ya Suwrah. Na hiyo ni kauli ya Madh-hab ya Imaam Abu Haniyfah na ndio kauli sahihi katika madh-hab ya Imaam Ahmad.
Rai hii ya nne, ameielezea Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah kuwa ni rai au maelezo yaliyo ya kati kwa kati katika maelezo yote yaliyotangulia.
Na inayoonekana ni kuwa kauli ya Abu Haniyfah ina nguvu zaidi.
Ama kusoma al-basmalah katika Swalah, wanachuoni pia wametofautiana kwa kauli zifuatazo:
1. Imaam Maalik amekataza kusoma al-basmallah katika Swalah za Faradhi, kwa sauti au kawa siri. Hilo halifai kufanywa katika ufunguzi wa Suwrah Al-Faatihah wala Suwrah nyingine. Na amejuzisha kusomwa katika Swalah za Sunnah.
2. Imaam Abu Haniyfah naye amejuzisha kuisoma kwa siri pamoja na al-Faatihah katika kila Rak'ah ya Swalah, na ikiwa ataisoma pamoja na kila Suwrah itakuwa vyema.
3. Ama Imaam ash-Shaafi'iy, ni wajibu kwa mwenye kuswali kuisoma, ikiwa kwa sauti aisome kwa sauti na ikiwa ni Swalah ya siri basi kwa siri.
4. Na Imaam Ahmad bin Hanbal naye amesema, anafaa mwenye kuisoma aisome kwa siri na haifai kuijihirisha kabisa.
Hakika ni kuwa Suwrah Al-Faatihah ina Aayah saba peke yake na katika hilo wametofautiana wanachuoni kuhusu ni ipi Aayah ya mwanzo. Wengine wamesema bismiLLaah ni Aayah na wengine wameona sio.
Na Allaah Anajua zaidi