04-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Hadithi Ya Shuka Na Dalili Katika Hadithi
Hadithi Ya Shuka Na Dalili Katika Hadithi
Kutokana na haya inafahamika zaidi tafsiri ya ile hadithi maarufu inayoitwa Hadiyth al-Kisaa na maana yake ni hadithi ya nguo au hadithi ya shuka, wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipowaingiza ndani ya shuka ile ‘Aliy na Bibi Faatwimah na Al-Hasan na Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhum), kwa ajili ya kuwaingiza na wao katika zile baraka zilizoteremshwa ndani ya aya ile ya Suratul Ahzaab.
Hadithi inasimulia kuwa baada ya kuwaingiza wote hao ndani ya shuka, akasema:
"أللهمَّ هؤلاء أهل بيتي فاذهب عنهم الرجس وطهرهم تطهيراً
"Mola wangu hawa ni watu wa nyumba yangu, waondolee uchafu na uwasafishe baarabara."
Na Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) mke wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipoingiza kichwa chake ndani ya shuka hiyo akasema:
"Ewe Mtume wa Allaah na mimi ni katika watu wa nyumba yako.»
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamuambia:
تنحي فإنك على خير
"Wewe umo katika kheri wewe umo katika kheri."
Na maana yake ni kuwa Ummu Salamah na wake wenzake wote wamekwishatajwa na Allaah katika aya hiyo na kwamba wao wamo katika kheri hiyo ya kusafishwa na kutakaswa.
Ndiyo maana akaambiwa:
"Wewe umo katika kheri wewe umo katika kheri."
Dalili nyingine inayothibitisha kuwa wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni katika watu wa nyumba yake imo katika Al-Bukhaariy na Muslim na At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy na wengine kama ilivyopokelewa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipoulizwa na Masahaba:
"Vipi tukuswalie?
Akasema:
"Semeni:
اللهم صل على محمد وأزواجه وذريته، كما صليت على إبراهيم، وبارك على محمد وأزواجه وذريته، كما باركت على آل إبراهيم إنك حميد مجيد
"Mola wangu mswalie Muhammad na wake zake na vizazi vyake, kama ulivyomswalia Ibraahiym, na umbariki Muhammad na wake zake na vizazi vyake kama ulivyowabariki watu wa nyumba ya Ibraahiym hakika Wewe ni Mwenye kuhimidiwa uliye Mtukufu."
Ikajulisha kuwa mke wa mtu na vizazi vyake ni watu wa nyumba yake.
Ikiwa mtu hajatoshelezwa na dalili zote tulizozinukuu kutoka katika kitabu cha Allaah na mafundisho ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), basi ipo dalili nyingine katika Sahih Al-Bukhaariy itakayoondoa shaka yoyote iliyobaki kwa mwenye kuutafuta ukweli bila ya chuki moyoni mwake.
Inajulikana kuwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) mke wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisingiziwa uwongo katika kisa mashuhuri kinachojulikana kwa jina la Haadithatul Ifk, uwongo ambao Allaah aliteremsha aya katika Qur-aan tukufu kuukanusha, na wakati huo huo aya hizo ziliwaonya Waislamu kutorudia tena kueneza uvumi huo, na zikawatahadharisha juu ya adhabu kali itakayomfikia mwenye kurudia tena.
Wakati ule Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipanda juu ya mimbari yake kuhutubia, akasema:
"يا معشر المسلمين من يعذرني من رجل قد بلغني أذاه في أهلي، فواللّه ما علمت على أهلي إلا خيراً، ولقد ذكروا رجلاً ما علمت عليه إلا خيراً، وما كان يدخل على أهلي إلا معي"
“Enyi Waislamu! Nani atakayenipumzisha na mtu aliyeniudhi katika Ahli yangu, kwani WAllaahi sijaona kwa Ahli yangu isipokuwa kheri tupu, na hakuwa akiingia kwa Ahli yangu isipokuwa akiwa pamoja nami.” Al-Bukhaariy
Atakayechunguza, ataona kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amelitaja neno أهلي Ahliy (watu wa nyumba yangu) katika hotuba hii fupi mara tatu, zote zikimaanisha mkewe Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu anha), ikituthibitishia kuwa neno أهلي Ahliy lina maana ya mke.
