Mu'aadh Bin Jabal (رضي الله عنه)
Mu'aadh Bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'Anhu)
Muhammad Faraj (Rahimahu Allaah)
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) Anarudi Madiynah
Kuvunja Masanamu
Anawalingania Mayahudi Katika Dini Ya Allaah
Jihadi Yake
Elimu Yake
Ibada Yake
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)Anapelekwa Yemen
Wa-Allaahi Mimi Nakupenda
Niusie
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Anarudi Kutoka Yemen
Mwalimu Kisha Gavana Wa Shaam
Kufariki Kwake
Jina lake ni Mu’aadh bin Jabal bin ‘Amru bin ‘Aws bin ‘Aidh bin Uday bin Ka’ab bin ‘Amru bin ‘Adiy bin Sa’ad Al-Khazraji Al-Answaariy, na umaarufu wake ni Abu Abdir-Rahmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu). Alizaliwa mwaka wa ishirini kabla ya Hijrah.
Katika mwaka wa kumi na tatu tokea kupewa utume Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na baada ya washirikina wa Makkah kukataa kumfuata, na badala yake wakawa wanawatesa na kuwaadhibu wale wachache waliomuamini, uliwasili Makkah kutoka Madiynah ujumbe wa watu sabini na tano uliokuja kukutana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa siri kwa ajili ya kufungamana naye katika fungamano lililokuja kujulikana kwa jina la 'Fungamano la ‘Aqabah la pili'.
Waliagana kukutana naye nyakati za usiku katika kijiji kimoja pale Mina karibu na Jamarat la mwanzo.
'Jamarat la mwanzo' ni yule anayeitwa 'shetani mkubwa', anayepigwa mawe siku za Hija.
Kabla ya kufungamana naye, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliuhutubia ujumbe huo, akasema:
"Nafungamana nanyi kwa masharti yafuatayo; Mnipe himaya kama mnayowapa watu wenu, na mufuate amri na kutii na kutoa katika dhiki na faraji, na katika kuamrisha mema na kukataza mabaya, na musimamie kazi ya Allaah bila ya kuogopa lawama za wenye kulaumu".
Wote kwa pamoja waliyakubali masharti hayo, wakafungamana naye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa kumpa mkono mmoja baada ya mwengine huku wakimuahidi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa watamlinda kwa hali na mali atakapohamia katika mji wao – Madiynah.
Katika mikono iliyonyoshwa kufungamana naye siku hiyo ulikuwa mkono wa kijana mdogo mwenye umri wa miaka kumi na nane - Mu’aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)Anarudi Madiynah
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alisilimu mikononi mwa Mus’ab bin ‘Umayr (Radhwiya Allaahu ‘anhu)aliyepelekwa Madiynah na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa ajili ya kuwafunza Dini na kuwasomesha Qur-aan tukufu, na hii ilikuwa baada ya Fungamano la mwanzo lililofanyika mwaka mmoja kabla, mahali pale pale lilipofanyika Fungamano la pili.
Juu ya udogo wa umri wake, Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alikuwa ‘Aalim miongoni mwa Ma’ulamaa waliokuwa wakitamba kwa elimu yao katika Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na alikuwa mcha Mungu sana.
Alirudi Madiynah baada ya kuhudhuria fungamano hilo akiwa na nia pamoja na hamasa kubwa ya kuilingania Dini ya Allaah na kuizamisha mizizi yake vizuri katika mji wa Madiynah kwa ajili ya kuutayarisha mji huo kuwa makao makuu ya Dini ya Kiislamu na ngome imara itakayomlinda Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pale atakapohamia kwao, na ili pia pawe mahali itakapoanza da’awah ya kuieneza Dini hii pembe zote za dunia.
Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu)akishirikiana na kijana mwenzake aitwae Tha’alaba bin Athamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu)pamoja na baadhi ya vijana waliosilimu wa kabila la Bani Salamah, walikuwa kila wanapopata fursa katika giza la usiku wakiyaendea masanamu ya washirikina na kuyavunjavunja au kuyatupilia mbali.
