Nini Hukmu Ya Sajdatut-Tilaawah (Sajda Ya Kisomo)

 

Nini Hukmu Ya Sajdatut-Tilaawah (Sijda Ya Kisomo)

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum. Kwanza napenda kumshukuru Allah kwa kunipa uzima na kuniwezesha kupata fursa hii ya kuuliza maswali Na kwa uhakika shukurani zote in zake. Na alafu napenda kuwashukuru maustadh wote ambao wamechangia kwa kuendesha hichi kiungo. Swali langu ni je tunatakiwa kusujudu wakati tukisikia Qur-aan? na kama ni kweli mbona jambo hili halifanywi katika jamii? Au ni bora kusujudu wakati mtu akisikia Qur-aan na si lazima?  Sijawahi kusikia mtu au Swahaba kusujudu katika enzi za kipenzi chetu    (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  baada ya kusikia Qur-aan. Inawezekana maswahaba walikuwa wanasujudu lakini sijasikia mimi tu. kwahiyo inabidi sasa niulize je Swahaba walikuwa wakisujudu?. Na kama ni kweli basi naomba nielezelewe hivyo visa. Lakini nahisi kutokana na hizi aya kuwa waislam wanatakiwa kusujudu wakati wakisomewa Qur-aan lakini sina uhakika. Na kama hisia zangu ni sahihi mbona hili jambo halifanywi? na watu wanalinyamazia? Kama sikosei Aayah 21 ya Inshaqaaq  inaelekea  inawahusu makafiri ambalo wanaosikia Quran alafu hawasujudu wakajisalimisha kwenye Uislam. lakini na Aayah ya 15 ya suratul assajdah si inahusu waislam? 

 

Aayah zenyewe ni zifuatazo:

 

وَإِذَا قُرِئَ عَلَيْهِمُ الْقُرْآنُ لَا يَسْجُدُونَ ۩﴿٢١﴾

 Na wanaposomewa Qur-aan, hawasujudu. [Al-Inshiqaaq: 21]

 

Na pia,

 

 إِنَّمَا يُؤْمِنُ بِآيَاتِنَا الَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِهَا خَرُّوا سُجَّدًا وَسَبَّحُوا بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ ۩﴿١٥﴾

Hakika wanaamini Aayaat Zetu wale wanapokumbushwa nazo huporomoka kusujudu, na wakasabbih kwa Himidi za Rabb wao, nao hawatakabari. [As-Sajdah 15]

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Sajdatut-tilaawa (Sijda ya kusoma Qur-aan) ni kitendo cha Sunnah, na kitendo chochote cha Sunnah humpatia mwenye kutenda thawabu. Ni bora zaidi kujitahidi kutimiza Sunnah ambazo nyepesi kama hizo ili kupata yafuatayo:

 

  • Thawabu kwa kutenda kitendo cha Sunnah.
  • Kupata fadhila za kufanya sijdah hiyo.
  • Kudhihirisha mapenzi ya Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
  • Kuzidumisha Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
  • Kujidhalilisha kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) kwa kuweka kipaji chako cha uso chini kwenye ardhi na kusema:

سُبْـحانَ رَبِّـيَ الأَعْلـى  

         Ametakasika Rabb wangu Aliye juu

  

Aayah hizo ulizozitaja kama ulivyoona kwamba ya kwanza inawahusu makafiri na ya pili inawahusu Waumini, lakini hazileti tofauti katika hukmu ya kusujudu kwa ajili ya kusoma Qur-aan inapofika sehemu yenye alama ya kusujudu. Swahaba walikuwa wakifuata Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hivyo na sisi ni vizuri kufuata nyendo zao.

 

Vile vile tutambue kuwa kila kitu kinamsujudia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) vilivyohai na visivyo hai, sasa vipi sisi wana Aadam tusimsujudie? Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ يَتَفَيَّأُ ظِلَالُهُ عَنِ الْيَمِينِ وَالشَّمَائِلِ سُجَّدًا لِّلَّـهِ وَهُمْ دَاخِرُونَ﴿٤٨﴾

Je, hawaoni vile vitu Alivyoumba Allaah ambavyo vivuli vyake vinasogea huku na kule, kuliani na kushotoni vikimsujudia Allaah na huku vinanyenyekea?  

 

وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مِن دَابَّةٍ وَالْمَلَائِكَةُ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ﴿٤٩﴾

Na ni kwa Allaah pekee vinasujudia vyote vilivyomo mbinguni na ardhini katika viumbe vitembeavyo, na Malaika, nao hawatakabari.