Sisi tunawakubali na tunawapenda na tunawapa heshima kubwa na tunawatambua watu wote wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), wale wanaokubaliwa na Shia na pia wasiokubaliwa na Shia kuwa ni katika Ahlul Bayt kama vile ‘ami zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), watoto wa ami zake pamoja na watoto wao (Radhiya Allaahu anhum), hawa ambao Shia hawawatambui kuwa ni watu wa nyumba yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kama walivyotajwa katika hadithi iliyotangulia, nao ni kama ifuatavyo:
1. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
2. Wake zake
3. Binti zake wote
4. Watu wa nyumba ya Al-‘Abbaas bin Abdilmuttalib
5. Watu wa nyumba ya Aqiyl bin Abi Twaalib
6. Watu wa nyumba ya ‘Aliy bin Abi Twaalib
7. Watu wa nyumba ya Ja’afar bin Abi Twaalib
Hawa wote wametajwa katika hadithi iliyotolewa na Muslim wakati Zayd bin Al-Arqam (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoulizwa:
‘Wake zake si katika watu wa nyumba yake?’
Akasema:
‘Wake zake ni watu wa nyumba yake. Lakini watu wa nyumba yake (waliokusudiwa hapa) ni wale walioharimishwa kupokea sadaka.’
Akaulizwa:
‘Nani hao.
Akasema:
‘Hao ni watu wa nyumba ya ‘Aliy na watu wa nyumba ya ‘Aqiyl na watu wa nyumba ya Ja’afar na watu wa nyumba ya ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhum).’
Kwa hiyvo watu wa nyumba hizo juu ya kuwa wengine hawakuwemo ndani ya ile shuka lakini wametajwa kuwa ni watu wa nyumba yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Wake zake bila shaka wanaingia katika watu wa nyumba yake kwa sababu ya kutajwa katika Suratul Ahzaab kama ilivyotangulia, na ndiyo maana katika kuikamilisha aya hiyo Allaah Akasema:
{ وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَى فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّهِ وَالْحِكْمَةِ إِنَّ اللَّهَ كَانَ لَطِيفاً خَبِير}
‘Na watajieni (watu) yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Allaah na hikima (ya Mtume), kwa hakika Allaah ni Mjuzi wa mambo ya siri na Mjuzi wa mambo ya dhahiri.’ Al-Ahzaab-34
Na maana yake ni kuwa zifanyieni kazi zile aya zilizoteremshwa ndani ya nyumba zenu, kwa sababu Allaah amezihusisha nyumba zenu kwa kuteremsha aya Zake, tofauti na nyumba nyingine. Na Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu anha) ndiye anayehusika zaidi kwa sababu hazikupata kuteremshwa aya juu ya kitanda cha yeyote miongoni mwa wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) isipokuwa kwake.
Na watoto na wajukuu wa Al-Hasan bin ‘Aliy na Al-Husayn bin ‘Aliy na Abdullaah bin ‘Abbaas na Muhammad bin Al-Hanafiyah (mtoto wa ‘Aliy kwa mke mwengine), na Al-‘Abbaas bin ‘Aliy na wajukuu zao na wajukuu wa wajukuu zao, wote hao pia ni miongoni watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na hii ni kwa wale waliokuwa Waislamu.
Abu Lahab juu ya kuwa ni ami yake Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam), lakini yeye hayumo katika Ahli yake kwa sababu hakuwa Muislamu.
Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam) allipomuona mwanawe amekimbilia jabalini na maji yanaanza kumfikia alimuomba Allaah amuokowe.
Allaah Anasema :
وَنَادَى نُوحٌ رَّبَّهُ فَقَالَ رَبِّ إِنَّ ابُنِي مِنْ أَهْلِي وَإِنَّ وَعْدَكَ الْحَقُّ وَأَنتَ أَحْكَمُ الْحَاكِمِينَ {45} قَالَ يَا نُوحُ إِنَّهُ لَيْسَ مِنْ أَهْلِكَ إِنَّهُ عَمَلٌ غَيْرُ صَالِحٍ فَلاَ تَسْأَلْنِ
مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنِّي أَعِظُكَ أَن تَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِينَ {46
“Na Nuuh alimuomba Mola wake akasema: ‘Ewe Mola wangu! Mwanangu ni katika watu wa nyumbani kwangu. Na hakika ahadi yako ni haki. Nawe ni Mwenye haki kuliko mahakimu (wote).
Akasema (Allaah), “Ewe Nuuh! Huyu si miongoni mwa watu wako. Yeye ni (mwenye) mwendo usiokuwa mzuri. Basi usiniombe ambayo huyajui mimi nakunasihi usiwe miongoni mwa wajinga.” Huud-45-46
Allaah Alimkatalia na kumuambia kuwa huyo si mwanawe, wala si katika watu wa nyumba yake kwa sababu ya kuukanusha ujumbe aliokuja nao Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam).
Shia hawakubali kuwaingiza wengine isipokuwa wale tu waliotajwa katika hadithi ya shuka pamoja na Maimamu kumi na mbili waliofuata wa madhehebu ya Ithnaashariyah kwa sababu wanaamini kuwa hao ndio viongozi wa Waislamu waliotakaswa wasiotenda makosa watakaowaongoza Waislamu baada ya kufa kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mpaka Siku ya Qiyaamah.