09-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Nani Swahaba Na Nani Mnafiki
Nani Swahaba – Kilugha Na Kidini
Katika kamusi la lugha ya Kiarabu, neno ‘Swahaba’, maana yake ni Rafiki, Mwenzi wake, Sahibu n.k.
Katika dini, neno ‘Swahaba’ maana yake ni Muislamu aliyemuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), akamfuata na kumuamini na akafariki katika imani hiyo.
Na hii ina maana kuwa, yeyote aliyewahi kumouna Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na asimuamini, basi hawezi kuingia katika maana ya neno ‘Swahaba’.
Nani Mnafiki – Kilugha Na Kidini
Katika kamusi la lugha ya kiarabu, neno ‘Mnafiki’ maana yake ni mtu mwenye kigeugeu au mwenye kuwa na sura mbali mbali: Leo hivi kesho vile.
Katika dini, neno ‘Mnafiki’ maana yake ni yule anayejidhihirisha kuwa ni Muislam na kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), wakati undani wake ni kafiri na adui wa Allaah na adui wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Baada ya tafsiri hii fupi ya nani Swahaba na nani Mnafiki, tutakubaliana kuwa maneno hayo mawili hayawezi kuwa na maana moja, (hayawezi kwenda sambamba) Kilugha wala Kidini.
Kwa sababu Swahaba ni yule aliyemuamini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akafariki dunia akiwa Muislam, wakati Mnafiki ni mwenye kujidhihirisha kama ni Muislam wakati ndani ya nafsi yake ni kafiri.
Kwa hivyo haiwezekani Swahaba akawa Mnafiki na wala Mnafiki hawezi akawa Swahaba.
Sasa Mtu anaweza kuuliza:
'Vipi tutaweza kutofautisha baina ya Swahaba na Mnafiki?'
Majibu:
Mnafiki ana sifa na alama maalum tulizojulishwa katika Qur-aan na katika Mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na kwa ajili hiyo tunaweza kutofautisha baina yake na Swahaba.
Wanafiki ni watu;
‘Wanaoeneza ufisadi ardhini, kuifanyia istihzai dini, kuwafanyia istihzai wacha Mungu, ni wavukaji mipaka katika kufanya maasi wenye kuununua upotofu (upotevu) kwa uongofu, wavivu katika kufanya ibada, hugeuka geuka, mara Waislamu mara makafiri, kama Alivyosema Allaah:
مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَلِكَ لاَ إِلَى هَـؤُلاء وَلاَ إِلَى هَـؤُلاء
“Wanayumba yumba baina ya huku (kwa Waislam) na huko (kwa makafiri). Huku hawako wala huko hawako),” An-Nisaa-143
Na katika sifa za wanafiki pia ni;
‘Kuwa hawamwamini Allaah wala Siku ya Akhera na kwamba Waislam wanapopata kheri yoyote au mafanikio, wao wanahuzunika, na hufurahi pale Waislamu wanapopata tabu au wanapokumbwa na masaibu au mitihani.
Huchukizwa na kutoa mali zao katika njia ya Allaah na hufurahi wanaporudi nyuma na kumuacha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) peke yake vitani.
Wameingia katika dini kwa ajili ya kujikinga wasiambiwe kuwa wao ni makafiri, na wanapenda kuwadhuru Waislam na kuwafarikisha. Na katika sifa za unafiki ni kuwa; wanaiahirisha Swalah mpaka nyakati zake za mwisho na hawahudhurii Swalah za jamaa na kwamba wanaionea uzito kabisa Swalah ya Alfajiri na ya ‘Ishaa’.
Hizi ni baadhi tu ya sifa za Wanafiki Alizozitaja Allaah katika Qur-aan tukufu, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika mafundisho yake.