Katika masanamu waliyokuwa wakiyashambulia lilikuwa lile la ‘Amru bin Jamuuh mmojawapo wa wakuu wa kabila la Bani Salamah aliyekuwa na sanamu la mbao alolipa jina la Manaat.
Walikuwa wakiliiba sanamu hilo nyakati za usiku na kulitupa ndani ya mojawapo ya mashimo ya kijiji cha Bani Salamah yaliyokuwa na vinyesi vya watu ndani yake, na ‘Amru anapoamka asilikute sanamu lake, huanza kutukana na kulaani huku akisema:
"Ole wenu! Muovu gani aliyemfanyia uadui mungu wetu usiku wa leo?" Kisha anatoka na kuanza kulitafuta, na anapolikuta limetupwa juu ya uchafu kichwa kimeangukia kinyesi, huliokota na kulichukuwa nyumbani, akalikosha na kulisafisha, kisha analipaka mafuta mazuri huku akiliambia:
"WaLlaahi ningelimjuwa aliyekufanyia hivi ningemdhalilisha."
Ikawa kila siku wakati wa usiku ‘Amru anapokwenda kulala, vijana hao huliendeea sanamu lakena kufanya yale yale.
Siku moja baada ya kuchoshwa na kazi ya kulifuta na kulisafisha sanamu lake, akaamua kulifunga na upanga, kisha akaliambia:
"WaLlaahi mimi simjui anayekutendea haya, lakini ikiwa una kheri yoyote basi jilinde kwa upanga huu." Kisha akaenda kulala.
Vijana wale wakaja na kulichukua sanamu hilo, wakalifunga na mzoga wa mbwa na kama kawaida yao wakalitupa ndani ya mojawapo ya mashimo ya kufanyia haja ya kijiji cha Bani Salamah, na ‘Amru alipoamka asilione sanamu lake. Akatoka na kuanza kulitafuta, na kama kila siku akalikuta limetupwa ndani ya shimo, na safari hii likiwa limefungwa na mzoga wa mbwa.
Akalitizama muda kidogo kisha akalitungia shairi akiliambia:
"WaLlaahi ungekuwa Mungu wa kweli, usingekubali kuwa dhalili, ukatupiliwa mbali, pamoja na mzoga wa mbwa ndani ya shimo hili."
‘Amru alisilimu baadaye na akawa Muislamu mwema.
Anawalingania Mayahudi Katika Dini Ya Allaah
Tokea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipohamia Madiynah, Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alikuwa daima yupo pamoja naye akiipokea Qur-aan moja kwa moja kutoka mdomoni mwake, huku akijifunza shari’ah za Dini kutoka kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), jambo lililomfanya awe msitari wa mbele miongoni mwa Maulamaa wa wakati wake, na pia katika kuwalingania watu wa mji wake.
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)hakuridhika na kuwalingania watu wa kabila lakena Waarabu peke yao pamoja na kuvunja masanamu yao, bali alikuwa pia akiwalingania Mayahudi wa pale Madiynah ambao hapo mwanzo walikuwa wakizungumza sana juu ya Mtume mpya atakayekuja. Kwani wasfu wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) umeandikwa ndani ya Taurati, lakini zilipowafikia habari za kuja kwake, walimkanusha na kumkataa, na kwa ajili hiyo Mu’aadh akifuatana na Bishr bin Al Bara-a aliwaendea na kuwaambia:
"Enyi Mayahudi, muogopeni Allaah na ingieni katika Dini ya Kiislamu, kwani si nyinyi mliokuwa mkitubashiria juu ya kuja kwa Mtume huyu wakati ule tulipokuwa washirikina tukiabudu masanamu, kisha mkawa mnatupa wasfu wake? Na mlipokuwa mkipigana vita kabla ya kuja kwa Mtume huyu si mlikuwa mkiomba mpate ushindi kwa baraka zake?
