Matumizi Ya Ijitihaad Kwa Swahaba (رضي الله عنهم) Na Sababu Za Kutofautiana Kwao

 

Matumizi Ya Ijitihaad Kwa Swahaba (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمْ)

 Na Sababu Za Kutofautiana Kwao

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Utangulizi

 

 

Taariykh ya Shari'ah ilianza kuchukua hatamu tokea siku ya mwanzo ambapo Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipewa Utume kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kutambulika kuwa ni Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wala hakuna shaka yoyote kwamba Nabiy Muhammad amefunga milango ya kuja Nabiy mwengine.

 

Shari'ah iliendelea kwa watawala wa mataifa ya Kiislamu baada ya kifo cha Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Matokeo yake kulikuwa na vyanzo tofauti vya Shari'ah kwa kulinganisha na kipindi cha Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Vyanzo vikuu vya Shari'ah wakati wa maisha ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) havikuwa tofauti na tunavyotumia sasa; navyo ni Qur-aan tukufu na Sunnah (mwenendo wa Nabiy). Hivyo, Shari'ah wakati wa kipindi hichi ilitokana moja kwa moja na hoja za wazi na sio dhana. Pindipo tatizo linapoibuka, kulikuwa na suluhisho mahsusi kutoka Qur-aan na Sunnah, ambazo hazikuleta mabishano ya mjadala. Kwani daima Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakitoa hoja moja kwa moja. Ingawa kwa upande mwengine Ijtihaad ilitumika, lakini bado vyanzo vikuu vilibaki kuwa ni Qur-aan na Sunnah.

 

 

Matumizi Ya Ijtihaad Miongoni Mwa Swahaba

 

Ijtihaad ilianza kutumika tokea zama za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini kilikuwa ni chanzo kidogo tofauti na ilivyopewa kipaumbele baada ya kifo cha Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa mujibu wa taariykh, Nabiy pia alikuwa akifuata Ijtihaad yake lakini pindipo tu anapokosea, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) alikuwa akimrekebisha mara moja. Mfano wa amri ya kuwaachia huru wapiganaji wa Taabuuk iliyotolewa na Allaah kwani hawakutaka kupigana. Na Allaah Aliwatambua kuwa ni wanafiki wa Uislaam.

 

Kwa vile Nabiy alitoa baadhi ya amri kwa kutumia Ijtihaad, ndio sababu ya kuwaruhusu Swahaba wengine kuifanyia kazi. Kwa mfano, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipompeleka Mu'aadh nchini Yemen[1], mazungumzo yao yalikuwa kama ifuatavyo:

 

Nabiy: Kwa kutumia nini utasuluhisha mgogoro?

Mu'aadh: Qur-aan.

Nabiy: Kama hutopata (kanuni kutoka Kitabu cha Allaah)?

Mu'aadh: Kwa kutumia Sunnah ya Rasuli wa Allaah.

Nabiy: Kama hutopata (kanuni kutoka Sunnah)?

Mu'aadh: Nitatumia maoni yangu.

Nabiy: Shukurani ni kwa Allaah, aliyempatia mafanikio mjumbe wa Rasuli wa Allaah kwa kufanikisha lile Analolipenda Allaah[2]

 

 

Sasa Ni Nini Hiyo Ijtihaad?

 

Kwa mujibu wa sifa zake, Ijtihaad inaweza kufasiriwa kama ni matumizi ya mawazo binafsi, ambayo chanzo chake na hoja yake yanatokana moja kwa moja aidha kutoka Qur-aan au Sunnah au vyote. Shari'ah inayofanywa hapa ni lazima iwe inatoka kwa mtu aliyebobea kielimu na kumcha Allaah kama vile Mujtahid au Swahaba. Wengine wanaifasiri kama ifuatavyo:

 

 

Matumizi ya hoja binafsi ya mwanazuoni ili kupata amri mpya ya kisheria.[3] Pia Ijtihaad inamaanisha kufanya bidii kubwa ya kutoa amri ya kisheria kwa kuegemeza kwenye ithibati yake au kuichambua kutoka vyanzo vyake ambapo ithibati zake au vyanzo vyake havijatolea maelezo ya wazi.[4]

 

 

Umuhimu wa Ijtihaad ni kupanua kanuni za jumla kutoka Qur-aan na Sunnah kwani idadi ya aayah za Qur-aan zinazojadili kuhusu mambo ya kisheria yamekadiriwa. Hali hiyo pia ni kwa Sunnah ambayo haiendi zaidi ya masuala ya kisheria alfu moja au mbili. Tofauti na masuala ya kisheria ambayo wanakumbana nayo Waislamu, ambayo hayana idadi maalum.