Bila shaka Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni watu walio mbali kabisa na sifa hizi. Hawa ambao Allaah Amewaambia:
كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللّهِ
“Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni) mnaamrisha yaliyo mema na mnakataza yaliyo maovu, na mnamwamini Allaah.” Aali ‘Imraan- 110
Na Akasema juu yao:
يا أيها النبي حسبك الله ومن اتبعك من المؤمنين
“Ewe Mtume wa Allaah! Allaah anakutoshelezea wewe na wale walokufuata katika hao walioamini”. Al-Anfaal-64
Na Akasema juu yao:
مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّهِ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاء عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاء بَيْنَهُمْ تَرَاهُمْ رُكَّعاً سُجَّداً يَبْتَغُونَ فَضْلاً مِّنَ اللَّهِ وَرِضْوَاناً
“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na walio pamoja naye ni wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja), wakitafuta fadhila za Allaah na radhi (yake).” Al Fat-h- 29
Na Akasema:
وَالَّذِينَ آمَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ آوَواْ وَّنَصَرُواْ أُولَـئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقّاً لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ
“Na wale walioamini wakahama (kuja Madiynah) na wakaipigania dini ya Allaah (Nao ni Muhajir); na wale waliowapa (Muhajir) mahala pa kukaa na wakainusuru dini (ya Allaah na Mtume wake).(nao ni Answaar) Hao ndio Waislam wa kweli. Watapata msamaha (wa Allaah) na kuruzukiwa kuzuri (kabisa huko Akhera).” Al-Anfaal – 74.
Maswahaba wa Makkah (Radhiya Allaahu ‘anhum) ndio walioamini, wakahama, na wakapigana jihadi. Na Maswahaba wa Madiynah (Radhiya Allaahu ‘anhum) ndio waliowapa mahala pa kukaa na wakainusuru dini.
Baada ya maelezo haya kutoka kwa Muumba wa mbingu na ardhi, asije mtu akatuambia kuwa Maswahaba na wanafiki ni kitu kimoja. Hakika haya ni matusi makubwa kabisa!
Hawawezi kuwa wanafiki watu ambao Allaah Amesema juu yao:
“Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni).”
Hawawezi kuwa wanafiki watu ambao Allaah Ameshuhudia kuwa ni:
“Wenye nyoyo thabiti mbele ya makafiri na wenye kuhurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama kwa kurukuu na kusujudu (pamoja), wakitafuta fadhila za Allaah na radhi (yake).”
Hawawezi kuwa wanafiki watu ambao Allaah Mwenyewe Anashuhudia kuwa “Hao ndio Waislam wa kweli.”
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:
"لا تَسُبّوا أَصْحَابِي، فَوَالّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَوْ أَنّ أَحَدَكُمْ أَنْفَقَ مِثْلَ أُحِدٍ ذَهَباً مَا أَدْرَكَ مُدّ أَحَدِهِمْ وَلاَ نَصِيفَهُ".
"Msiwatukane Swahaba wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, hata mmoja wenu atajitolea katika njia ya Allaah kugawa dhahabu ukubwa wake mfano wa jabali Uhud, basi hatofikia gao lao wala hata nusu ya gao lao." Al-Bukhaariy na Muslim
Na akasema:
من سب أصحابي فعليه لعنة الله والملائكة والناس أجمعين
“Atakayewatukana Maswahaba wangu, basi itampata laana ya Allaah na (laana ya) Malaika na (laana ya) watu wote”.
((At-Twabariy, katika ‘Al-Kabiyr’, Abu Na’iym katika ‘Al Hiliyah’ na Abu ‘Aaswim, na hadithi hii pia inapatikana katika ‘Silsila za hadithi sahihi kilichoandikwa na Sheikh Al-Albaaniy)).
Na akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
“Nihifadhieni Maswahaba wangu, kisha wale waliowafuatilia kisha wale waliofuatilia”. Imam Ahmad, Ibn Maajah, na Al-Haakim.
Ikiwa Maswahaba waliokuwa wengi wanatuhumiwa kuwa ni watu wenye kigeugeu na unafiki, hii italeta maana kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakuweza kuwalea na kuwafundishsa vizuri Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) wakaijuwa haki, na kwamba yeye ni mlezi asiyefanikiwa, aliyeshindwa kuifanya kazi yake ya kuwalea Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum).
