Vipi Kumsaidia Kaka Yangu Mwenye Matatizo Ya Ndoa Na Iymaan Yake Dhaifu?
Vipi Kumsaidia Kaka Yangu Mwenye Matatizo Ya Ndoa Na Iymaan Yake Dhaifu?
Swali
Assalam Alaikum Warahmatullah Wabarakatuh
Naomba munishauri nini nifanye kumsaidia kaka yangu kurejesha imani yake ya dini. Kaka yangu huyu ni mtokaji sana wa usiku kwa kufanya starehe zake mwenyewe mpaka akafika kumi na moja asubuhi ndio anaingia ndani na pia linalonisikitisha zaid siku hizi kuwa bado anafanya haya katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhwaan. Mimi kama ni dada yake inaniuma sana kumuona kipenzi changu anaenda mwendo huu. Naomba munishauri kivipi niseme nae? kivipi nimuonyeshe kama anayofanya sivo wala sio muislam anavyostahiki aishi? Naomba tafadhali nasaha kutoka kwenu kwani ni jambo linaniuma sana sana sana.
Pia nisema kuwa kishaowa na mara zote mke wake humnunua mume wake hali kaka yangu unakuta anataka kuzungumza na mke wake sasa hivi imefika hata kaka yangu akimpa mke wake pesa za matumizi nyumbani huzichukuwa lkn akaziwacha pale pale (huyo mke) bila ya kuziuliza halafu anapohitaji pesa akenda kumuomba mtu wa mbali si hata mimi (wifi yake) lakini kama shangazi huko nje na watu ambao hahitaji yeye kwenda kwa mambo kama haya hasa ukiangalia sote pale ndani tupo. Wakati nazungumza na kaka yangu akanijibu moja linalomtowa ndani ya nyumba ni kutokana na hii behaviour ya mke inamkera sana; sasa anaona bora aondoke. Naomba tafadhali munishauri nifanye nini kuweka sawa hii hali. Inanikera na kuniuma sana. Nategemea mutaweza kupata nguvu kuweza kunijibu haya karibu. Ameen
Wasalaam Alaykum
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Ni miongoni mwa itikadi yetu kuwa imani yetu inazidi na kupunguwa kutokana na amali tuzifanyazo; imani huzidi kwa kusoma Qur-aan, kuswali jamaa, kuhudhuria mihadhara, kusikiliza mawaidha na kadhalika. Na imani hupungua kwa kutenda maovu au kuwa mbali na hayo yaliyotangulia au kuwa na urafiki na wasio mpenda Allaah na dini Yake. Na hali hii ni kwa wale wenye imani zao ya dini; hivyo basi wakipewa nasaha wakikumbushwa au wakisemezwa kwa kuelezwa yenye kheri au hata wakisikia tu yenye kuwakumbusha Allaah na dini Yake huwa na hali kama hii inayotuelezea Qur-aan:
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا
"Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao hujaa khofu, na wanaposomewa Aayah Zake huwazidisha Iymaan…" [Al-Anfaal: 2]
Mwanadaam amepambiwa kupenda matamanio na ni mwenye kuyapenda ya kuvutia na starehe za kidunia iwe ni mtokaji sana wa usiku kwa kufanya starehe zake mwenyewe mpaka akafika asubuhi ndio anaingia ndani huku akijisahau kuwa na mke mwenye haki naye. Ikiwa sababu ya mume kufanya hivyo ni kuwa hana hamu na mke, au amechoka naye au anamchukia basi asiwe mwenye kumdhiki hivyo na ufumbuzi upo wa hili. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) :
وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ فَإِن كَرِهْتُمُوهُنَّ فَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللَّـهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا
Na kaeni nao kwa wema. Na mkiwachukia, basi asaa ikiwa mnachukia jambo na Allaah Akalijaalia kuwa lenye khayr nyingi. [An-Nisaa: 19]
Kwa kweli tatizo kama ulivyolieleza ni kuwa uhusiano uliopo baina ya kaka yako na mkewe ndio tatizo kubwa na inaweza kuwa shina la yote; na kama halikushughulikiwa basi hapatakuwa na ufumbuzi wa tatizo lake wala hutoweza kumsaidia kurudisha imani yake; Wewe kama dada unaweza kusema nae lakini itakuwa vyema na vizuri kama utawashirikisha wengine (jamaa) walio karibu wa pande zote mbili ili waweza kutatua matatizo yao kwani huo ndio ushauri wa Qur-aan:
وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا ﴿٣٥﴾
"Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaahu atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari." [An-Nisaa: 35]
Vilevile kwa upande mwengine ijulikane kuwa mke katika nyumba akijiweka kama ni mwanamke tu na sio mke basi huwa ni tatizo kwa mume -sio mwanamume- ambae alitegeme kupata utulivu utaoweza kumrejesha katika imani ya dini yake na kama utulivu hauko katika nyumba yake hubakia kuutafuta kwengine kwani yeye ni mwanamume na sio mume na huku ndiko kuanza kupotea kwake.
