Hilaal: Nilifunga Na Waliochelewa Kuanza Swawm Nikasafiri Nikafika Siku Ya ‘Iyd Niendelee Swawm?

SWALI:

 

ASALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH.

Mimi niko safarini Uingereza, nimeondoka Tanzania nikiwa nimefunga siku ya 28. Nimefuturu njiani na kula daku njiani na kunuia swaumu ya 29, nimeingia UK asubuhi watu wanazungumzia Idd kwamba wao wamefungua wamemaliza Ramadhani na sio kwamba waliuona mwezi bali ni ule wa kimataifa. Nikafikiria kwamba nifungue swaumu yangu wakati nilikotokea nimekuja nayo na siku hazijatimia ndiyo nimefunga ya 29, nikakosa jibu na nikaendelea na swaumu yangu mpaka saa za kufuturu jioni ndiyo nikafuturu.

 

Je, nimepata dhambi kufunga siku ya IDD ya wale wenyeji niliowakuta?

 

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kufunga Siku ya ‘Iyd.

Bila shaka katika suala la kufunga na kufungua yapo makundi mawili kila moja linafuata rai ambayo imetolewa na wanazuoni waliotangulia na wa sasa. Rai hizo ni:

 

1.     Kufuata mwezi wa kimataifa unapoonekana popote. Hii ni rai ya jamhuri (wengi) miongoni mwa wanazuoni mfano Abu Haniyfah, Maalik na Ahmad bin Hanbal.

 

2.     Kufuata mwezi wa kitaifa, nayo ni rai ya Imaam Ash-Shaafi’iy.

 

Hata hivyo, rai yenye nguvu ni ile ya kwanza ambayo inafaa ifuatwe na Waislamu kwa dalili zilizochukuliwa.

 

Kwa hali yako uliyoieleza ilikuwa wewe siku hiyo ufungue kwani ulikuwa mgeni na ilikuwa uache rai yako hiyo ili uwafuate wenyeji na baada ya Ramadhaan ulipe siku hiyo moja. Na lau mwezi ulikuwa umeonekana katika nchi hiyo au zile zilizo karibu basi ingekuwa ni madhambi kwako kufunga siku hiyo kabisa. Lakini kwa kuwa hukufungua tunatarajia kuwa Swawmu yako ni sahihi na tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akulipe wewe malipo mema na sisi pia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share