Haikubaliki akilini abadan kuwa baada ya kuishi nao muda mrefu wote huo alifanikiwa kuwalea na kuwafundisha Maswahaba watatu tu au wasiozidi saba?
Kila anayesoma na kuidurusu Siyrah (historia) ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), anaelewa kwamba wakati Waislam walipokuwa Makkah hapakuwa na unafiki, na hii ni kwa ajili ya adhabu kali walizokuwa wakipata waliosilimu wakati ule. Na inajulikana pia kwamba unafiki ulianza kujitokeza baada ya Waislam kuhamia Madiynah, na baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kupata nguvu, na dini ya Allaah kuanza kutambulika kila mahala.
Na inaeleweka pia kwa kila mwenye kuidurusu Siyrah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan na wengineo ni miongoni mwa Maswahaba walioingia katika dini ya Allaah tokea siku za mwanzo, wakapata tabu na shida kama walivyopata wenzao, na hii ni dalili wazi kuwa walikuwa mbali na sifa ya unafiki.
Allaah Amewafedhehesha wanafiki kwa kuwateremshia Suratul Munafiquun na At-Tawbah; Akaelezea ndani ya sura hizo juu ya hali zao na vitimbi vyao; na Akatuelezea yale yaliyofichika nyoyoni mwao katika kuwachukia Waislam, na ndiyo maana Suratut Tawbah ikaitwa 'Sura ya Kufedhehesha'. Katika sura hiyo Allaah Alitaja pia sifa za Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) na Akatujulisha kuridhika kwake nao. Na huu ni ushahidi utokao Kwake (Subhaanahu wa Ta’ala).
Ama Suratul Munafiquun, hii imeteremshwa kwa ajili ya kutujulisha juu ya mkubwa wa wanafiki na kiongozi wao aitwae Abdullah bin Ubay bin Saluul na wenzake.
Anasema Zayd bin Al-Arqam (Radhiya Allaahu ‘anhu):
"Nilikuwa vitani, nikamsikia Abdullah bin Ubay akisema:
“Msitoe mali kuwasaidia waliokuwa na Mtume wa Allaah mpaka watakapomwondokea pale alipo, na tutakaporudi Madiynah yule mtukufu (akimaanisha yeye Abdullah bin Ubay ‘mkuu wa wanafiki’ kuwa ni mtukufu) atamtoa (katika mji wa Madiynah) yule aliyedhalilika (akimaanisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam kuwa eti ndiye aliyedhalilika)”.
Nikamhadithia ‘ami yangu hayo niliyoyasikia (au ‘Umar) naye akamhadithia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): Akaniita na mimi nikamhadithia. Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamtuma mtu amuite Abdullah bin Ubay pamoja na wenzake, wakaapa na kukanusha yale waliyosema, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakunisadiki na akamsadiki yeye. Nikaona dhiki sijapata kuona mfano wake. Nikakaa nyumbani kwangu, lakini haujapita muda Allaah akateremsha Suratul Munafiquun, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamtuma mtu aniite, akanisomea (Sura hiyo) kisha akaniambia:
“Allaah Amesadikisha maneno yako ewe Zayd”. Al-Bukhaariy.
Tafsiri hii pia inapatikana katika kitabu cha tafsiri cha Mashia kiitwacho ‘Maj ma’ul bayaan fiy tafsiyril Qur-aan’, kilichoandikwa na At-Tubrusy ambaye ni miongoni mwa Maulamaa wakubwa wa Kishia. Na katika kitabu hicho, ameelezea sababu ya kuteremshwa Suratul Munafiqun kuwa ni juu ya Abdullah bin Ubay ‘mnafiki’ na wenzake …
(‘Maj ma’ul bayaan fiy tafsiyril Qur-aan’ ukurasa 85)
Kisha Mwanachuoni huyu wa Kishia akazitaja riwaya zile zile alizozielezea Imam Al-Bukhaariy zinazothibitisha hoja hiyo.
