Tofauti Kuu Baina Ya Shariy'ah Za Allah (سبحانه وتعالى) Na Sheria Azitungazo Mwana-ِAadam
Tafauti Baina Ya Shariy’ah Za Allah (سبحانه وتعالى)Na Sheria Azitungazo Mwana-Aadam
Imeandaliwa na Naaswir Haamid
"Allaah Akimtakia Kheri Mja Humfahamisha
(Humpa Elimu) Kwenye Dini"
Kwa jina la Allaah Mwingi wa Rehma na Mwenye Kurehemu. Swalah na salamu ziwe juu ya kipenzi wa viumbe vyote duniani, mbora wa viumbe, Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Shukrani ni zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) (Subhaanahu wa Ta’ aalaa) na Kwake tunajitakasa na Kwake tunaomba msaada, muongozo sahihi na msamaha wa makosa yetu. Tunaomba hifadhi Kwake Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kutokana na vitimbi vya sheytan na hifadhi ya makosa ambayo tumeyatenda.
Utangulizi
Hamna shaka yoyote kuwa kuna tofauti kubwa baina ya Shariy'ah za Kiislamu na zile atungazo Mwana-Aadam. Sababu hii ndiyo inayowafanya maadui wa Uislaam kuzitaka Shariy'ah za Kiislamu ziwe ni kama za kwao. Masikio na macho yetu hayajaacha kushuhudia ni namna gani Shariy'ah za Kiislamu zinavyopingwa mbele ya wale Makafiri na hata Waislamu poa. Kwa Muislamu wa kweli anaelewa fika kuwa ni sheria za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ndizo zitampa mafanikio hapa Duniani na Aakhirah. Nimejitahidi kutoa maneno yalokuwa magumu na kutumia zaidi maneno ya Kiswahili ili makala hii iweze kusomeka na Waislamu wote. Yapo baadhi ya maneno ambayo nimeyawekea kwenye mabano kwa ueleo mzuri. Hali kadhalika nimeonelea kuonesha mifano michache kwa kutumia sheria za nchi ili kuweka wazi hoja.
Makala hii nimeigawa na kuelezea kwenye vipengele vifuatavyo:
1. Asili ya Shariy'ah za Kiislamu.
2. Shariy'ah za Kiislamu hazina tofauti ya mwanaadamu.
3. Shariy'ah za Kiislamu zinaenda na wakati.
4. Shariy'ah za Kiislamu na Allaah.
5. Sheria na mahusiano ya Wana-Aadamu.
6. Usimamizi na muundo wa sheria.
7. Adhabu (Punishment)
8. Malipo mema kwa anayejiepusha kuvunja sheria.
Baada ya kusoma makala hii, utakuwa na nafasi nzuri ya kuelewa ni namna gani Shariy'ah za Kiislamu zinamfaa binaadamu. Tofauti kuu baina ya Shariy'ah za Kiislamu na zile zitungwazo na binaadamu utapata kuzielewa na kujiweka katika ufahamu mzuri wa dini ya Kiislamu. Mwisho utakuwa na uwezo mzuri wa kuzitetea sheria hizi mbele ya wale wasiozifahamu au wale wanaozikejeli.
1. - Asili Ya Shariy'ah Za Kiislamu
Kwa dunia ya sasa na maisha yaliyotuzunguka, hapana shaka kuwa Sheria nyingi zinazotugusa ni kutoka kwa binaadamu ambazo zinaamrisha mwenendo wa binaadamu na mahusiano yake na Serikali ilokuwa madarakani. Qur-aan na mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio chanzo na msingi wa Shariy'ah za Kiislamu.
Tunaposema sheria za Uingereza, Marekani n.k ni mifano ya sheria za binaadamu. Takriban mataifa mengi, yakiwemo Tanzania, Uganda na Kenya. Ukiachilia nchi za Kiislamu, nchi nyingi zina sheria za Muingereza (Common Law). Tofauti na Shariy'ah za Kiislamu ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Sheria za duniani zinatoka kwa binaadamu ambaye ameumbwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Hivyo, sheria za binaadamu ni zenye kubadilika, wakati Shariy'ah za Kiislamu hazibadiliki kwa sababu zimewekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Tokea mwanzo wa kuumbwa mwanaadamu, ni jambo lisilopingika kuwa mwanaadamu hana ukamilifu kwenye maisha yake, ni mnyonge, asiyejitosheleza kwa nafsi yake moja. Matokeo yake ni sawa sawa na sheria zake, hazina ukamilifu wowote. Dunia inazunguka na kuendelea ndivyo sheria zake zinavyobadilika na kuhitaji mabadiliko ili ziendane na wakati. Kwa maneno mengine sheria za mwanaadamu hazina ukamilifu kwenye sehemu yoyote wala haziwezi kuwa kamili mpaka binaadamu aondokane na kasoro zote. Shariy'ah za Kiislamu zinagusa sehemu zote za maisha ikiwa ni katika uchumi, jamii, siasa au imani.