 

 

Kutokana na kubadilika wakati na Uislaam kuenea zaidi, kulikuwa na haja ya kufasiri adhabu kwa wanaotiwa hatiani. Kulikuwa na sababu ya kutofautisha baina ya wajibu wa kijamii na wa kisheria, wajibu wa yale yanayopendekezwa, yanayozuiwa na yanayoruhusiwa.[5]

 

 

Ijtihaad ilitumiwa kwa mapana na Swahaba wa Nabiy Muhammad (Radhwiya Allaahu ‘Anhum). Sababu kuu ya Khulafaau Raashiduun kuifanyia kazi Ijtihaad ni kupanuka kwa Taifa la Kiislamu hadi sehemu za Persia, Iraaq, Syria na Misri. Ambapo huko walikuwa na mila, tamaduni, miiko, lugha, siasa na uchumi; yote yakiwa tofauti na mazingira aliyoyaacha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kanuni ya Ijtihaad haitolewi tu kama ni mawazo huru kabisa. Ni lazima yapite kutoka Qur-aan kupitia Sunnah, kama hakujaonekana kitu, basi hilo suala ni geni na itabidi lifananishwe na Qur-aan au Sunnah, hapo kati ndipo panapopatikana Ijtihaad.

 

 

Swahaba walikuwa na kawaida ya kuifanyia kazi Ijtihaad kupitia Qur-aan au Sunnah. Ijtihaad ilifanyiwa kazi kwenye kuifasiri Qur-aan na Sunnah pamoja na fafanuzi zake. Kama tatizo halijaonekana ama halipo, wanalifananisha na mfano uliomo ndani ya Qur-aan au Sunnah.

 

 

Kwa mfano, Sayyidna 'Aliy (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alifananisha baina ya kizuka ambaye mumewe hakumpatia kiwango maalum cha mahari kabla ya kufariki na kesi ya mjane aliyeachwa kabla ya kuingiliwa na hakuwekewa wala hakupatiwa mahari yake.

 

 

Ni kupitia kwa aayah ifuatayo ambapo Sayyidna 'Aliy aliilinganisha:

 

لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً ۚ وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ ﴿٢٣٦﴾

Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia kwao mahari. Wapeni kiliwazo kwa mwenye wasaa kadiri ya uwezo wake na mwenye dhiki kadiri ya uwezo wake. Maliwaza kwa mujibu wa ada, ni haki kwa wafanya ihsaan. [Al-Baqarah: 236]

 

 

Hoja ya kulinganisha aliyoruhusu kuifanya Sayyidna 'Aliy (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) ilikuwa kwamba talaka na kifo ni sababu za kubatilisha mahusiano baina ya mume na mke.

 

 

Ukusanyaji wa Qur-aan kukusanywa pamoja ni mfano mwengine wa namna Ijtihaad ilivyofanyiwa kazi. Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alikubaliana na Ijtihaad zilizofanywa na Swahaba wengine za kuikusanya pamoja Qur-aan wakikhofia kuipoteza Qur-aan kutokana na sababu za uhamiaji na kufariki kwa mahaafidh wa Qur-aan. Sayyidna 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alitoa wazo (Ijtihaad) kuikusanya Qur-aan kwa kuiwekea irabu ili kwamba kusitokee khitilafu ya kisomo baina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu.

 

 

Sababu Za Kutofautiana Kwa Ijtihaad

 

Kwa mujibu wa Dr. Hussain Alamid Hassan, yeye ameeleza sababu za kutokea kwa hitilafu baina ya Swahaba, ambazo tunazifupisha kama ifuatavyo:

 

1.   Ufahamu wa maana za maneno ya Qur-aan.

 

 

2. Matini mbili zenye maana tofauti. Kwa mfano katika suala la eda kwa mwanamke aliyeaachika akiwa mja mzito. Hili linajadiliwa ndani ya matini mbili sawa sawa.