Inajulikana wazi kuwa Abdullah bin Ubay pamoja na wafuasi wake walikuwa wakijulikana na Maswahaba wote (Radhiya Allaahu ‘anhum) kuwa ni wanafiki, na mtu yeyote anaposoma Surat at Tawba ataona kuwa sura hiyo imeelezea juu ya vituko mbali mbali walivyokuwa wakivifanya wanafiki hao kiasi ambapo ilikuwa ikijulikana wazi mbele ya kila mtu kuwa wao ndio waliokusudiwa.
Kwa mfano kuanzia aya ya 44 hadi 49 ya sura hiyo Allaah Anasema:
لاَ يَسْتَأْذِنُكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَن يُجَاهِدُواْ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ وَاللّهُ عَلِيمٌ بِالْمُتَّقِينَ {44} إِنَّمَا يَسْتَأْذِنُكَ الَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُونَ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ وَارْتَابَتْ قُلُوبُهُمْ فَهُمْ فِي رَيْبِهِمْ يَتَرَدَّدُونَ {45} وَلَوْ أَرَادُواْ الْخُرُوجَ لأَعَدُّواْ لَهُ عُدَّةً وَلَـكِن كَرِهَ اللّهُ انبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ وَقِيلَ اقْعُدُواْ مَعَ الْقَاعِدِينَ {46} لَوْ خَرَجُواْ فِيكُم مَّا زَادُوكُمْ إِلاَّ خَبَالاً ولأَوْضَعُواْ خِلاَلَكُمْ يَبْغُونَكُمُ الْفِتْنَةَ وَفِيكُمْ سَمَّاعُونَ لَهُمْ وَاللّهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ {47} لَقَدِ ابْتَغَوُاْ الْفِتْنَةَ مِن قَبْلُ وَقَلَّبُواْ لَكَ الأُمُورَ حَتَّى جَاء الْحَقُّ وَظَهَرَ أَمْرُ اللّهِ وَهُمْ كَارِهُونَ {48} وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ ائْذَن لِّي وَلاَ تَفْتِنِّي أَلاَ فِي الْفِتْنَةِ سَقَطُواْ وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ {49}
“Hawatakuomba ruhusa wale wanao muamini Allaah na Siku ya Mwisho, wasende kupigana Jihadi kwa mali yao na nafsi zao. Na Allaah ni Mwenye kuwajua wachaji Allaah.
Wasiomuamini Allaah na Siku ya Mwisho na nyoyo zao zikatia shaka, hao tu ndio wanao kutaka ruhusa. Basi hao wanataradadi katika shaka zao.
Na ingelikuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangelijiandalia maandalio, lakini Allaah kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo Akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanaokaa!
Lau wangelitoka nanyi wasingelikuzidishieni ila mchafuko, na wangetangatanga kati yenu kukutilieni fitna. Na miongoni mwenu wapo wanaowasikiliza. Na Allaah Anawajua madhaalimu.
Tangu zamani walitaka kukutilieni fitna, na wakakupindulia mambo juu chini, mpaka ikaja Haki na ikadhihirika amri ya Allaah, na wao wamechukia”.
Na miongoni mwao wapo wanaosema: ‘Niruhusu wala usinitie katika fitina’. Kwa yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina. Na hakika Jahannamu imewazunguka.” At-Tawbah – 44-49
Inaeleweka na kila mtu kuwa Maswahaba wote walitoka kwenda vitani siku hiyo ya vita vya Tabuuk (vita ambavyo aya hizo zinazungumzia juu yake), na waliobaki nyuma ni Abu Dharr na Abu Khaythamah (Radhiya Allaahu ‘anhum), kisha nao pia wakenda kujiunga na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na wenzao, na walikutana nao njiani kabla ya kuwasili uwanja wa vita.
