08-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Wake Zake
1- Wake Zake
Sisi tunaamini kuwa wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni katika watu wa nyumba yake, na kwamba wao ni mama zetu.
Allaah Anasema:
(( النَّبِيُّ أَوْلَى بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنْفُسِهِمْ وَأَزْوَاجُهُ أُمَّهَاتُهُمْ )) [الأحزاب:6]
«Nabii ana haki zaidi kwa Waislamu kuliko nafsi zao.na wakeze ni mama zao.» Al-Ahzaab -6
Na Akaharamisha kuwaoa baada ya kufariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Allaah Anasema:
(( وَمَا كَانَ لَكُمْ أَنْ تُؤْذُوا رَسُولَ اللَّهِ وَلا أَنْ تَنْكِحُوا أَزْوَاجَهُ مِنْ بَعْدِهِ أَبَدًا))
«Wala haikupasieni kumuudhi Mtume wa Allaah. Wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni dhambi kubwa mbele ya Allaah.» Al-Ahzaab-53
Tunawapa heshima kubwa mama zetu hawa, na wa mwanzo wao ni Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha). Wa mwanzo kuamini, aliyemsaidia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa hali na mali huku akimpa moyo na kumliwaza kila anapopatwa na masaibu au shida. Bibi Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) ndiye aliyeambiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
"إن اللّه أمرني أن أبشر خديجة ببيت في الجنة لا صخب فيه ولا نصب"
“Allaah Ameniamrisha nimpe bishara njema Khadiyjah juu ya nyumba yake Peponi ya Lulu, hamna zogo ndani yake wala tabu (yoyote).” Al-Bukhaariy na Muslim
Na kutoka kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
خير نسائها مريم بنت عمران، وخير نسائها خديجة بنت خويلد
«Mwanamke bora (katika zama zake) ni Maryam binti ‘Imraan, na mwanamke bora (katika zama zake) ni Khadiyjah binti Khuwaylid» Al-Bukhaariy na Muslim
Kisha anafuatia Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), binti wa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu), Bibi aliyetakaswa kutoka mbingu ya saba baada ya mnafiki yule aliyejitwika sehemu yake kubwa katika uzushi wake ambaye ni ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul kueneza uvumi mbaya juu ya mama huyu wa Waislamu kipenzi cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Maulamaa wote wamekubaliana kuwa kumsingizia uongo bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) katika kile kisa cha uongo alichozuliwa (hadithi ya "Al-Ifki") wakati Allaah kishamtakasa, basi anakuwa si Muislamu tena.
Allaah Anasema:
إِنَّ الَّذِينَ جَاؤُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ لَا تَحْسَبُوهُ شَرّاً لَّكُم بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ وَالَّذِي تَوَلَّى كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ {11} لَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْراً وَقَالُوا هَذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ {12} لَوْلَا
جَاؤُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاء فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاء فَأُوْلَئِكَ عِندَ اللَّهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ {13} وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ {14} إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّناً وَهُوَ عِندَ اللَّهِ عَظِيمٌ {15} وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَذَا سُبْحَانَكَ هَذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ {16} يَعِظُكُمُ اللَّهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَداً إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ {17} وَيُبَيِّنُ اللَّهُ لَكُمُ الْآيَاتِ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ {18} إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَاللَّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ {19} وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّه رَؤُوفٌ رَحِيمٌ {20}
"Hakika wale walioleta uongo huo (wa kumsingizia bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) mkewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) [kuwa amezini] Ni kundi miongoni mwenu (ni jamaa zenu) msifikiri ni shari kwenu bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aloyachuma katika madhambi yao na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kubwa (zaidi).
Kwa nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?
Kwa nini hawakuleta mashahidi wane? Na ilivyo kuwa hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Allaah ni waongo.
Na lau kuwa si fadhila ya Allaah juu yenu na rehema yake katika dunia na
Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyo jiingiza. Mlipoupokea (uongo huo mkawa mnautangaza) kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Allaah ni kubwa.
Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhaanaka (Mola wetu) Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!?
Allaah anakuonyeni msirudi kabisa (msirejee tena) kufanya kama haya, ikiwa nyinyi ni Waumini! (Waislamu) kweli.”
An-Nuur – 11-17
Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika aya hizi Ametumia neno; ‘Subhaanaka’ katika kumtakasa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kutokana na uongo aliozuliwa, na neno hili ‘Subhaanaka’ Allaah Analitumia katika kukanusha uongo mkubwa tu, Anaponasibishwa na mwana au mshirika.