Akasema Sallaam bin Mishkam mmoja katika Mayahudi wa kabila la Bani Nadhiyr:
"Hana wasfu wowote katika ule tunaoujuwa, na wala si huyu tuliyekuwa tukikubashirieni."
Ndipo Allaah Alipoteremsha kauli Yake;
"Na kilipowajia Kitabu kitokacho kwa Allaah kinachothibitisha waliyo nayo - na wao walikuwa wakitafutia ushindi kuwashinda makafiri - yalipowajia yale waliyokuwa wakiyajua waliyakanusha. Basi laana ya Allaah juu ya wakanushao!" Al-Baqarah: 89.
Jihadi Yake
Tokea siku ile alipounyosha mkono wake na kuuingiza ndani ya mkono wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) huku akimuahidi kuilingania Dini aliyokuja nayo, Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alisimama imara katika kulinyanyua neno la Allaah ili liwe juu, na akaendelea juu ya njia hiyo maisha yake yote.
Alishiriki katika vita vya Badr, Uhud, Taabuuk na vita vyote alivyoshiriki ndani yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Alikuwa daima ubavuni mwake, na baada ya vita vya Taabuuk, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimpeleka Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)Yemen kwa ajili ya kuwaongoza watu wa huko na kuwafundisha Dini pamoja na Kitabu cha Allaah, na hakurudi tena Madiynah mpaka baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kufariki.
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)hakuacha kupigana jihadi hata baada ya kufariki kwa Mtume wa Allaah, bali alishiriki katika vita vingi vilivyopiganwa katika nchi ya Shaam na kwengineko.
Juu ya udogo wa umri wake, Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alikuwa ‘Aalim aliyezama katika bahari ya elimu, na siku ile Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akiwasifia Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum) alisema:
"Mwenye huruma kupita wote katika umma wangu Abu Bakr, na mkali kupita wote katika Dini ya Allaah ni ‘Umar, na mwenye kuona hayaa kupita wote ‘Uthmaan, na mwenye hekima kupita wote katika kutoa hukmu ‘Aliy, na mwenye elimu zaidi juu ya halali na haramu Mu’aadh bin Jabal."
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alipata sifa zote hizo akiwa na umri mdogo sana, kwani wakati alipofariki alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitatu tu.
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwausia Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) wajifunze Qur-aan kutoka kwa wanne, na Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alikuwa katika wanne hao. Alisema:
"Jifunzeni Qur-aan kutoka kwa wanne; Ibnu Mas’uud, Saalim mawla Abi Hudhayfah, Ubay bin Ka’ab na Mu’aadh bin Jabal."
Al-Bukhaariy 7/125 Hadiyth nambari 3806, Muslim 2464
Abu Muslim Al-Khawlaniy, na huyu ni katika wacha Mungu maarufu wa Taabi'ina (waliokuja baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wakawaona Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) anasema:
"Niliingia Msikiti wa mji wa Hims nikawakuta Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) watu wazima wapatao thelathini, na miongoni mwao akiwemo kijana mwenye macho meusi na meno yenye kung'ara aliyekuwa amekaa kimya. Na kila watu wanapokhitalifiana au wanapotatanishwa na jambo humwendea kijana huyo na kumuuliza. Nikamuuliza aliyekaa karibu nami: 'Nani huyu?' akaniambia; 'Mu’aadh bin Jabal'.
AtwTwabaqaat Al-Kubra 3/590
‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alipozuru nchi ya Shaam aliwahutubia watu wa huko na kuwaambia:
"Mwenye kutaka kuuliza juu ya fardhi amwendee Zayd bin Thaabit, na mwenye kutaka kuuliza juu ya fiqh amwendee Mu’aadh bin Jabal."
Imepokelewa pia kuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu)aliwahi kusema:
"Nikimpa uongozi Mu’aadh na Mola wangu akiniuliza: 'Kwa nini umempa uongozi?' Nitasema: "Nilimsikia Mtume wako akisema; 'Hakika Maulamaa watajapohudhurishwa mbele ya Mola wao ‘Azza wa Jalla, Mu’aadh atakuwa mbele yao."
