Abu 'Ubaydah 'Aamir Bin Al-Jarraah (رضي الله عنه): Mwaminifu Wa Ummah
Abu 'Ubaydah 'Aamir Bin Al-Jarraah - Muaminifu Wa Ummah Huu
Muhammad Faraj Saalim As-Sa’y (Rahimahu Allaah)
YALIYOMO
Nasaba Yake
Sifa Zake
Kusilimu Na Hijra Yake
Mitihani Yake
Hakimu Muaminifu
Ustahamilivu Wake
Uaminifu Wake
Kifo Chake
Nasaba yake
Jina lake kamili ni ‘Aamir bin ‘Abdillaah bin Al-Jarraah bin Hilaal bin Uhayb bin Swabbaah bin Al-Haarith bin Fihri bin Maalik bin An-Nadhar bin Kinaanah bin Khuzaymah bin Mudrikata bin Ilyaas bin Madhar bin Nizar bin Maad bin ‘Adnaan kutoka katika kabila la Quraysh. Uhusiano wake na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) unakutana kwa Fihri
Huyu ni Swahaba ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa jukumu la kuliongoza jeshi lililokwenda kumsaidia ‘Amru bin Al-‘Aas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika vita vilivyojulikana kwa jina la 'Dhaatus Salaasil'.
Katika vita hivyo alipewa uongozi wa jeshi ambalo ndani yake alikuwemo Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhum).
Huyu ni Swahaba ambaye Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema juu yake:
"Hakika kila umma una mwaminifu wake, na mwaminifu wa umma huu ni Abu ‘Ubaydah ‘Aamir bin Al-Jarraah."
Na hii haina maana kuwa Maswahaba wengine hawakuwa waaminifu, bali hizi ni sifa ambazo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipenda kuwahusisha nazo Sahibu zake (Radhiya Llaahu ‘anhum), mfano aliposema:
"Mwenye huruma kupita wote kwa umma wangu ni Abu Bakr."
Hii haikuwa na maana kuwa wengine hawakuwa na huruma.
Na aliposema:
"Mkali kupita wote katika kufuata maamrisho ya Allaah ni Umar"
Hii haikumaanisha kuwa wengine walikuwa wakisahilisha katika kufuata maamrisho.
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mwenye uso mkunjufu, mwembamba, mrefu, mwepesi, na jicho hutulia na kufurahi kila linapomuona. Alikuwa mpole mwenye huruma.
‘Abdullaah bin ‘Umar bin Al Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhuma) alisema juu yake:
"Watatu katika Makureshi walikuwa wenye nyuso kunjufu, mwenendo na tabia njema, wingi wa hayaa, na hawasemi uongo wanapozungumza na wala hawakukadhibishi unapozungumza nao; Abu Bakr Asw-Swiddiyq, ‘Uthmaan bin ‘Affaan na Abu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah."
Imepokelewa pia kuwa siku moja ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliwaambia watu waliokuwa naye:
"Kila mtu atamani anachokitaka."
Kila mmoja akasema anachotamani, mwisho ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:
"Ama mimi natamani nyumba iliyojaa watu mfano wa Abu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah."
Hata hivyo, katika vita dhidi ya maadui wa Allaah, Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mkali na hatari kama simba.
Alisilimu siku iliyofuata baada ya kusilimu Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kwa ajili hiyo alikuwa miongoni mwa wachache wa mwanzo walioingia katika dini hii tukufu ambao Allaah (Subhanahu wa Ta’ala) Alisema juu yao:
وَاذْكُرُوا إِذْ أَنتُمْ قَلِيلٌ مُّسْتَضْعَفُونَ فِي الْأَرْضِ تَخَافُونَ أَن يَتَخَطَّفَكُمُ النَّاسُ فَآوَاكُمْ وَأَيَّدَكُم بِنَصْرِهِ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴿٢٦﴾
Na kumbukeni pale mlipokuwa wachache, mkikandamizwa ardhini, mnakhofu watu wasikunyakueni. (Allaah) Akakupeni makazi na Akakutieni nguvu kwa nusra Yake, na Akakuruzukuni katika vizuri mpate kushukuru. [Al-Anfaal: 26]
Alisilimishwa na Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) siku moja yeye pamoja na ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf na ‘Uthmaan bin Madh’uun na Al-Arqam bin Al-Arqam (Radhiya Llaahu ‘anhum), kisha Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawapeleka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambako mbele yake walizitamka shahada mbili, na kwa ajili hiyo wakawa miongoni mwa nguzo madhubuti za mwanzo zilizoisimamisha dini hii tukufu.
