03-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Nani Ahlul-Bayt

 

Nani Ahlul-Bayt?

 

 

Mojawapo ya hitilafu kubwa baina ya Sunnah na Shia ni juu ya tafsiri ya neno 'Ahlul Bayt'. (Watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Wakati Shia wanasema kuwa Ahlul Bayt ni ‘Aliy bin Abi Twaalib na Faatwimah binti Muhammad na wanawe (Radhiya Allaahu anhum) peke yao, Ahlus Sunnah wanaitakidi kuwa Ahlul Bayt ni wote hao waliotangulia kutajwa pamoja na wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na binti zake waliobakia wasiotambuliwa na Shia, na pia wajukuu zake na baadhi ya waliohusiana naye katika ukoo wake.

Imeandikwa katika kamusi maarufu "Lisaanul Arab" kuwa; mke na jamaa za mtu ni Ahli Bayti yake.

Na katika Qur-aan tukufu, Allaah Anawataja wake wa mtu kuwa ni Ahli yake.

Allaah Anasema:

 

قَالُواْ أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللّهِ رَحْمَتُ اللّهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَّجِيدٌ

 

"Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Allaah? Rehema ya Allaah na baraka Zake ziko juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye ndiye Msifiwa wa kutukuzwa." Huud-73

 

Maulamaa wote wanasema kuwa neno (Watu wa nyumba), katika aya hii anakusudiwa Sarah mke wa Nabii Ibraahiym ( ‘Alayhis Salaam).

 

Na Akasema:

إِذْ رَأَى نَارًا فَقَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا

 

"Alipouona moto, akawaambia watu wake (Ahli yake): Ngojeni! Mimi nimeuona moto." Twahaa-10

 

Inajulikana hapa pia kuwa neno (Ahli yake) anakusudiwa mke wa Nabi Musa (Alayhis Salaam) aliyekuwa amefuatana naye katika safari hiyo.

 

Na Allaah Akasema pia:

 

قَالَتْ مَا جَزَاء مَنْ أَرَادَ بِأَهْلِكَ سُوَءًا إِلاَّ أَن يُسْجَنَ أَوْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

 

 "Hapana malipo ya mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipokuwa kufungwa au kupewa adhabu iumizayo." Yuusuf-25

Neno (Ahlika katika aya hii) na maana yake ni 'mkeo' aliyekusudiwa ni mke wa Al-Aziz.

 

Kwa hivyo dalili zote zinaonyesha kuwa neno Ahlul Bayt au Ahl linatumika zaidi kwa maana ya mke.

Na katika Surat Al-Ahzaab kuanzia aya ya 28 hadi ya 33 Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا، وَإِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا

 

"Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni, nitakupeni kitoka nyumba, na kukuacheni mwachano mzuri.

 

Na ikiwa mnamtaka Allaah na Mtume Wake na nyumba ya Akhera, basi Allaah Amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa."

 

يَا نِسَاء النَّبِيِّ مَن يَأْتِ مِنكُنَّ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ يُضَاعَفْ لَهَا الْعَذَابُ ضِعْفَيْنِ وَكَانَ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرًا، وَمَن يَقْنُتْ مِنكُنَّ لِلَّهِ وَرَسُولِهِ وَتَعْمَلْ صَالِحًا نُّؤْتِهَا أَجْرَهَا مَرَّتَيْنِ وَأَعْتَدْنَا لَهَا رِزْقًا كَرِيمًا

 

"Enyi wake wa Nabii! Atakayefanya uchafu dhaahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Allaah ni mepesi.

Na miongoni mwenu atakeyemtii Allaah na Mtume Wake, na akatenda mema, tutampa malipo yake mara mbili, na tutamwandalia riziki ya ukarimu."

 

يَا نِسَاء النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاء إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفً

 

"Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema."