Na ineleweka pia kuwa miongoni mwa waliobaki nyuma ni Ka’ab bin Maalik, Hilaal bin Umayyah na Miraarah bin Rabi’ah (Radhiya Allaahu ‘anhum), nao ni katika watu wa Madiynah na inajulikana na kila mtu kuwa Allaah Aliwasamehe Maswahaba hao kama ilivyoelezwa katika kisa cha ‘Wale watatu waliongojeshwa’.
Ama wengine waliobaki Madiynah wasiende vitani walikuwa wakijulikana kuwa ni katika wale wanafiki waliomuendea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuomba udhuru wa uongo, au wale waliokuwa na udhuru wa kutopigana Jihaad kwa ajili ya ugonjwa au udhuru mwingine unaokubalika.
Na haya tulieleza hapo mwanzo katika kisa cha Ka’ab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa katika waliobaki pale Madiynah wasende vitani hakuwa akimuona aliye kufu yake isipokuwa wenye udhuru au wale waliokuwa wakijulikana kuwa ni Wanafiki.
Na hii ni dalili kuwa wanafiki walikuwa wakijulikana na Maswahaba.
Na katika sura hiyo hiyo ya At-Tawbah, Allaah Anatujulisha kuridhika kwake na Maswahaba waliotangulia kuingia katika Uislamu miongoni mwa Wahajir (watu wa Makkah waliohamia Madiynah) na Answaar (Watu wa Madiynah waliowapokea Wahajir wa Makkah) na akawatayarishia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele.
Allaah Anasema:
وَالسَّابِقُونَ الأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللّهُ عَنْهُمْ وَرَضُواْ عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَداً ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ
“Na wale waliotangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Answaar, na walio wafuata kwa wema, Allaah Ameridhika nao, na wao wameridhika Naye; na Amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.” At-Tawbah - 100
Sasa tizameni ndugu zangu, vipi Allaah Anatuelezea juu ya kuridhika kwake na Maswahaba katika Muhaajir na Answaar kinyume na wanavyotuhumiwa unafiki, na kwamba walirudi nyuma na kukufuru, akiwemo mbora wa Maswahaba wote Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Sisi tunaridhika na wote alioridhika nao Allaah, na tunawafanyia uadui maadui wote wa Allaah, na tunafuata yale tuliyofundishwa na Allaah pamoja na mafundisho ya Mtume wa Allaah wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Allaah Anasema:
لَقَد تَّابَ الله عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ إِنَّهُ بِهِمْ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ {117}
“Allaah Amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Answaar waliomfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.” At-Tawbah - 117
Allaah ni Mpole kwao na Anawarehemu na Ameridhika nao na Anawasifia namna walivyosimama pamoja na Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika saa ile ya dhiki (vita vya Tabuuk), na huu ni ushahidi utokao kwa Allaah Asiye mshirika.
Utayakuta haya pia katika vitabu vya wanavyuoni wakubwa wa Kishia (Ithnaasheri) waliotamka ukweli ndani ya baadhi ya vitabu vyao vinavyotambulika.
Tafsiri ya Al-Iyaashi
Anasema Abu Naswr Muhammad bin Mas’uud, anayejulikana kwa jina la ‘Al-Iyaashi’ katika tafsiri yake juu ya kauli ya Allaah isemayo:
إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِين
“Hakika Allaah huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojitakasa.’ Al-Baqarah – 222
Alisema:
"Kutoka kwa Salaam anasema: ‘Nilikuwa kwa Abu Ja’afar (Muhammad Al-Baaqir Imam wa tano kwa Shia) akaingia Hamran bin Ayun na kumuuliza baadhi ya mambo, na alipotaka kuondoka, Ayun akamuuliza Abu Ja’afar:
'Tuelezee Allaah Akupe umri mrefu, sisi tunapokuwa nawe nyoyo zetu hulainika na nafsi zetu zinakuwa mbali na dunia, tunadharau kila kilichomo mikononi mwa watu katika mali, lakini tunapotoka na kuchanganyika na watu na kufanya biashara, tunaanza kuipenda tena dunia.’