 

Ya kwanza ambapo inabainisha kuwa kipindi cha eda kinamalizika baada ya kujifungua ni:

 

وَاللَّائِي يَئِسْنَ مِنَ الْمَحِيضِ مِن نِّسَائِكُمْ إِنِ ارْتَبْتُمْ فَعِدَّتُهُنَّ ثَلَاثَةُ أَشْهُرٍ وَاللَّائِي لَمْ يَحِضْنَ ۚ وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ ۚ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا﴿٤﴾

Na wale wanawake wanaokoma hedhi miongoni mwa wanawake wenu, mkiwa mna shaka, basi eda yao ni miezi mitatu, pamoja na wale wanawake wasiopata hedhi. Na wenye mimba muda wao (wa eda) watakapozaa mimba zao. Na yeyote anayemcha Allaah Atamjaalia wepesi katika jambo lake. [Atw-Twalaaq: 4]

 

 

Na ya pili ni ile inayoeleza kipindi cha miezi minne na siku 10, hata kama hakuzaa:

 

 وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا ۖ فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا فَعَلْنَ فِي أَنفُسِهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿٢٣٤﴾

Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, hao wake wangojee peke yao (eda) miezi minne na siku kumi. Watakapofikia muda wao, si dhambi kwao katika yale waliyoyafanya katika nafsi zao kwa ada ya shariy’ah. Na Allaah kwa yale myatendayo, ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Al-Baqarah: 234]

 

3.    Kiwango cha ufahamu wa Sunnah.

 

 

4. Kutofautiana katika hoja za ufahamu wa Sunnah. Mujtahiduun waliokuwa wakifanya Ijtihaad walikuwa na mawazo yanayokaribiana. Baadhi ya Mujtahid walihitaji kwamba Mujtahid mwengine ama msimulizi lazima akubaliane na Ijtihaad yake na ale kiapo.

 

 

5. Tofauti ya mawazo ya kisheria (fatwa) ambapo Swahaba atalinganisha kesi na nyengine kwa kukisia, vivyo hivyo akimtumia Swahaba mwengine na hapo hitilafu hutokezea na kutofautiana na kiwango ama hadhi ya maamuzi.

 

 

Hizo ni sababu alizozieleza Dr. Hussain. Hata hivyo, wanazuoni wengine wengi wanakubaliana kwamba sababu zilizo hapa chini ndizo zilizosababisha kutofautiana kwao.

  

 

a)     Kupanuka Kwa Taifa la Kiislamu

 

Kutokana na kupanuka kwa taifa la Kiislamu na mabadiliko yaliyotokea kutokana na tofauti ya tamaduni, 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alikataa kukubaliana na mawazo ya Swahaba wengine. Simulizi ya Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) kusafiri pamoja na Swahaba kwenda Iraaq ni vyema kuitaja. 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) aliwaambia kwamba watu wa Iraaq sio Waarabu wanaoweza kuisoma Qur-aan vizuri. Wana sauti kama za mingurumo ya nyuki. Alieleza zaidi:

 

 

"Hivyo, msiwaweke mbali na Qur-aan kwa kufananisha tamaduni kibubusa. Kufanya hivyo kutawavunja (moyo). Isome Qur-aan vizuri na wasimulieni Hadiyth kutoka kwa Rasuli wa Allaah kila mara, na mimi ni mfuasi wenu.[6]

 

 

b)  Eneo La Mgongano Wa Mawazo

 

Sehemu ambapo masuala yanatokea ni sababu nyengine ya kutokea tofauti ya mawazo baina ya Swahaba. Mila na tamaduni za Makkah ni tofauti na watu wa Iraaq. Hiyo ndio sababu 'Umar alifanya Ijtihaad na kupingana na Swahaba wengine wa Makkah au Madiynah kwa sababu ya eneo.

 

 

Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) aliifanyia kazi Ijtihaad kwa kusimulia Hadiyth kutoka kwa Rasuli wa Allaah na ili kuaminiwa alikula kiapo. Katika jambo hilo, tunalotambua hapa ni kwamba hakukuwa na lengo la kuwaweka mbali Wairaqi na Qur-aan kwa kuwa tu haifanani moja kwa moja na tamaduni zao na kisomo chao. Hivyo, Swahaba walihitajika kuwa wakali katika kutoa Ijtihaad kwa kuegemeza ushahidi madhubuti.

 

c)   Wakati

 

Wakati unaweza kuwa sababu nyengine ya kutokea Ijtihaad tofauti. Kwa mfano, wakati wa kipindi cha vita, Qur-aan ilikusanywa pamoja kama ni kitabu kimoja chini ya uongozi wa Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) ambapo 'Uthmaan aliweza kubuni irabu za Qur-aan ili kuzuia usomaji wa makosa huku Taifa la Kiislamu likipanuka zaidi.

 

Ndani ya mifano hiyo ya Ijtihaad iliyokuwa ikifanyiwa kazi, tumeona kwamba waliifanyia kazi Ijtihaad kwa kufasiri au kufananisha matini ya Qur-aan na Sunnah. Lakini kutokana na wakati na eneo ambapo hiyo kesi imeibuka, matumizi ya Ijtihaad yalitofautiana.