 

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَى وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُم تَطْهِيراً ْ     

 

"Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na shikeni Swalah, na toeni Zakaah, na mtiini Allaah na Mtume Wake. Hakika Allaah anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba (ya Mtume), na kukusafisheni baarabara."

 

Ahlus Sunnah wanasema kuwa; kama vile katika aya zote zilizotangulia, kila anapotajwa Ahli ya mtu hukusudiwa mke, na katika aya hizi pia Allaah Anapotaja Ahli Anawakusudia wake zake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Ukizisoma kwa utulivu aya hizi utaona kuwa kuanzia aya ya 28 Allaah Anazungumza na wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

Allaah Anasema: "Ee Nabii! Waambie wake zako….”, Akaendelea: "Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine.”

Akaendelea kuwahutubia: «Kaeni majumbani mwenu» «Toeni Zakaah». «Mtiini Allaah».

Mpaka Aliposema: "Hakika Allaah Anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba (ya Mtume), na kukusafisheni baarabara."

Yote haya wanaambiwa wake zake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuanzia aya ya 28 hadi 33.

Hivi ndivyo ulivyo mfumo wote wa aya hizi zilizokamatana na haziwezi kutenganishwa isipokuwa kama mtu anataka kuvuka mipaka na kwenda kinyume na nassi.

 

Mtu anaweza kuuliza: ‘Kwa nini basi Allaah Ametumia ‘sigha’ (mfumo wa maneno) ya wingi wa wanaume na wanawake kwa pamoja Aliposema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ ‘Ankum’

Ikiwa Amewakusudia wake za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa nini asitumie sigha ya wanawake peke yao Akasema:

 

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُن  ‘Ankunnaُ

 

Kwa nini Asitumie sigha ya wanawake kama Alivyotumia katika aya nyingine zilizomo ndani ya mfumo huu?

 

Majibu ni kuwa; Aya za mwanzo Allaah Alipozungumza juu ya hukmu za kisheria na makatazo na maamrisho yanayowahusu wake za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alitumia ‘Nuun’ ya wanawakeعنكن  ‘Ankunna’ lakini Alipozungumza juu ya wema anaotaka kuuingiza ndani ya nyumba ile pamoja na kuwasafisha watu wa nyumba ile barabara, Alimuingiza pia na mwenye nyumba ambaye ni mwanamume naye ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ili kheri hiyo iwaenee wote. Na kawaida katika Lugha ya Kiarabu wanapotajwa wanawake na wanaume kwa pamoja hutumiwa wingi wa wanaume عنكم ‘Ankum’

 

Nani wanaostahiki zaidi kusafishwa na kutakaswa kuliko wake zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), watu wa nyumba yake, mama wa Waislamu, na wanaostahiki pia ni jamaa zake, watu wa aila yake. Kwa sababu Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anastahiki kuwa pamoja na kila kheri na kila jema na kila kilicho bora, na anastahiki zaidi kuwa pamoja na watu wema, naye haridhiki isipokuwa awe pamoja na watu wema, kwani wema lazima siku zote uwe katika mtiririko mmoja.

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alitaka kuwatakasa wake zake na jamaa zake, akamtunukia haya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

 

Ikiwa tumemkubali mke wa Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam) katika aya tuliyotangulia kuitaja kuwa ni Ahli yake na tukamkubali mke wa Al-‘Aziz kama ilivyokuja katika aya kuwa ni Ahli yake na tukamuingiza Sarah mke wa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) kuwa ni Ahli yake, juu ya kuwa katika aya ile Allaah Alitumia mfumo ule ule wa wingi wa wanaume na wanawake kwa pamoja Aliposema:

 

رحمة الله وبركاته عليكم أهل البيت

Alitumia neno (عليكمAlaykum)

 

Kama alivyotumia (عنكم Ankum) katika Suratul Ahzaab Aliposema:

 

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ

 

Ikiwa tumewakubali wake wa Mitume wote hao kuwa ni watu wa nyumba, tunalazimika pia kuwakubali wake wa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa ni watu wa nyumba yake.

 

 

Share