Mashairi: Twawapenda Aali Bayti
Muhammad Faraj Salim As-Sa’ay
Ndugu yangu hebu keti |
usikiye nisemayo |
Andika kila ubeti |
wa maneno ninenayo |
Uchukuwe na sileti |
na kalamu uwe nayo |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |
|
|
Nyumba ya tumwa Nabia |
nuru ilikochomoza |
Ikaangaza dunia |
huku ikituongoza |
Tukaifahamu njia |
hako wa kutupotoza |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |
|
|
Wao wametoka kwake |
maimamu na Khalifa |
Ni watu wa nyumba yake |
walopata kila sifa |
Waume kwa wanawake |
hekima na maarifa |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |
|
|
Isomeni Quruani |
mupate kuyafahamu |
Yote yamo humo ndani |
maneno Yake Karimu |
Kwa mapenzi na hisani |
ataka tuwakirimu |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |
|
|
Ali Hasani Huseni |
Fatwima na dada zake |
Muttalibi si wageni |
wote ni aila yake |
Hawa wote wa nyumbani |
pamoja na wake zake |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |
|
|
Wakeze ni wetu mama |
hayo kasema Manani |
Neno Lake kaditama |
halifutwi asilani |
Haishi ila na wema |
Hamadi kwake nyumbani |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |
|
|
Wakeze ni wetu mama |
Aali Bayti nao piya |
Sifa mbili zote njema |
ni tunuku la Jaliya |
Ni daraja na rehema |
za akhera na duniya |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |
|
|
Wote sisi twawapenda |
Rabbi Mola Shuhudiya |
Kwa maneno na kutenda |
Uloridhi twaridhiya |
Sisi hatufanyi inda |
huyu towa huyu tiya |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |
|
|
Swala baraka salamu |
mfikishie Nabiya |
Mbora wa wanadamu |
mola Ulomswaliya |
Na Aali Bayti kiramu |
na Swahaba zake piya |
Hikaya za Aali Bayti |
nyumba ya tumwa Nabiya |