Abu Ja’afar akasema:
"Nyoyo zinashindwa na mambo baadhi ya wakati, na wakati mwengine mambo yanakuwa mepesi.’ Kisha Abu Ja’afar akaendelea kusema: ‘Kwa hakika Maswahaba wa Mtume wa Allaah walisema:
‘Ewe Mtume wa Allaah, tunajiogopea unafiki’ akasema: “Kwa nini mnaogopa?”
Wakasema:
“Sisi tunapokuwa nawe ukatukumbusha, huwa na uoga, na nyoyo zetu zinalainika tukaisahau dunia, hatuitamani, hata hufikia kuwa tunaiona Akhera Pepo na Moto mbele yetu. Lakini mara tunapotoka kwako na kuingia majumbani mwetu na kuanza kuwabusu watoto wetu na kuonana na wake zetu na mali zetu, tunaanza kubadilika hali zetu kinyume na pale tunapokuwa nawe, kama kwamba hatukuwa na kitu. Je! Hutuogopei unafiki?"
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia:
“Kabisa sikuogopeeni hilo, kwani hizi ni katika hatua za Shaytwaan akijaribu kukupendezesheni dunia, Wallahi lau kama mungebaki katika hali ile mliyokuwa nayo pale mlipokuwa nami, basi Malaika wangekusalimieni majiani na mungekuwa mnatembea juu ya maji, na kama mungelikuwa hamtendi madhambi na kumuomba Maghfira Allaah, basi Allaah Angeliumba viumbe vingine ili wafanye madhambi kisha wamuombe maghfira ili apate kuwaghufiria, kwani Muislam siku zote yupo katika mtihani, hukuisikia kauli ya Allaah isemayo:
إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ
‘Hakika Allaah huwapenda wanaotubu?’
na isemayo:
وَأَنِ اسْتَغْفِرُواْ رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُواْ إِلَيْهِ
“Na ili muombe msamaha kwa Mola wenu kisha mtubie (mrejee)?"
Huud – 3 (Tafsir Al-Iyaashi Juz. 1 uk. 128)
Katika riwaya hii, anatubainishia Al-Iyaashi katika tafsiri yake kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameshuhudia kuwa hawaogopei Swahaba zake unafiki. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hasemi kwa matamanio ya nafsi yake.
Kwa hivyo mwenye kumuita Swahaba yeyote kuwa ni mnafiki, mtu huyo atakuwa ana moja katika mawili:
1- Ama anakwenda kinyume na mafundisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
2- Au anajua zaidi kupita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Ikiwa tunautaka umoja wa Waislamu kikweli na kuiondoa chuki iliyopo, basi nawaomba ndugu zetu Mashia waache kuwakufurisha Maswahaba au kuwaita wanafiki na kuwaapiza, na badala yake tumfanye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa ni ruwaza njema kwetu, kuwa ni mfano mwema kwetu wa kuigwa, na tuwapende kama alivyokuwa akiwapenda (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwapenda Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum). Na watu wa nyumba yake 'Ahlul Bayt' (Radhiya Allaahu ‘anhum) nao pia walikuwa wakiwapenda Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum), na Maswahaba nao walikuwa wakiwapenda Ahlul Bayt.
Huyu hapa Imam Al-Hasan Al-‘Askari, ambaye ni Imam wa kumi na moja wa Shia alipokuwa akiwafahamisha watu daraja ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) mbele ya Allaah alisema:
‘Miongoni wa masuala aliyouliza Muusa ('Alayhis Salaam) kumuuliza Allaah alisema:
‘Wapo Maswahaba wa Mtume yeyote wa Allaah walio bora kuliko Maswahaba wangu?'
Allaah Akamjibu:
“Ewe Muusa kwani hujui kuwa ubora wa Maswahaba wa Mtume wa Allaah Muhammad juu ya Maswahaba wa Mitume yote ni sawa na ubora wa watu wa nyumba ya Muhammad juu ya watu wa nyumba za Mitume yote, na mfano wa ubora wa Muhammad juu ya Mitume yote?”