Allaah Amesema:
سُبْحَانَكَ هَذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ
“(Mola wetu) Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!?”
Wamasema baadhi ya Wafasiri:
“Alipokanusha kuwa hana mwana wala mshirka alisema:
وَقَالُواْ اتَّخَذَ اللّهُ وَلَداً سُبْحَانَهُ بَل لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ
“Na wanasema:”Allaah amejifanyia mtoto” ‘Subhaanahu’ Ameepukana na hilo bali ni vyake hivyo vilivyomo mbinguni na ardhini . Vyote vinamtii Yeye.” Al-Baqarah-116
Na Akasema:
مَا كَانَ لِلَّهِ أَن يَتَّخِذَ مِن وَلَدٍ سُبْحَانَهُ
“Haiwi kwa Allaah kufanya mtoto; ‘Subhaanahu’ Ametakasika.” Maryam-35
Amelitumia neno ‘SubhaAnahu’ kwa ajili ya kujitakasa na kukanusha kuwa Anaye mwana, na Amelitumia neno hilo hilo ‘SubhaAnahu’ katika kuukanusha uongo aliozuliwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha).
Miongoni mwa wake wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pia ni Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha), mama yetu mtulivu wa tabia, mwenye akili yenye uwezo wa kupima mambo, mwingi wa hekima ambaye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mara nyingi alikuwa akichukuwa ushauri wake katika baadhi ya mambo. Alimshauri siku ile ya Sulhu ya Hudaybiyah na akapata ushauri mwema kutoka kwake.
Hawa na wake zake wengine wote ni mama zetu. Ni watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kama ilivyokuja katika aya za Surat al Ahzaab, na kama tulivyoona katika dalili mbali mbali kutoka katika Qur-aan tukufu na katika Mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Inatuwajibikia kuwapenda na kuwaenzi na kuwaheshimu mama zetu hawa.
Baada ya kumalizika vita vya Ngamia (Waqi'at al Jamal), ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliamua kumuacha huru Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Wafuasi wake wakamuuliza:
«Inakuwaje halali kumwaga damu zao na haiwi halali kwetu mali zao na mateka wao?»
‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema:
«Yupi kati yenu atakayefurahi Mama wa Waislamu awe mateka wake?»
Wote wakanyamaza.
Ikiwa ni haramu kumsema vibaya Muislamu yeyote, basi inakuwa vibaya zaidi kuwasema vibaya watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wakiwemo wake zake na watu wa ukoo wake pamoja na wajukuu wake na wajukuu wa wajukuu wakiwemo Al-Hasan na Al-Husayn na ‘Abdullaah bin Al-Hasan na ‘Aliy bin Al-Hasan na Muhammad bin ‘Aliy na Ja’afar bin Muhammad na Muusa bin Ja’afar na ‘Aliy bin Muusa Ar-Ridhwaa na waliobaki, na pia Sahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) wote kwa pamoja wa Makkah na wa Madiynah, na wale ambao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amewabashiria Pepo, na pia viongozi wetu wa dini.
Haiwezekani ukapatikana umoja wa Waislamu ikiwa kundi lolote litakuwa shughuli yao kubwa ni kuweka vikao vya kila mwaka kuwalaani na kuwatukana Watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wakiwemo wake zake, au Sahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum), kwa sababu hawa ni viongozi wetu waliokuwa naye tokea siku ile ya mwanzo. Hawa ni mifano mema kwetu, walioisimamia dini hii na kuieneza ulimwenguni kote, na hawa ndio waliotufikishia dini hii baada ya kujitolea mhanga roho zao na mali zao.
Wakati huo huo sisi tunaamini kuwa watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wanatoka katika nyumba bora kupita zote, lakini pia tunaamini kuwa hapana ajuaye Ghaybu isipokuwa Allaah peke Yake.
Allaah Anasema:
(( قُلْ لا يَعْلَمُ مَنْ فِي السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّهُ ))[النمل:65].
“Sema: ‘Hakuna aliyoko katika mbingu na ardhi ajuaye Ghayb ila Allaah.” An-Naml-65
Na Anasema:
(( وَعِنْدَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ))[الأنعام:59]
“Na ziko Kwake (Allaah tu) funguo za siri (Ghayb) hakuna azijuaye ila Yeye tu.” Al-An’aam-59