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Alihajir (alihama) kwenda nchi ya Uhabeshi (Ethiopia) katika hijra ya pili kisha akarudi na kuhajir tena, mara hii kuelekea Madina.
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipambana na mashaka, huzuni na mitihani mingi mikubwa alipokuwa Makkah sawa kama Waislamu wenzake, lakini mtihani mkubwa aliopambana nao usioweza kusahaulika na hata masikio hayakubali kusadiki wala moyo hauwezi kuustahamilia ulikuwa siku ya vita vya Badr.
Katika vita vya Badr, siku ambayo Allaah Alitaka aihakikishe haki kwa maneno Yake, na Aikate mizizi ya makafiri. Siku hiyo Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliingia vitani akipambana kwa ushujaa mkubwa huku akikata kila kichwa cha kafiri aliyemkaribia. Hofu iliingia ndani ya nyoyo za Makureshi, wakawa wanamkimbia kila anapowasogelea huku yeye akisonga mbele bila ya kuhofia mauti. Lakini mtu mmoja katika jeshi la maadui alikuwa akimsogelea na kusimama mbele yake huku akimshambulia akijaribu kumzuia asisonge mbele. Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alijaribu kumuepuka na kuelekea kwengine, lakini mtu huyo aliendelea kumfuata huku na kule akimzonga na kumshambulia kwa upanga wake ili amzuie asiendelee kupambana na adui wa Allaah, na hatimaye mtu huyo akageuka kuwa ngome isiyopitika baina yake na baina ya adui.
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliposhindwa kustahamili na alipoona kuwa akitaka kuendelea kuipigania dini ya Allaah hana budi kupambana na mtu huyo, akaamua kufanya hivyo. Na kwa pigo moja la upanga wake alimkata kichwa.
Usijishughulishe sana kutaka kumjua ni nani huyu, kwani mtu huyo alikuwa ni ‘Abdullaah bin Al-Jarraah baba yake Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akipigana upande wa washirikina.
Allaah kwa ajili yake Akateremsha aya inayosema:
لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ ۖ وَيُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ رَضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ ۚ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ اللَّـهِ ۚ أَلَا إِنَّ حِزْبَ اللَّـهِ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿٢٢﴾
Hutokuta watu wanaomuamini Allaah na Siku ya Mwisho kuwa wanafanya urafiki na kuwapenda wanaompinga Allaah na Rasuli Wake, japo wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao (Allaah) Amewaandikia katika nyoyo zao iymaan, na Akawatia nguvu kwa Ruwh (Wahyi) kutoka Kwake, na Atawaingiza Jannaat zipitazo chini yake mito ni wenye kudumu humo. Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hao ndio kundi la Allaah. Tanabahi! Hakika kundi la Allaah ndio lenye kufaulu. [Al-Mujadaalah: 22]
Haya si ya kushangaza kwa Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye wengi katika Maswahaba wakubwa (Radhiya Llaahu ‘anhum) walitamani kuifikia daraja ya imani yake iliyoshuhudiwa hata na Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Ulipokuja ujumbe kutoka Najraan (Yemen) kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumtaka awape mtu aliyeridhika naye katika Maswahaba wake ili awe hakimu baina yao wanapohitalifiana katika mambo mbali mbali ya maisha yao pamoja na yale yanayohusu mali zao, aliwaambia:
"Rudini mchana nitakupeni mwenye nguvu na muaminifu afuatane nanyi."