Tafsiri ya Al-Hasan Al-‘Askariy uk. 11(Tafsiri ya Surat Al-Baqarah)
Ndani ya kitabu kitukufu kwa Shia kiitwacho ‘Nahjul Balaaghah’, Sharhi ya Muhammad ‘Abdu Uk. 225, imeandikwa kuwa Imam ‘Aliy alisema:
“Nimewaona Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Laahu ‘alayhi wa sallam), na sioni yeyote kati yenu aliyeshabihiana nao. Walikuwa wakati wa asubuhi utawaona nywele zimetimka kwa sababu ya kusimama kwao usiku kucha wakisujudu na kusimama (kwa kuswali), wanaomba huku wakisujudu, na wanapolala, na wanapokumbuka Akhera yao utawaona wanasimama kama kwamba wamesimamia makaa ya moto. Na Anapotajwa Allaah basi macho yao yanatoa machozi mpaka nyuso zao zinaroa, na wanainamisha vichwa vyao chini mfano wa miti iliyopinda kwa upepo mkali wa kimbunga kwa kuhofia adhabu na kutarajia thawabu”.
Ama Ibraahiym At-Thaqafiy ambaye ni katika Maulamaa wakubwa wa Shia, katika kitabu chake kiitwacho ‘Al-Ghaaraat’ Juzuu ya 1 Uk. 177 akimnukuu ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu):
“Aliulizwa ‘Aliy: ‘Ewe Amiri wa Waislam, tuelezee juu ya Swahibu zako.’
Akauliza:
“Juu ya Swahibu zangu wepi?”
Wakamwambia:
“Juu ya Swahaba wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).”
Akasema:
“Maswahaba wa Muhammad wote ni Swahibu zangu”.
Tunamuomba msomaji arudie marejeo yote tuliyonukuu kutoka katika Qur-aan tukufu na kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kutoka kwa Maulamaa wa pande zote mbili ili imbainikie heshima ya Maswahaba hawa wakiwemo Makhalifa watatu wa mwanzo wa Waislam mbele ya Allaah na mbele ya Mtume wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na mbele ya Maulamaa waliotangulia wa pande zote mble, kisha ajiulize; ni kwa maslahi ya nani mtu anaweza kuthubutu kuwatukana au kuwazulia uongo na kuwawekea vikao vya kila mwaka kuwalaani na kuapa juu ya kulipa visasi.
Bali hata Sayiduna Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa katika nchi ya Constantinople akipigana jihadi, na wakati huo Mu’awiyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyekuwa Khalifa wa Waislamu. Kwa hivyo Maswahaba na Watu wa Nyumba ya Mtume (Radhiya Allaahu ‘anhum) walikuwa wakishirikiana na kupendana na kunasibiana na walikuwa pamoja katika jihadi yao dhidi ya maadui wa Uislamu.
Siku moja kundi la watu lilikwenda kwa Imam ‘Aliy Zaynul-’Aabidiyn (Radhiya Allaahu ‘anhu) na walikuwa wakiwasema vibaya Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Laahu alayhi wa sallam); Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhum).
‘Aliy Zaynul-’Aabidiyn (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawauliza:
“Kwanza nielezeni ni nani nyinyi? Nyinyi ni katika wale Wahajir (Watu wa Makkah) waliohama mwanzo waliotolewa majumbani mwao na katika mali zao wakitaka fadhila za Allaah na radhi zake na wakamnusuru Allaah na Mtume wake?”
الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلاً مِّنَ اللَّهِ وَرِضْوَاناً وَيَنصُرُونَ اللَّهَ وَرَسُولَهُ
Al-Hashr -8
Wote kwa pamoja wakasema: “La, sisi si katika hao”
Akawauliza tena:
“Basi nyinyi ni katika watu waliofanya maskani yao hapa (Madiynah) na wakautakasa Uislamu (wao barabara) kabla ya (kuja ) hao (Muhaajiriyn) na wakawapenda hao waliohamia kwao”
.