Moja katika tabia mbaya kabisa wanazokuwa nazo wanawake ni kuwanunia waume zao wakidanganyika kuwa kumnunia kutapeleka mume kuregeza msimamo wake na kuelekea kwenye yale anayoyataka mke, hili si kweli kwani mke kuwa na tabia ya kumnunia mumewe kunapelekea mume kutokuwa na mapenzi na mke huyo kwani tabia ya kununa sio tabia anayotarajiwa awe nayo mke kwa mume ampendae, bali hutarajiwa awe na wivu wenye mipaka na badala ya kununa ovyo alitarajiwa amuongoze na kumshauri kama anayoyataka ni ya kheri na ni yenye kujenga familia yao.
Chanzo cha makosa ni mume kutoka usiku kucha bila ya kurudi nyumbani kwa mkewe na kutimiza haki za mke. Kwani mke anamhitaji mumewe kwa kila jambo sio kumpa pesa za matumizi tu. Miongoni mwa haki muhimu ni kuwa naye kitandani atakapomhitaji kupata utulivu wa nfasi na kukidhiwa matamanio yake ya kimwili kama ilivyo baina ya mke na mume. Kwa hiyo tunakushauri dada yetu ufanye chini juu kuwakusanya watu wa mume na wa mke walio karibu nao upate sulhu katika tatizo hilo.
Na jaribu sana kuwa pamoja na wifi yako umuonyeshe kuwa wewe uko naye katika shida zake na umfahamishe kuwa afanyayo kaka yako wewe huko radhi na utajaribu kufanya kila njia kutatua tatizo hilo lake. Pia mshauri kuwa apokee pesa za matumizi kutoka kwa mume hadi itakapopatikana sulhu. Na mfahamishe kuwa kwenda kumuomba mtu wa mbali huku mume akiwa yuko ni katika makosa na huyo mtu wa mbali kama ni wa mbali alihitaji kutafiti chanzo cha huyo mke kujua kwake kumuomba kwani na apate kumtoa katika tatizo na mumewe.
Ama kuhusu tabia ya kaka yako kutokuwa na taqwa na kufanya maovu, hapo utakapokutana na jamaa kutafuta sulhu, unaweza pia kuwaomba wampe nasaha. Njia nyingine ni wewe kusema naye kwa upole na vizuri na kumpatia mawaidha, makala zenye kufahamisha haki za mke na mume na pia ukiweza kumpatia Shekhe atakayeweza kumpa nasaha itakuwa vizuri zaidi. La muhimu ni kwamba aweze kutimia haki ya mkewe kwanza, kisha uongofu ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anamuongoa Amtakaye na kwa du'aa zako pamoja na mkewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atazitakabalia InshaAllaah.
Tunakuombea wepesi katika kazi hiyo, na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akulipe kwa iymaan yako ya kupenda kumuongoza kaka yako na kusuluhisha baina ya wifi yako na kaka yako kwa ajili ya usalama wa ndoa yao.
Na Allaah Anajua zaidi