2. - Shariy'ah Za Kiislamu Hazina Tofauti Ya Mwan-Aadam
Hapana shaka kuwa binaadamu mmoja anatofautiana na mwengine, ni sababu hii imesababisha kuwepo mipaka ya nchi, tofauti ya lugha, kutofautiana kwa makabila na rangi. Ndivyo sheria za mwanaadamu zinavyotafautiana baina ya sheria moja na nyengine. Pia sheria hizi za leo ni tofauti na zile za miaka hamsini tu iliyopita.
Shariy'ah za Kiislamu zinajulikana na zitaendelea kuwa hazina mpaka (boundary) wowote wa tofauti ya wakati, taifa au sehemu anayoishi. Tuelewe kuwa mwananchi yeyote aliyekuwa chini ya Taifa la Kiislamu awe mweupe au mweusi, wa nchi yoyote, basi sheria ya mwizi (pindi ushahidi wa kweli ukithibitishwa) ni kukatwa kiganja cha mkono wa kulia, mlevi bakora 80 na mengineyo. Tofauti na sheria za binaadamu ambapo akibadili taifa na sheria zake zitabadilika.
Kwa mfano, twaelewa sote namna ya gonjwa hatari la ukimwi linavyoangamiza dunia nzima. Lakini Tanzania ipo kimya kuhusu muathirika anayetambuwa kuwa ameathirika kujamiiana na asokuwa muathirika kwa lengo la kumuambukiza gonjwa la ukimwi kwa makusudi. Hali sio hiyo kwa Afrika ya Kusini kwani sheria zao zinaruhusu muathirika wa namna hiyo kufikishwa Mahakamani. Kwa upande wa silaha za nyuklia, Marekani na Israel zimejipa ruhusa ya kutengeneza na kuhifadhi silaha hizo ilhali nchi nyengine zote yawa ni haramu kwao sio tu kutengeneza, hata kuhifadhi mali asili zinazotumika kutengenezea nyuklia kama zebaki “mercury”. Pia vitendo vya liwaati vimezuiwa Zanzibar (kifungu namba 150 cha Sheria ya Jinai namba 6 ya mwaka 2004). Wakati sheria za Magharibi sio tu zinaruhusu maingiliano haya machafu, hata ndoa zafungwa baina ya watu wa jinsia moja.
Hivyo, ni kusema Tanzania inaruhusu kuambukizana ukimwi wakati Afrika Kusini inazuia. Israel na Marekani wanaruhusa ya kutengeneza nyuklia ilhali nchi nyengine ni kosa. Liwaati ni kosa ndani ya Zanzibar wakati nchi za Magharibi zinaruhusu.
Tofauti na Uislaam, Sheria ipo wazi kuhusu muathirika kumuambukiza mwengine kwa lengo la kupata maradhi ateseke na mwisho kufariki kifo kibaya. Uislaam unasema anayeua nafsi moja ni sawa na kuua nafsi zote. Pia ipo Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema “Aliye na maradhi asimuambukize asiyekuwa nayo.” Kwa upande wa nyuklia, ni sawa tunasema mtu ajihami na kumruhusu kukaa nazo lakini nyuklia zina hatma mbaya. Sadd Adh-Dharai ni sheria inayozuia halali ambayo inaweza kuleta athari ya haramu. Sheria inayofafanua mwenendo wa maisha ya Muislamu (MajAllaah Al-Ahkaam Adaliyah) Kifungu 30 pia chaeleza Sadd Al-Dharai. Haramu hii ni mfano wa ile tuipatayo juu ya ulevi, kwani ina manufaa lakini ni finyu ukilinganisha na athari zake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anasema:
يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ ۖ قُلْ فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ
Wanakuuliza kuhusu pombe na kamari. Sema: Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. Na dhambi yake viwili hivyo ni kubwa kuliko manufaa yake.. [Al-Baqarah: 219]
Hivyo nyuklia inafanana na kesi ya ulevi na hivyo kuwa ni haramu. Ama kuhusu liwati, hamna mjadala kuwa ni haraam na itafika Qiyaamah, liwaat itabaki kuwa ni haraam. Liwaat ni katika dhambi kubwa ndani ya Uislaam na katu haikubaliki kwa jamii. Sheria zote hizi hazitakuwa na mabadiliko ndani ya Uislaam kwa sababu Allaah ni Mmoja na Sheria Zake ni hizo hizo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:
أَئِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ وَتَقْطَعُونَ السَّبِيلَ وَتَأْتُونَ فِي نَادِيكُمُ الْمُنكَرَ ۖ فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَن قَالُوا ائْتِنَا بِعَذَابِ اللَّـهِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٢٩﴾
Je, nyinyi mnawaendea wanaume na mnawaibia (na kuwaua) wasafiri, na mnafanya katika mikutano yenu munkari? Basi halikuwa jawabu la watu wake isipokuwa kusema: Tuletee adhabu ya Allaah ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli. [Al-Ankabuwt: 29]
Je, hamna mtu asiyejua nini kiliwafika watu wa Nabiy Luwt (Alayhis-salaam)?.