وَالَّذِينَ تَبَوَّؤُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ
Al-Hashr -9
Wakajibu:
“La! Sisi si katika hao”
Kisha Imam ‘Aliy Zaynul-’Aabidiyn (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawaambia:
“Nyinyi wenyewe mumeshuhudia kuwa si katika hawa wala si katika wale. Basi na mimi ninashuhudia pia kuwa nyinyi si katika kundi lile la tatu ambalo Allaah Amesema juu yao:
وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلّاً لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ
“Na Waliokuja baada yao (wakawa wanapendana na Waislamu waliotangulia wanawaombea du’aa) wanasema; ‘”Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu waliotutangulia (kufa) katika Uislamu. Wala usijaaliye katika nyoyo zetu undani kuwafanyia Waislamu (wenzetu). Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole sana, Mwenye Rehema mno.” Al-Hashr – 10
Katika aya hizi Allaah Anashuhudia kuwa watu wa Makkah waliacha majumba yao na mali zao na watu wao kwa ajili ya kutaka fadhila za Allaah na radhi Zake, na kwa ajili ya kumnusuru Allaah na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na akashuhudia kuwa ni wakweli.
Na Allaah Anashuhudia pia watu wa Madiynah waliutakasa Uislamu baraabara, juu ya kuwa walifikiwa na wageni wazito na hawakuwa na mali ya kutosha, waliwapokea wageni hao kwa moyo mkunjufu, wakahiari kujinyima wao kwa ajili ya kuwakirimu wageni.
Kisha Allaah Akatuamrisha tuliokuja baada yao kuwaombea maghfira na Akatutaka tusijaaliye ndani ya nyoyo zet undani wowote juu yao.
Imepokelewa kutoka kwa Yahya bin Kathiyr kutoka kwa Ja’afar bin Muhammad bin ‘Aliy bin Al-Husayn kutoka kwa baba yake ((Radhiya Allaahu ‘anhum) kuwa amesema:
« Alikuja mtu kwa baba yangu akamuambia : ‘Nihadithie juu ya Abu Bakr.’ Akasema: ‘Unauliza juu ya Asw-Swiddiyq.’ Akasema yule mtu : ‘Allaah akurehemu, na wewe pia unamuita Asw-Swiddiyq ?’ Akamuambia : ‘Akukose mama yako wewe. Ameitwa Asw-Swiddiyq na aliye bora kupita mimi na wewe, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Watu wa Makkah na watu wa Madiynah. Asiyemuita kwa jina la Asw-Swiddiyq basi Allaah hatosadiki kauli yake duniani wala akhera. Nenda, tena umpende Abu Bakr na ‘Umar.»
Imeandikwa katika Nahjul Balaaghah pia kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuandikia Mu’aawiyah bin Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) akimuambia:
Kwa Mu’aawiyah:
"BismiLlaahir Rahmaanir Rahiym,
Amma ba’ad, kwa vile watu wote wamefungamana nami katika mji wa Madiynah, basi nawe pia uliyeko huko Shaam (Syria) unalazimika kufungamana nami. Na hii ni kwa sababu watu waliofungamana nami ni wale wale waliofungamana na Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan. Kwa hivyo aliyehudhuria hana haki ya kulikataa na asiyehudhuria hana haki ya kulipinga. Kwa hakika ushauri ni wa Muhaajiriyn na Answaar (Watu wa Makkah na wa Madiynah). Wanapokubaliana wote juu ya mtu na kumchagua kuwa Imam wao, na Allaah Anaridhika na uchaguzi wao.
Nimemtuma kwako Jariyr, naye ni katika watu wa Imani na watu waliohajir, kwa hivyo fungamana nami - Walaa quwwata illa biLlaah!!".
(Nahjul-Balaaghah- uk. 427 mlango wa 6)
SubhaanAllaah! Huyu hapa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) anakiri mwenyewe kuwa hapana mwenye haki ya kupinga uchaguzi wa watu wa Makkah na wa Madiynah na kwamba Allaah ameridhika na kuchaguliwa kwa Abu Bakr na ‘Umar na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhum) kwa sababu wote wamechaguliwa kwa njia hiyo.