 

 

d)  Ufahamu Wa Vyanzo Vikuu

 

Sababu nyengine ni uweledi wa Qur-aan na Sunnah pamoja na fafanuzi tofauti. Mfano ni suala la ugawaji wa mali ya hazina (baytul maal). Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alisema kwamba usawa katika ugawaji ni bora. Lakini Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alipingana na Ijtihaad hiyo akiwa na maoni kwamba ruzuku hiyo itolewe kwa mujibu wa haja ya mtu; kwa mfano jihaad, masikini na wale Waislamu wepya walioingia kwenye Uislaam. Hivyo, Swahaba hawa wawili walitofautiana na namna ya kugawa mali ya hazina.

 

 

'Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) aliifanyia kazi Ijtihaad pale alipoteka sehemu nyengine za ardhi kama vile Syria na Iraaq. Alitoa Ijtihaad yake kwamba ardhi hiyo isigaiwe lakini iwekwe Waqf kwa Waislamu.

 

 

Pia tunaona namna walivyotofautiana Sayyidna 'Uthmaan na 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhum). Hitilafu yao ilitokana na Ijtihaad ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba ngamia wasichukuliwe na mtu mwengine hadi afike bwana wake. 'Umar alitoa hoja kwamba ngamia hao wasichukuliwe na wala hawatapotea. 'Umar aliitumia hoja yake kwa kuwepo athari yake inayoonekana. Kwa upande wa Sayyidna 'Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) hakukubalina na Ijtihaad iliyowahi kutolewa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa sababu athari ya kutowachukua na matumizi yake hayaonekani tena. Hoja yake Sayyidna 'Uthmaan kwamba, iwapo ngamia hao wataachwa bila ya kuchukuliwa, wataibiwa. Matumizi ya matini pamoja na kutotimiza sababu ya matumizi yake hakutoi maslahi kwa jamii, ingawa matini hiyo inadhaminiwa ndani ya Ijithaad ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).[7]

 

 

Swahaba hawakuwa tu wakitumia Ijtihaad bila ya sababu za msingi. Walikuwa wakiifanyia kazi Ijtihaad kwenye kufasiri matini iwapo imeonekana na inahitaji fafanuzi na matumizi yake kwa tatizo lililowakabili.[8]

 

 

e)   Maana Tofauti Ya Matini

 

Pia tunaweza kupata sababu nyengine ya kutofautiana kwa Ijtihaad. Hii sasa inapatikana kutokana na maana tofauti ya matini. Kwa mfano neno "qur’u" ndani ya Qur-aan. Sayyidna 'Umar na Ibn Mas'uud wao wamesema kwamba ina maana ya twahara wakati Zayd ametofautiana kwa maana ya hedhi.

 

 

Hivyo, tafsiri ya neno "qur’u" linatambulika kuwa lina maana nyingi, wakati tafsiri kwa maana ya hedhi na twahara inaitwa kuwa ni Ijtihaad ya 'Umar, Ibn Mas'uud[9] na Zayd (Radhwiya Allaahu ‘Anhum).

 

 

Kutokana na hitilafu hiyo, Swahaba walitofautiana na hukumu ya kipindi cha eda cha hedhi ya mwanamke aliyeachwa. 'Umar na Ibn Mas'uud (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) waliitumia Ijtihaad katika somo hilo wakifananisha "qur’u" na twahara kuwa kipindi cha eda kinamalizika baada ya kuhitimisha vipindi vitatu vya twahara. Zayd kwa upande wake anaifasiri kumaliza kipindi cha eda kwa kuanza kipindi chake cha tatu.

 

 

Swahaba hawa watatu, wote walitoa hoja zao katika kufikia hukumu ya kisheria, ambapo ilizuka hitilafu katika maamuzi yao kutokana na ufahamu tofauti wa neno "qur’u".