Anasema ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu):
"Siku hiyo niliwasili mapema sana Msikitini kuswali Adhuhuri (ili nipewe mimi jukumu hilo), na sikupenda kupewa jukumu hilo isipokuwa kwa sababu ya kuitamani kwangu ile sifa ya uaminifu."
Baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumaliza kutuswalisha akaanza kutazama kulia na kushoto akitafuta, na mimi nikawa najisogeza mbele apate kuniona. Akawa anaendelea kutafuta huku na kule mpaka alipomuona Abu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah, akamuita na kumuambia:
"Fuatana nao uwe hakimu katika waliyokhitalifiana baina yao."
Nikajisemea nafsini mwangu:
"Abu ‘Ubaydah keshaichukua (daraja ile)."
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuwa muaminifu tu, bali alikuwa mwenye nguvu na mstahamilivu pia.
Siku moja alipotakiwa kuongoza jeshi litakalokwenda kuuteka msafara wa Kikureshi, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na chakula cha kutosha cha kuwapa isipokuwa mfuko wa tende. Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akawa anawagawia watu wake kila mtu tende moja kwa siku. Mtu anainyonya tende hiyo kama mtoto mchanga anavyonyonya ziwa la mama yake, na akishaimaliza anakunywa maji.
Siku ya vita vya Uhud baada ya maadui kufanikiwa kulizunguka jeshi la Waislamu na kuwapiga vibaya, Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa miongoni mwa watu kumi waliobaki katika uwanja wa vita waliomzunguka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakimlinda na kumkinga na mikuki ya makafiri iliyokuwa ikirushwa kutoka huku na kule, huku makafiri wakisonga mbele na kupiga kele:
"Tuonesheni alipo Muhammad, tuonesheni alipo Muhammad!"
Wakati huo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa keshajeruhiwa vibaya sana; jino lake lilivunjika, kipaji cha uso wake kilipasuka na shanga mbili za ngao yake zilikatika na kuzama ndani ya shavu lake tukufu, huku uso wake ukivuja damu.
Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa karibu alijaribu kuzitoa shanga zile, lakini Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamuambia:
"Nakula kiapo juu yako uniachie mie."
Akamuchia, na Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akihofia kuzitoa kwa mikono asije akamuumiza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamua kuzitoa kwa meno yake.
Akaibana shanga ya mwanzo kwa meno yake ya upande wa kulia kwa nguvu zake zote na ustadi, akafanikiwa kuitoa lakini jino lake moja liling'oka na kuanguka.
Kisha akaibana shanga ya pili kwa meno yake ya upande wa kushoto akafanikiwa pia kuitoa na jino lake la pili likang'oka na kuanguka.
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alishuhudia vita vyote alivyoshiriki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tokea alipokuwa sahibu yake mpaka alipofariki dunia.
Kama alivyokuwa muaminifu wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliendelea kuwa muaminifu wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr na pia wakati wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhum).
Bila kujali akiwa ni kiongozi au askari wa kawaida, alipigana chini ya bendera ya Uislam kwa ajili ya kulinyanyua neno la Allaah kila bendera hiyo ilipokwenda
Abu ‘Ubaydah ((Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa askari wa kawaida wakati Khaalid bin Al-Waliyd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa akiongoza majeshi ya Waislamu katika mapambano makubwa na muhimu sana dhidi ya makafiri katika nchi ya Shaam. Khalifa wa Waislamu ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alituma mjumbe amkabidhi Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) barua yenye amri ya kumpa yeye uongozi wa jeshi hilo.
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimtaka mjumbe huyo asimjulishe mtu juu ya amri hiyo mpya mpaka baada ya vita kumalizika, kwa sababu usiku huo jeshi lilikuwa katika mapambano yake ya mwisho yatakayoupa ushindi mkubwa jeshi la Waislamu.
Baada ya vita kumalizika na Waislamu kushinda, Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuendea Khaalid (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kumkabidhi barua.
Khaalid akamuambia:
"Allaah Akurehemu ee Abu ‘Ubaydah, jambo gani lililokuzuia usinionyeshe barua tokea ulipoipokea?"