Sheria kuu za Kiislamu ambazo zinapatikana ndani ya Qur-aan imechukua sifa Yake Allaah, imehifadhiwa tokea mwanzo wa kushushwa hadi leo na mpaka siku ya Qiyaamah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema na tutajaribu kutafsiri kama ifuatavyo:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾
Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka ndio Wenye kuihifadhi. [Suratu Al-Hijr: 9]
Hapana shaka kuwa Qur-aan tuliyonayo leo ni kitabu hichi hichi alichoshushiwa Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Ummah wake wote. Sheria hizi zilizowekwa kutoka Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) zinadhihirisha sifa Zake Rabb ambazo hazina doa, Mwenye kuishi daima, Hakimu wa Mahakimu, Mfalme wa Wafalme na sifa zengine nzuri nzuri. Sifa hizi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anazo kabla, leo na mpaka Qiyaamah. Ni sifa hizi tuzipatazo kwa Qur-aan isobadilika na kwa Shariy'ah za Kiislamu zisotaka mabadiliko yoyote!
Kwa hiyo sheria za binaadamu ni kanuni zinazotungwa kwa ajili ya kuitengeneza vizuri jamii ili kutimiza matakwa ya hiyo jamii husika. Sheria za binaadamu zinatungwa kutokana na matatizo yanayojitokeza ndani ya jamii. Mahitaji ya jamii yenye kubadilika kutokana na yeye binaadamu kuwa na mabadiliko ndio sababu ya sheria za binaadamu. Jamii inaendelea, ndivyo sheria zinavyobadilika. Hivyo, sheria za binaadamu haziishi maisha ya milele, bali zinazaliwa na kufa. Kutokana na sababu ya wakati, sheria za mwanaadamu zinakwisha muda (expire). Hapa tunaona kuwa sheria za mwanaadamu zinatengenezwa kutokana na mahitaji ya jamii na kwa ajili ya muda fulani na baada ya muda huo kupita na jamii kubadilika kutokana na sheria hizo basi sheria hizo huwa sawa na takataka zitakiwazo kutupwa jalalani.
Kwa mfano sheria ya makosa ya Jinai ya Zanzibar namba 13 ya mwaka 1934 inaruhusu adhabu ya viboko. Adhabu hii imefutwa mwaka 2004 (Kifungu namba 26 ya sheria namba 6 ya mwaka 2004 – Sheria ya Makosa ya Jinai ya Zanzibar) Hivyo ni kusema sheria hii imezaliwa 1934, imeishi na kufa mwaka 2004. Adhabu zinazokubaliwa kwa sasa ni kama faini, kifungo cha jela na nyenginezo.
Tofauti na Uislaam, kwa mfano sheria ya mzinifu asoowa/kuolewa atatumikia mijeledi mia moja. Haitobadilika sheria hii mpaka Qiyaamah kisimame hata ikiwa Waislamu poa hawaitaki hata kuisikia. Ile dhana za zinaa kamwe hazijabadilika ila huongezeka. Uislaam umeliona hilo ndiyo maana sheria hiyo inadumu. Mwanadamu ana kasoro zake na huona yale madhara ndiyo faida. Mwanaadamu anaivamia zinaa akidhani ina manufaa ila haina hiyo zinaa ila madhara matupu tena ya kuangamiza. Matokeo ya kukataa kufuata Shariy'ah za Kiislamu ni kujiangamiza. Shariy'ah za Kiislamu zinamzuia mwanaadamu asijiangamize. Ni dhambi kubwa mtu kujiingiza katika hilaki yeye mwenyewe kwa mwenyewe.
3. - Shariy'ah Za Kiislamu Zinaenda Na Wakati
Dalili zinaonesha kuwa Shariy'ah za Kiislamu ni za milele na hazihitaji marekebisho na wala marekebisho hayahitajiki kwa Shariy'ah za Kiislamu. Shariy'ah za Kiislamu zimewekwa kurekebisha tabia na matatizo ya jamii ya binaadamu kwa muda wote ambao atajaaliwa kuishi ndani ya dunia hii. Ingawa Shariy'ah za Kiislamu msingi wake ni Qur-aan na isiyohitaji mabadiliko, lakini sheria hizi za Kiislamu zinaweza kuendelezwa na kupatiwa ufumbuzi wa mambo ambayo yana khitilafu ndogo ndogo. Hii ni kwa kutumia vipengele vya Fiqhi kama Qiyaas (ufumbuzi), kauli za Swahabah, Sadd Al-Dharai (kuharamisha halali inayopelekea kwenye haramu) na nyenginezo.
Kwa mfano asili ya kuharamishwa ulevi ni kuwa na athari mbaya kwa jamii, lakini Qur-aan imezungumzia kinywaji cha ulevi na sio kuhusu madawa ya kulevya kama kokeni na bangi. Hapa tunatumia Qiyaas ili kupata hukmu yake na kuona kuwa nayo pia yana athari mbaya kwa jamii, hivyo kila chenye madhara ni haramu. Na kupata hukmu ya madawa ya kulevya kuwa ni haramu pia.
Itambulike kuwa vipengele hivi (mfano Qiyaas, Sadd Al-Dharai, kauli za Swahaba na kadhalika) vyote vya Fiqhi vinapitia msingi wa sheria ya Qur-aan ama Sunnah. Ikiwa Qur-aan au Sunnah imetoa hukmu, hamna sheria nyengine itakayotolewa ufafanuzi. Na wala isiwe sheria itokanayo na fiqhi haramu inayohalalisha au halali inayoharamishwa. Kwa mfano kuhalalisha kutovaa Hijabu kwa mwanamke au kuharamisha Zakaah.