 

 

Kama ambavyo tumeifasiri Ijtihaad kwa maana ya Mujtahid kuelewa hukumu ya Shari'ah na kuvitumia vipengele hivi kutokana na vyanzo vikuu ambavyo vitatoa hukumu mpya. Tunaweza kuelewa kwamba, Mujtahid yeyote alikuwa huru kutoa na kuitumia Ijtihaad. Na kwa vile ni toleo la kibinaadamu, watu waliruhusiwa kuitolea hoja. Hili liliwafanya Swahaba kutojipa hadhi ya kuifanya hoja yake kuwa yenye nguvu kuliko ya mwengine. Hivyo, hawakufungika na Ijtihaad. Kila mtu alikuwa huru kutoa Ijtihaad isipokuwa tu iwe inaenda sambamba na Qur-aan na Sunnah. Kwa mujibu wa Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), mawazo (Ijtihaad) ni maarufu baina ya Mujtahid wote. Ni ushahidi kwamba wanazuoni ama Swahaba daima walitangaza na kutambulika kwamba Ijtihaad zao zilikuwa sahihi au sio sahihi.[10]

 

 

Hitimisho

 

Swahaba kama tulivyoeleza hapo juu ni kwamba walihitalifiana kutokana na wakati na eneo. Kwa mfano Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), katika kipindi chake cha Ukhalifa hakushuhudia upanuzi mkubwa wa Taifa la Kiislamu hali ya kuwa Sayyidna 'Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) alilishuhudia hilo. Sambamba na Sayyidna 'Aliy (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), ambapo kipindi chake cha utawala kilikuja na mizozano kadhaa baina ya Waislamu wenyewe.

 

 

Pia tofauti ya kiwango cha ufahamu wa Sunnah, ambapo baadhi ya Swahaba wa Nabiy (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) walikuwa karibu naye kuliko wengine ambao walijishughulisha zaidi kuhifadhi Qur-aan ndani ya vifua vyao.

 

 

Sunnah ilikusanywa na kuwekewa kumbukumbu kwa kuandikwa. Sunnah haikuwa na maelezo ya hadhi ya maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), na kila Swahaba alitofautiana na mwenziwe kutokana na ufahamu wake. Hili lilisababisha kuwepo na kiapo wakati wa utawala wa Sayyidna 'Aliy (Radhwiya Allaahu ‘Anhu). Kwani Hadiyth zilikuwa ni nyingi mno na nyengine alisingiziwa tu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Kwa maelezo hayo, kuanzia taariykh ya Ijtihaad hadi sababu za hitilafu ya maamuzi ya Ijtihaad baina ya Swahaba. Tunaweza kutambua kwamba Ijtihaad ilikuwa muhimu wakati huu, kwani ilitoa nafasi ya fafanuzi zaidi na iliyo pana ndani ya maeneo ambayo Uislaam haukuota mizizi sana kama ilivyo kwa Makkah na Madiynah. Hivyo, kwa kutumia Ijtihaad Waislamu waliweza kuzielewa amri kwa uwazi.

 

 

Kwa vile Ijtihaad ni mawazo binafsi, haikutambulika kuwa ni miongoni mwa chanzo kikuu mwa vyanzo vya Shari'ah. Ilipewa hadhi yake ya juu iwapo Swahaba tofauti watakubaliana na Ijtihaad mpya.

 

 

Ijtihaad ilisuluhisha migogoro na kutoa mawazo bora kabisa ambayo yalirithishwa hadi kwa Waislamu wa leo.

 

 

Kwa kuwa Ijtihaad ilifanyiwa kazi, ililazimika kupitia mianya ya hitilafu lakini iliyo finyu kabisa wakati wa Khulafaau Raashiduun. Hivyo, walikhitalifiana katika maamuzi.

 

 

Kutokana na maelezo hayo juu, tunaweza kukhitimisha kwa ufupi tu kwamba sababu kuu ya kutokea hitilafu za Ijtihaad baina ya Swahaba ni elimu na wakati. Nyengine ni mawazo binafsi ya kisheria, mtindo wa kuchambua na kutoa hoja. Hizo zilikuwa ni sababu ndogo ndogo.

 

 

Kwa kweli matumizi ya Ijtihaad yalienea kwa kasi bila ya kujali mipaka baada ya kifo cha kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kuwa maeneo mepya yaliongezwa na kutekwa na kufanya Taifa la Kiislamu kukuwa zaidi.[11]

 

 

[1] Japokuwa tukio hili ambalo ni maarufu sana linatumika sana kama hoja kuu ya Ijtihaad, wanachuoni wa Hadiyth wameona kuna udhaifu wa riwaya hiyo.

 

[2] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 2.

 

[3] Dr. R. K. Sinha, The Muslim Law, Toleo La 4, Uk. 30.

 

[4] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 22.

 

[5] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 39.

 

[6] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 40.

 

[7] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 45.

 

[8] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 46.

 

[9] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 46.

 

[10] H. H. Dr Hussain, An Introduction To The Study Of Islamic Law, Uk. 42

 

[11] M. Al-Haj Ahmed, The Urgency Of Ijtihaad, Uk. 32.

 

Share