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamuambia:
"Sikupenda kukuharibia vita vyako. Sina haja ya ufalme wa kidunia mimi Wala siitumikii dunia. Sisi sote ni ndugu kwa ajili ya Allaah."
Na hivi ndivyo walivyokuwa – Allaah awe radhi nao; hawakuwa wakijishughulisha na vyeo wala dunia, bali walikuwa watu waliojitolea nafsi zao na roho zao na mali zao kwa ajili ya kulinyanyua neno la Allaah.
Wakati Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa Shaam akiongoza majeshi ya Kiislamu yaliyokuwa yakiendelea kuteka nchi baada ya nchi; kutoka Euphrates upande wa mashariki hadi Asia minor kaskazini, maradhi ya tauni yasiyopata kuonekana mfano wake yaliivamia nchi ya Shaam na kuua watu wengi sana.
Alipoona maisha ya Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) yamo hatarini, ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa Khalifa wa Waislamu wakati ule, alimtuma mjumbe kwa Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akiwa na barua iliyoandikwa yafuatayo:
"Ninakuhitajia sana. Itakapokufikia barua hii wakati wa usiku, usingoje asubuhi iingie ufunge safari kuja kwangu. Na ikikufikia wakati wa mchana usiungoje usiku uingie, uifunge safari ya kuja kwangu."
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alifahamu kusudi la barua ile, nayo ni kumtaka aondoke Shaam asije akapatwa na maradhi ya tauni.
Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akamjibu ifuatavyo:
"Ee Amiri wa Waumini, nishaijua haja yako kwangu. Mimi ni askari katika askari wa Kiislamu na sipendi kujiepusha na kile kinachowasibu wenzangu. Na sitaki kuachana nao ndugu zangu, mpaka pale Allaah Atakapoipitisha amri Yake.
Itakapokufikia barua yangu hii, unipe udhuru katika haja yako na uniruhusu nibaki."
‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipoisoma alilia sana, hata walio karibu naye wakamuuliza:
"Amekwishafariki dunia Abu ‘Ubaydah?"
Akasema:
"Hapana. Lakini kifo chake kipo karibu."
Hakukosea ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kwani Abu ‘Ubaydah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipata maradhi ya tauni, na alipokuwa akikata roho aliwausia waliokuwepo kwa kuwaambia:
"Hakika mimi nakupeni usia wangu, mukiufuata mtakua katika kheri;
Simamisheni Swalah, fungeni mwezi wa Ramadhaan, toeni Sadaka, msiache kufanya ibada ya Hija na ya ‘Umrah. Mupeane usia mwema baina yenu, na muwape nasaha njema viongozi wenu na msiwaghushi, na isikubabaisheni dunia kwa sababu mtu hata aishi miaka elfu, lazima siku moja atakuwepo juu ya njia hii mnayoiona niliyopo mimi hivi sasa juu yake. Was-Salaamu ‘Alaykum wa RahmatuLlaahi wa Barakaatuh."
Kisha akageuka kumtizama Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu), akamuambia:
"Swalisha watu."
Kisha akafariki dunia. Na Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akainuka na kuwahutubia watu akasema:
"Enyi watu! Tumeondokewa na mtu ambaye Wa-Allaahi sijui kama nimewahi kumuona mwenye ustahamilivu na upole kupita yeye, na mwenye kujiweka mbali na shari kupita yeye. Wala sijapata kumuona mtu mwenye kuipenda Akhera yake na mwenye kupenda kuwanasihi watu kupita yeye.
Kwa hivyo muombeeni rehma Allaah Akurehemuni."
Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka hamsini na nane kwa ugonjwa wa tauni uliojulikana kwa jina la 'Twa’uun Amuwaas' kutokana na jina la mji wa Amuwaas (Jordan) ulioshambuliwa na maradhi hayo. Na hii ilikuwa katika mwaka wa kumi na nane, na wengine wakasema kuwa amefariki katika mwaka wa kumi na saba Hijra.