Mfano mzuri ni kuhusu mjadala wa Hijaab. Kwani Hijaab ina nafasi kubwa katika hukmu za Kiislamu. Lakini Dkt. Zaki Badawi (mwanazuoni wa Kiislamu aliyekuwa Uingereza) ameruhusu wanawake kutovaa hijaabu kwa kuwa hijabu inamfanya adhuriwe kama vile kutukanwa, kusumbuliwa na hata kuvamiwa. Dr. Badawi ameghafilika na kusahau Quran (Suwraah An-Nuwr: 31 na Suwraah Al-Ahzab: 59) kuwa hijabu ni lazima na wala sio Sunnah. Kisingizio cha kukejeliwa wanaovaa hijab sio sahihi kwani Waislamu waliopita walikashifiwa zaidi ya haya lakini sheria zilibaki kama zilivyo.
Hivyo, Shariy'ah za Kiislamu ni zenye kwenda na wakati, kwani sheria kuu za Kiislamu zipo kamili na mawazo ya kisheria (Fiqhi) yapo wazi kutumika.
Shariy'ah za Kiislamu zinatofautiana baina ya mwanazuoni mmoja na mwengine tu. Tunaposema Qur-aan na Sunnah ni vyanzo vya sheria, tunakusudia kusema kuwa hivi ndivyo vyanzo na dalili kuu zinazofuatwa na kupatiwa ufumbuzi ikizingatiwa kufuata kanuni zinazohusika katika kutoa ufumbuzi kwa suala la Kiislamu.
Kanuni hizi za Kiislamu hazipatikani isipokuwa kwenye vyanzo vikuu. Hii ndio tofauti kubwa na sheria zenginezo. Kwani sheria za mwanaadamu zinatokana na akili yake mwenyewe, akija mmoja ataweka sheria hii na akiingia mwengine madarakani atazibadilisha. Anavyoamka ndivyo anavyotunga sheria. Shariy'ah za Kiislamu zimeshushwa zaidi ya miaka 1441 iliyopita. Tokea muda huo, binaadamu anajulikana kubadilika kiakili, muundo na maendeleo. Watu wa kale hawakuweza hata kuota uvumbuzi usioingia akilini kutoka katika Shariy'ah za Kiislamu. Adabu za binaadamu zimeelezwa humo na matawi mengi tu ya elimu yametokana na hiyo Sheria kuu ya dunia.
Ama kwa binaadamu, huweka sheria kwa ajili ya kutawala muda mchache unaomzunguka akiangalia matakwa yake na jamii kuwa ujumla. Juu ya kubadilishwa na kutiwa viraka sheria hii, haijawa mfano hata chembe, mbele ya Shariy'ah za Kiislamu ilhali sheria hizi zinatungwa mpya. Lakini ile kongwe (Sheria ya Kiislamu) ipo imara na katu haihitaji viraka na wala haitohitaji viraka. Ukiangalia na kuisoma Sheria ya Kiislamu utakutia bado binaadamu hajafikia mambo yote yaliyotajwa, hivyo kuifanya kwenda na wakati. Kwa mfano ujio wa Nabiy ‘Isaa (‘Alayhis-salaam) kabla ya Qiyaamah, ni nani ajuaye lini atafika duniani? Ni Qur-aan tu iliyoeleza haya! Bado wakati wake tu kufika. Ni hivi karibuni tu imegundulika kuwa ni dunia inayozunguka jua na sio jua kulizunguka dunia. Qur-aan imetaja hili miaka 1441 iliyopita. Mfano mwengine ni kugundulika upulizwaji wa roho kwa kiumbe kilicho ndani ya tumbo la mama kabla ya kuzaliwa, wanasayansi wasiokuwa na ujuzi wa Qur-aan bado wanashikilia kusema kuwa kiumbe kinakuwa hai tokea pale yanapotoka manii. Hii sivyo kwa elimu sahihi ya Uislaam kwani tunafundishwa kuwa linakuwa ni pande la nyama tu (sio kiumbe hai), na hupuliziwa roho baada ya miezi minne tokea mimba inapotungwa.
Imepokewa kutoka kwa [Bukhari na Muslim], kutoka kwa Abdillahi bin Masu’ud (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kutokana na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “(Hakika mmoja wenu linakusanywa umbile lake ndani ya tumbo la mama yake kwa siku arobaini kuwa ni tone (nutfaa), kisha linageuzwa kuwa pande la nyama (‘alaqatah) mfano wa hizo (siku), kisha linakuwa mifupa mfano wa hizo (siku), kisha anateremshwa juu yake malaika, anampulizia ndani yake roho…)” Amesema kweli Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.