Rijaal Hawla ar-Rasuul –Khaalid Muhammad Khaalid
Imepokelewa pia kuwa Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wanapokuwa wanazungumza, na Mu’aadh yuko pamoja nao, walikuwa kila mara wakimuangalia, na hii inatokana na haiba aliyokuwa nayo Swahaba huyu mtukufu (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Juu ya kuwa alikuwa akipenda kukaa kimya, lakini anapoanza kuzungumza wote kwa pamoja hunyamaza na kumsikiliza.
Anasema mmoja katika Swahibu zake:
"Anapozungumza Mu’aadh, inakuwa kama kwamba vipande vya lulu vinadondoka kutoka mdomoni mwake".
Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alikuwa mcha Mungu sana mwenye kupenda kuswali. Alikuwa akishamaliza kuswali Msikiti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akirudi kijijini kwake, kijiji cha Bani Salamah waliokuwa wakiishi nje ya mji wa Madiynah na kuwaswalisha watu wa kabila lakeMsikitini kwao.
Alikuwa anaposwali akiona kama kwamba Swalah yake hiyo ni ya mwisho na kwamba hatopata tena fursa nyingine ya kuswali.
Imepokelewa kuwa alikuwa akimuusia mwanawe kwa kumwambia: "Unaposwali, swali Swalah ya kuaga, kama kwamba hutopata tena fursa ya kuswali Swalah nyengine. Na elewa ewe mwanangu kuwa mtu anakufa baina ya mema mawili; Jema alilojitangulizia na jema aloliacha asilifanye."
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)Anapelekwa Yemen
Baada ya vita vya kuuteka mji wa Makkah 'Fat-hu Makkah' na vita vya Taabuuk kumalizika, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliamua kuwaacha Makkah Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu)na ‘Utab bin Usayd (Radhwiya Allaahu ‘anhu)ili wawe magavana wa mji huo na kuwafundisha watu wake Qur-aan pamoja na hukmu za Dini.
Na haukupita muda mrefu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaamua kumpeleka Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)Yemen kwa ajili ya jukumu hilohilo.
Anasema Al-Bukhaariy katika mlango wa kupelekwa Abu Muusa Al-Ash'ariy Yemen ili awe gavana wa huko, na hii ilikuwa kabla ya Hija ya mwisho ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
"Ametuhadithia Muusa, aliyehadithiwa na Abu Awuanah aliyehadithiwa na ‘Abdul-Malik, kutoka kwa Abu Bardah kuwa; Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwapeleka Yemen Abu Muusa na Mu’aadh bin Jabal na kila mmoja alipewa sehemu yake, na Yemen ilikuwa sehemu mbili wakati huo, kisha akawaambia:
"Yarahisisheni mambo wala msiyafanye magumu, na muwapendezeshe watu wala msiwachukize."
Imepokelewa pia kuwa alipokuwa akimsindikiza Mu’aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akitembea kwa miguu huku Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)akiwa amepanda mnyama, akawa anamwambia:
"Ewe Mu’aadh! unakokwenda kuna watu wa kitabu (Mayahudi na Manaswara), basi utakapokutana nao, jambo la mwanzo utakalofanya ni kuwalingania katika 'La ilaaha illa Allaah' na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Wakikutii katika hilo utawajulisha kuwa Allaah Amewafaradhishia Swalah tano kila usiku na mchana. Na wakikutii katika hilo utawajulisha kuwa Allaah Amewafaradhishia kutoa Zakaah zitakazochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kupewa masikini wao. Na watakapokutii katika hilo usije ukawalazimisha tena kutoa katika mali zao wanazozipenda sana (muhimu watoe Zakaah na kiwango kiwe kinachokubaliana na shari’ah), na uigope du’aa ya aliyedhulumiwa, kwani haina kizuizi baina yake na baina ya Allaah (hapana kitakachoweza kuizuia du’aa ya aliyedhulumiwa isifike kwa Allaah)."