Shariy'ah za Kiislamu sio zenye kubadilika ukilinganisha na za binaadamu ambazo zinabadilishwa kuanzia sheria ndogo mpaka Katiba. Kwa mfano ili kuingiza siasa za sasa (demokrasia) inabidi Katiba ibadilishwe kuruhusu vyama vingi. Historia ya Uislaam umeruhusu changamoto inayoanza kutoka Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa) dhidi ya Ibilisi. Kisha kumuachia ibilisi akawa na sifa ya kuishi, kutembea ndani ya mishipa ya damu ya mwanaadamu. Akimuachia mwanaadamu aamue mwenyewe pa kufuata (ama Allaah (Subhanahu Wataala) au Ibilisi). Siasa ya Uislaam iliendelea hata kwa Swahaba baada ya kufa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Historia ya Kiislamu inaonesha kuwa baada ya kufa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Waislamu walichagua Khalifa (kiongozi) wa mwanzo msikitini, walitumia haki yao kwa kwenda kumpa mkono (kura) Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kuonesha kuridhika naye kuwa ni Khalifa wao. Hakuingia madarakani Sayyidna Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwa nguvu au kujipigia kampeni na propaganda. Hataaa! Njia ya Baya’h (kupiga kura) ilitumika.
4. - Shariy'ah Za Kiislamu Na Muumba (Allaah)
Mazingatio makuu ya Sheria ya Kiislamu ni kuweka uhusiano imara baina ya Allaah na kiumbe. Kwa mfano Swalah, Zakaah, kufunga Ramadhwan ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) peke Yake tu na kumuabudu Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa.) Yeye ndie Mtoa Sheria, Anaamrisha binaadamu kufanya au kujizuia kufanya kitu kwa ajili ya kuwa karibu na Allaah na wakati huo huo kulinda haki yake mwanaadamu na viumbe wengine. Kwa mfano tunazuiwa kuzini, kuiba, kuua, kuharibu mazingira n.k ili kulinda cheo cha binaadamu pamoja na kulinda haki za binaadamu na viumbe wengine. Tofauti na sheria za binaadamu ambapo mazingatio yake makuu ni kutofautisha dini na sheria. Ni kusema kuwa sheria za mwanaadamu haiweki kanuni na mahusiano baina ya watu au watu na Serikali yao. Lakini sheria ni sehemu ya dini ndani ya Uislaam. Uislaam unaweka kanuni baina ya binaadamu na Allaah wake na wakati huo huo ukiwekwa uhusiano mzuri baina yake na watu wengine, tofauti na sheria za binaadamu ambazo zinaweka mahusiano baina ya watu tu.
Hapa lazima tukumbushe kuwa mwanaadamu ametunga sheria za kulinda wanyama na mazingira. Sio kwa ajili ya hao wanyama au mazingira, bali kuharibiwa kwake kunaathiri maisha ya mwanaadamu na uhai wa dunia kwa ujumla. Uislaam umeenda mbali na kusema kila kiumbe (hata jua ni kiumbe) kina haki ya kuishi na kutumiwa kulingana na mafundisho sahihi ya dini.
5. - Sheria Na Mahusiano Ya Wanaadamu.
Wamejiwekea wanaadamu sheria zinazoeleza mahusiano baina ya watu “tort.” Sheria hizi hazina uhusiano wa maadili, msingi mkuu wa sheria hizi “tort”) ni kutoka kwa aliyevunjiwa hizo sheria na wala sio Serikali.
Kwa upande wa Uislaam, kiini kikuu cha mahusiano ya wanaadamu ni kutoka kwenye Qur-aan ambayo inakataza dhana mbaya, kupeleleza na kusengenya. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾
Enyi walioamini! Jieupusheni sana na dhana kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msifanyiane ujasusi, na wala wasisengenyane baadhi yenu wengineo. Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa? Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah! Hakika Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Hujuraat: 12]
Hivyo, sio tu sheria ya Kiislamu inakataza mahusiano mabaya baina ya wanaadamu bali inaeleza kwanini asifanye hivyo na kutolea mfano ni namna gani lilivyo hilo kosa kuwa ni kubwa. Hapa tumeoneshwa kusengenya ni mfano wa kula nyama ya ndugu yako tena aliye maiti. SubhaanAllaah!
Baadhi Tu Ya Kasoro Juu Ya Sheria Hizi Ni Kama Ifuatavyo:
Hazielezi “tort” ni kwa nini mwananchi asikiuke hizo sheria. Bali zinamzuia na kumlazimisha tu kufuata hiyo sheria. Kwa mfano asiwashe redio sauti kubwa hadi kumuudhi jirani. Akiwa hayupo jirani? Ni ruhusa kuwasha? Je wapita njia? Ndege warukao? Haki za majini na malaika zipo hapa? Majibu yote utayapata kuwa sheria za mwanaadamu hazina mazingatio kwa viumbe vyote. Zinagusa sehemu chache tu ya vitu.
Kasoro nyengine ni kuwa hazifikishwi Mahakamani kuvunjwa kwake ila mpaka aliyekosewa afunguwe kesi kwa gharama zake mwenyewe. Serikali haina mkono wake kwenye kesi hizi. Hii ni kwa sababu sheria za mwanaadamu hazitaki kujiingiza kwenye mahusiano haya wala hazigusi maadili. Tofauti na Uislaam, umegusa kila nyanja ya maisha ya mwanaadamu. Katu Taifa la Kiislamu haliruhusiwi kukimbia majukumu kwani sheria zote zinatoka kwa Mkuu wa Serikali zote duniani, naye ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
6. - Usimamizi Na Muundo Wa Sheria.
Tofauti nyengine inahusiana na usimamizi na namna zinavyoundwa hizo sheria.
Kawaida, jamii fulani inaunda sheria zake kwa ajili ya kutawala jamii husika na kuilinda. Mfano Hitler alipoingia madarakani alipitisha sheria ya kuuawa kwa Mayahudi wote ilimradi tu kulinda maslahi ya wajerumani walio wengi ndani ya Ujerumani. Alipoondoka madarakani sheria hii ikafa. Ama kwa Sheria ya Kiislamu, sio ya jamii fulani pekee. Inagusa ulimwengu mzima hata kwa wasio Waislamu. Kwa mfano kuna sheria baina ya taifa la Kiislamu linavyoishi na wasio Waislamu (Dhimmi). Muislamu hatakiwi kuimwaga damu ya binaadamu hata awe Dhimmi bila ya sababu. Ni dhambi kubwa kuimwaga damu ya Muislamu bila ya sababu yoyote. Maingiliano baina ya Waislamu na wasio Waislamu, uchumi wa Kiislamu na siasa za Kiislamu ni vipengele vilivyokuwa huru kutumiwa na walimwengu wote kwani kuna faida kubwa. Ikiwa ni Muislamu au sio Muislamu. Sheria ya Kiislamu ni ya ulimwengu mzima na watu wake wote. Tofauti na sheria za binaadamu ambazo haziwezi kwenda pamoja na maendeleo anayofanya mwanaadamu duniani. Ni lazima zitabadilika tu.
Dhumuni kuu ya Sheria ya Kiislamu haikufungwa kuzunguka jamii pekee. Bali kumpa haki kila mmoja, kuunda jamii yenye tabia nzuri, taifa imara na mwisho kuifanya dunia sehemu inayofaa kuishi kwa mazingira yake mwenyewe binaadamu.
7. - Adhabu (Punishment)
Adhabu za Sheria ya Kiislamu pia ni tofauti na sheria za mwanaadamu. Hakika haitakuwa sheria ikikosa adhabu, na kama sheria itakosa adhabu ni sawa na msumeno usokuwa na meno (makali) au kisu butu. Ingawa zote zinawaadhibu wanaokiuka hiyo sheria, lakini bado tofauti ipo.
Kabla ya kuendelea mbele, lazima tuelewe kuwa Uislaam umeletwa kwa wanaadamu wote. Hivyo kukataa kufuata Uislaam hapa duniani na kuabudia asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi hilo pia ni kosa.
Sheria ambazo atakiuka Muislamu ataadhibiwa Qiyaamah na mara nyengine sheria inaruhusu kuadhibiwa duniani na Qiyaamah pia. Kwa mfano shirk, khadaa ya kujifanya umefunga, kibri, riyaa na dhambi nyenginezo ambazo haziwezi kuonekana ila kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) zitaenda kuadhibiwa Qiyaamah, hii ni kwa sababu zinafanywa kupitia ndani ya nafsi ya mwanaadamu. Ni Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) pekee mwenye uwezo wa kuona kinachopita ndani ya nafsi. Kwa nini tuseme hivi?
Chukua mfano wa Marekani akirusha roketi kwenye mwezi, hakika haitoachiwa kwenda tu yenyewe, bali itakuwa inarikodi na kuangaliwa huku duniani kila hatua inayokwenda na namna mashine yake inavyofanya kazi. Pia “black box” kwa upande wa ndege “aeroplane” inarikodi hata mazungumzo ya pilot, na ndio maana ndege inapopata ajali kwanza hutafutwa hiyo “black box”. Hivyo kila mtengenezaji hukijua vizuri mwenendo wa anachotengeneza, na hamna mwengine wa kujuwa nafsi ya mwanaadamu ila Muumba Subhaana.
Na kwa mfano wa adhabu zinazoweza kuthibitika duniani ni zinaa, wizi, ulevi na mengineo ambayo mkosaji anaweza kutiwa hatiani tofauti na yale makosa yalokuwa yanapita ndani ya nafsi.
Pia Uislaam utamuadhibu mtenda dhambi aliyekuwa hajatiwa hatiani hapa duniani. Mfano wanaokiuka kutoa Zakaah, ingawa anaweza kufoji karatasi na kusema uongo ili tu kukwepa kutoa Zakaah hapa duniani lakini ataenda kuilipa huko Qiyaamah. Hamna kukimbia kosa ndani ya Uislaam, limetendwa basi litahesabiwa tu mbele ya Allaah. Mfano mwengine ni makafiri walokataa kufuata Uislaam. Pia nao wana hukmu zao siku ya Haki.
Tofauti na sheria za mwanaadamu ambazo zinamuadhibu mkosaji duniani pekee. Na ikiwa mwanaadamu atakwepa mkono wa sheria hadi kufa hatahisabiwa katu kuwa ni mkosaji. Uislaam unamkamata mkosaji duniani na kama hatakamatwa basi adhabu ipo siku ya Qiyaamah. Sheria ya Kiislamu inawafanya Waislamu kuwa makini muda wote kutokiuka sheria za dini.