Imepokelewa pia siku hiyo alimuusia mambo mengi, kisha akamuambia:
"Ewe Mu’aadh! Huenda usionane na mimi tena baada ya mwaka wangu huu. Na huenda ukaja Msikitini kwangu hapa na kulipitia kaburi langu." Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alilia sana baada ya kujua kuwa anafarikiana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa mara ya mwisho. Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Usilie (sana) ewe Mu’aadh, kwani kilio kinatokana na Shaytwaan."
Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaugeuza uso wake kuelekea upande wa mji wa Madiynah, akasema:
"Wanaonistahiki zaidi ni wacha Mungu, wowote watakaokuwa na popote watakapokuwa."
Kisha akamwambia:
"Ewe Mu’aadh! Nakupeleka kwa watu wenye nyoyo laini na wenye kuipigania haki mara mbili. Kwa hivyo pigana pamoja na atakayekupa Allaah katika hao dhidi ya watakaokuasi."
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alibahatika kupata sifa ambayo kila Muislamu anatamani aipate, nayo ni mapenzi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Imepokelewa kuwa siku aliyokuwa akimsindikiza kuelekea Yemen, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliuingiza mkono wake mtukufu ndani ya mkono wa Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu)kisha akamwambia:
"Ewe Mu’aadh! WaLlaahi mimi nakupenda."
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)akasema:
"Na mimi WaLlaahi nakupenda ewe Mtume wa Allaah."
Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipomuambia:
"Ewe Mu’aadh! Nakuusia Kila utakapomaliza kusali usiache kusema; 'Allaahumma a’inniy ‘alaa dhikrika wa shukrika wa husnu ‘ibaadatika.'
Niusie
Imepokelewa pia kuwa Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alimwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
"Niusie."
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Mche Allaah popote utakapokuwa."
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)akasema:
"Niongeze."
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Ukitenda ovu, lifuatilie na jema litalifuta."
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)akasema:
"Niongeze."
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Ishi na watu kwa mwenendo na tabia njema."
Al-Bidaayah wan-Nihaayah – juz. 5
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)Anarudi Kutoka Yemen
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alifariki dunia wakati Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)bado yupo Yemen, akarudi Madiynah wakati wa ukhalifa wa Ab Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Wakati wa ukhalifa wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu)ulikuja ujumbe kutoka Shaam na kumwambia:
"Ewe Amiri wa Waislamu! Watu wa Shaam ni wengi na wanahitajia waalimu wa kuwafundisha Dini ya Allaah."
‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu)akawachagua Maswahaba watatu akiwemo Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu)na kuwapeleka huko, na alipofariki dunia Abu ‘Ubaydah ‘Aamir bin al-Jarraah aliyekuwa gavana wa nchi ya Shaam, ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alimchagua Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)kushika mahali pake, na Mu’aadh akakubali, lakini hakuishi muda mrefu naye pia akafariki dunia.
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alifariki dunia katika mji wa Amuwas uliopo baina ya Baytul Maqdis na Ramalah katika nchi ya Palestina, na alifariki kwa maradhi ya tauni yaliyopewa jina la mji huo wa Amwas (Taa’uun Amwas). Maradhi haya yaliua zaidi ya watu elfu ishirini, na katika riwaya nyengine; zaidi ya watu elfu thelathini na tano.
Alipokuwa akiirudisha roho kwa Mola wake Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alikuwa akisema:
"Najikinga kwa Mola wangu na usiku ambao asubuhi yake inaelekea motoni. Nayakaribisha mauti, nayakaribisha kwa maua. Mola wangu nilikuwa nikikuogopa, lakini leo nakuomba. Mola wangu unajua kuwa sikuwa nikiipenda dunia wala sikuwa nikipenda kubaki ndani yake muda mrefu, wala sikuwa nikiipenda kwa ajili ya kupandisha miti, bali nilikuwa nikiipenda kwa ajili ya kukaa pamoja na Ma’ulamaa na kukaa katika vikao vya kukutaja."
Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu)alifariki dunia katika mwaka wa kumi na nane baada ya Hijrah akiwa na umri wa miaka thelathini na mitatu.