8. - Malipo Mema Kwa Anayejiepusha Kuvunja Sheria
Juu ya hayo, Uislaam unatoa malipo kwa mtiifu na adhabu kwa mtenda dhambi. Hivyo, Shariy'ah za Kiislamu zinawakamata wote ikiwa ni mtiifu au ni mtenda makosa. Shariy'ah za Kiislamu zinalinda kanuni zake na zinawalazimisha binaadamu kujisalimisha nazo sio kwa kuweka adhabu tu bali hata kwa kutoa malipo mazuri kwa mwenye kuzifuata. Ambapo sheria za mwanaadamu zinamuadhibu mkosaji na wala hazitoi zawadi kwa anayezifata. Jee tumepata kusikia Raisi/Hakimu akitoa zawadi kwa mwananchi aliyejiepusha kuiba hadi uzee umemfikia? Hapa sio mzee aliyeiba lakini hakukamatwa, tunazungumzia mzee aliyekuwa mswaafi wa matendo tokea kuzaliwa kwake.
Kwa mfano dhambi ya kuua mtoto, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anasema:
وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلَاقٍ ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُمْ ۚ إِنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْئًا كَبِيرًا ﴿٣١﴾
Na wala msiue watoto wenu kwa kukhofia ufukara. Sisi Tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua imekuwa ni hatia kubwa. [Al-Israa: 31]
Hivyo binaadamu anayeacha kumuuwa mtoto wake anaahidiwa kuruzukiwa yeye na mtoto wake.
Ni Rehma Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuweka malipo hata kwa jambo la kutosheleza shahawa za binaadamu kwa njia ya halali. Hili sio tendo jengine ila ni tendo la ndoa baina ya mume na mke nalo pia lina ajira ndani yake.
Imepokewa na Muslim kutoka kwa Abi Dharr Al-Ghaffarriy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu Alayhi Wasalam) amesema: “Hakika ya tasbihi ni sadaka, na kila takbira ni sadaka, na kila shukrani ni sadaka, na kila tahliyl ni sadaka, na kuamrisha mema ni sadaka, na kukatazana maovu ni sadaka, na kumuingilia mmoja wenu ni sadaka”. Wakasema Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum), Je kumuendea mmoja wetu kwa kuondoa shahawa, pia ndani yake kuna malipo? Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Je, anaonaje kama ataendea tendo hilo katika haramu, halitakuwa dhambi?….Na hivyo basi, likiendewa kwa uhalali, lina malipo”.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) pia Anatoa malipo kwa wamchao Allaah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ مَفَازًا ﴿٣١﴾حَدَائِقَ وَأَعْنَابًا ﴿٣٢﴾وَكَوَاعِبَ أَتْرَابًا ﴿٣٣﴾وَكَأْسًا دِهَاقًا ﴿٣٤﴾لَّا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا كِذَّابًا ﴿٣٥﴾جَزَاءً مِّن رَّبِّكَ عَطَاءً حِسَابًا ﴿٣٦﴾
Hakika wenye taqwa watapata mafanikio. Mabustani na mizabibu. Na wanawake wenye vifua vya kujaa wa hirimu moja. Na kikombe kilojaa pomo mvinyo. Hawatosikia humo upuuzi na wala kukadhibisha. Jazaa kutoka kwa Rabb wako, tunukio la kutosheleza. [An-Nabaa: 31-36]
Shariy'ah za Kiislamu zinagusa nyanja zote muhimu za maisha, roho, usalama, amani na heshima. Kwa vile kuna malipo mazuri kwa mwenye kushikamana nazo, basi hakika ni kivutio kwa mwenye kushikamana nazo. Vitu hivi vyote vinakosekana kutoka sheria za mwanaadamu. Kwa sababu kushikamana kwa Shariy'ah za Kiislamu ni kitendo cha utiifu na kujitoa mhanga kwa ajili ya Allaah, utiifu ambao unamweka karibu na Muumba wake.
Ikiwa kanuni zimeegemea kwa dini na kujilinda nazo, mwanaadamu yoyote atahofia adhabu zake hata kama sheria za mwanaadamu hazitamtia hatiani. Mfano, Uislamu unaamrisha kuwa msafi na kuweka mazingira safi. Hivyo kiimani tunajuwa kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) anatuona, hivyo hata ukiwa pwani hutokaa ukatupa uchafu ndani ya bahari (kwani kutaathiri viumbe baharini) seuze kwa kutupa uchafu duniani. Hii ni kwa sababu ya “mkono wa sheria” chini ya Utakaso Wake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ambao hautegemei kukamatwa mtuhumiwa wala kushitakiwa kabla ya Mahkama za sheria. Hakuna njia ya kukimbia mtenda dhambi asotubia ila atahukumiwa tu.
Kwa kumalizia makala hii, majumuisho yafuatayo yanatolewa kwa tofauti kuu mbili baina ya sheria hizi:
Kwanza, kiini cha Sheria ya Kiislamu ni kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Kwa upande wa sheria za mwanaadamu zinatokana na akili za binaadamu. Sheria na adhabu zake ndani ya Uislaam zinapatikana kwenye viini vikuu: Qur-aan na Sunnah. Fiqhi hutumika kutoa ufumbuzi wa jambo kutoka Qur-aan na Sunnah. Utawala wa Taifa la Kiislamu hauruhusiki kuharamisha halali iliyobainishwa chini ya Muumba wala kinyume chake. Halali, haraam na adhabu zake ni vitu vinavyozuiwa kwa hali zote.
Pili, maadili ndani ya Shariy'ah za Kiislamu yana nafasi muhimu. Wakati sheria za mwanaadamu inakataa kabisa maadili na haijishughulishi nayo. Uislaam unachukua maadili ni asili ya dini, hakuna mtengano wowote.
Kwa mfano, muislamu anawajibu wa kuwatumikia vizuri wazee wake bila ya hata kusema “Ah!” na wazazi wakifika uzee basi ukae nao kwa wema. Sheria ya mwanaadamu haina kanuni kama hiyo. Au kwa mfano mwengine ni mwanamke anayevaa hijaabu vizuri, sio kwamba ndio amemaliza sheria zote za dini. Na haimlazimu mwanamke huyu kuswali, hataa. Hapa Uislaam unagusa maadili (kuvaa hijabu) na kuswali, (sheria) zote zafuatwa bila ya kuacha nyengine.
Fikra ya kuwa sheria ni upande mmoja na maadili upande mwengine ni kosa. Mtengano huu hauna nafasi ndani ya Uislaam kwani unaweza kusababisha kutokea kwa watu wa aina mbili ambao wote hawataweza kukubalika. Kwa mfano:
Wa mwanzo ni mtu mwenye maadili mabaya lakini ni mzuri wa kufuata sheria. Mfano kutowatumikia vizuri wazee lakini hana chembe ya uzinifu.
Wa pili ni mfuataji mbaya wa sheria lakini anajionesha kwa watu kutenda mema. Mtu huyu hana tofauti na Mnafiki. Hivyo huwa anachanganya mambo tu, huku yupo na kule yule. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) amemwita mtu kama huyu kwa jina la Mudhabdhabiyna. Mfano anatoa hukumu ya waliodhulumiana hali ya kuwa yeye mwenyewe ni mdhulumu mkuu.
Mifano hii inadhihirisha ya kuwa upande wa sheria za mwanaadamu huangukia baina ya pande hizo mbili. Binaadamu anajizuia kuiba kwa sababu tu ni kosa mbele ya sheria lakini hatoi kipato chake kuwasaidia masikini kwa sababu sheria haijashurutisha hivyo. Na kwa upande wa pili unamkuta mtu ameamua kuvunja sheria na kuanza kuiba lakini anatoa mali yake kuwasaidia masikini.
Pia tunaona sheria za mwanaadamu zinazuia wari/wajane kupata mimba lakini haiwazuii kufanya tendo la ndoa (Sheria ya Kuwalinda Wari na Wajane Namba 4 ya mwaka 1985 kifungu cha 3 – Zanzibar). Kwa sababu kujamiiana ni tendo linalogusa maadili na sheria za mwanaadamu hazijishughulishi na vitu vya maadili kama kujamiiana wasokuwa wanandoa, kutembea utupu wanawake, kuchanganya mavazi baina ya mwanaume na mwanamke na mengineyo.
Tunamuomba Allaah Subhaanahau wa Ta’aalaa Atuhifadhi na makosa, Atupe malipo kwa amali zetu njema. Atuepushe na elimu isiyokuwa na manufaa. Tunamuomba Atuthibitishe katika itikadi hii na Atuonjeshe matunda Yake na Atuongezee katika fadhila Zake na Asizipoteze nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na Atumiminie Rehma kutoka Kwake kwani Yeye ndiye Mpaji.
Shukrani zote ni Zake Yeye Mola wa ulimwengu, na viumbe vyote vya dhahir na siri. Rabb wetu Msalie na Mpe Amani Nabiy wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Swahaba wake na Aali zake wema, na kila atakayewafuata kwa wema na uongofu mpaka Siku ya Kiama. Kwake Yeye Allaah twajitakasa na Kwake twaomba Atutakabalie dua zetu.
Amiyn
Marejeo:
§ Britanic Encyclopaedia Vol Xxii
§ Dr. H. H. Hussain, An Introduction To Islamic Law.
§ H. P. Thomas, Dictionary Of Islam, Adam Publishers And Distributors, India (1998)
§ J. J. Mohammed, Introduction To Islamic Law, International Islamic Publishers (1989
§ Nyanzi, Islamic Jurisprudence
§ Q. Abdul-qadir, Criminal Law Of Islam, Vol. I
§ Q. Abdul-rahman, Criminal Law Of Islam, Vol. I
§ Sh. Muhammad Ahmad Kan’ani, Usul Al-maasharatu Zawjiyah (misingi Ya Maisha Ya Ndoa).
§ Sheria Ya Kuwalinda Wari Na Wajane Ya Zanzibar Ya Mwaka 1985.
§ Tafsiri Ya Qur-aan Kwa Lugha Ya Kiswahili,
§ Zanzibar Penal Act No. 6 Of 2004