 

يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ۩﴿٥٠﴾

Wanamkhofu Rabb wao Aliye juu yao, na wanafanya yale wanayoamrishwa.  [An-Nahl: 48-50]

 

Pia katika Suwrah Ar-Ra’d Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ۩﴿١٥﴾

Na kwa Allaah (Pekee) Humsujudia waliomo mbinguni na ardhini wakipenda wasipende na vivuli vyao pia (vinamsujudia) asubuhi na jioni.  [Ar-Ra'd: 15]

 

Na katika Hadiyth ifuatayo:

 

حَدَّثَنَا مُحَمَّدُ بْنُ يُوسُفَ، حَدَّثَنَا سُفْيَانُ، عَنِ الأَعْمَشِ، عَنْ إِبْرَاهِيمَ التَّيْمِيِّ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ أَبِي ذَرٍّ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم لأَبِي ذَرٍّ حِينَ غَرَبَتِ الشَّمْسُ ‏"‏ تَدْرِي أَيْنَ تَذْهَبُ ‏"‏‏.‏ قُلْتُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ‏.‏ قَالَ ‏"‏ فَإِنَّهَا تَذْهَبُ حَتَّى تَسْجُدَ تَحْتَ الْعَرْشِ، فَتَسْتَأْذِنَ فَيُؤْذَنَ لَهَا، وَيُوشِكُ أَنْ تَسْجُدَ فَلاَ يُقْبَلَ مِنْهَا، وَتَسْتَأْذِنَ فَلاَ يُؤْذَنَ لَهَا، يُقَالُ لَهَا ارْجِعِي مِنْ حَيْثُ جِئْتِ‏.‏ فَتَطْلُعُ مِنْ مَغْرِبِهَا، فَذَلِكَ قَوْلُهُ تَعَالَى ‏  وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَهَا ذَلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ‏

 

Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniuliza wakati wa machweo: “Je, unajua jua linapokwenda (wakati wa kuzama kwake)?”  Nikamjibu: “Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi.” Akasema: “Hakika linakwenda mpaka linasujudu chini ya ‘Arsh, na kutaka idhini kuchomoza tena, nalo linaruhusiwa. Na inachelewa kuwa (itafika wakati ambapo) litakaribia kusujudu lakini sijda yake haitokubaliwa, na litaomba idhini lakini litakataliwa (kutimiza mizunguko yake). Litaambiwa: ‘Rudi ulipotoka’. Hivyo, litachomoza Magharibi. Na hiyo ndiyo Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ﴿٣٨﴾

“Na jua linatembea hadi matulio yake.[1] Hayo ni Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.” [Yaasiyn 36:38)- Hadiyth ameipokea Imaam Al-Bukhaariy]

 

Na pia,

 

عن ابن عباس قال: "جاء رجل فقال: يا رسول الله، إني رأيتني الليلة وأنا نائم، كأني أصلي خلف شجرة، فسجدتُ فسجَدَت الشجرة لسجودي، فسمعتُها وهي تقول:

 

 اللّهُـمَّ اكْتُـبْ لي بِهـا عِنْـدَكَ أَجْـراً، وَضَـعْ عَنِّـي بِهـا وِزْراً، وَاجْعَـلها لي عِنْـدَكَ ذُخْـراً، وَتَقَبَّـلها مِنِّـي كَمـا تَقَبَّلْتَـها مِنْ عَبْـدِكَ دَاوُد

 

   قال ابن عباس: فقرأ   النبي صلى الله عليه وسلم سجدة ثم سَجَد، فسمعته وهو يقولُ مثلَ ما أخبره الرجل عن قول الشجرة.  " رواه الترمذي، وابن ماجه، وابن حبّان في صحيحه

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya-Allaahu 'anhu) amehadithia: "Mtu moja alikuja na kusema: "Ee Rasuli wa Allaah, nilijiona katika ndoto jana usiku nikiswali nyuma ya mti. Niliposujudu na mti ukawa unasujudu. Kisha nikausikia unasema:

 

اللّهُـمَّ اكْتُـبْ لي بِهـا عِنْـدَكَ أَجْـراً، وَضَـعْ عَنِّـي بِهـا وِزْراً، وَاجْعَـلها لي عِنْـدَكَ ذُخْـراً، وَتَقَبَّـلها مِنِّـي كَمـا تَقَبَّلْتَـها مِنْ عَبْـدِكَ دَاوُد

Ee Allaah niandikie Kwako kwa sijdah hii malipo, na nifutie kwayo madhambi, na ijaalie kwangu mbele Yako ni akiba, na nikubalie kama Ulivyomkubalia mja wako Daawuwd.

 

Ibn 'Abbaas akasema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akasoma Aayah inayotaja kusujudu kisha akasujudu na nikamsikia akisema maneno hayo hayo aliyosimulia mtu yaliyotajwa na mti."  [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake]   

 

Na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَسْجُدُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ وَالنُّجُومُ وَالْجِبَالُ وَالشَّجَرُ وَالدَّوَابُّ وَكَثِيرٌ مِّنَ النَّاسِ ۖ وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ الْعَذَابُ ۗ وَمَن يُهِنِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن مُّكْرِمٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ ۩﴿١٨﴾

18.   na mwezi na nyota, na majabali na miti na viumbe vinavyotembea, na wengi miongoni mwa watu? Na wengi imewastahiki adhabu. Na ambaye Allaah Amemdhalilisha, basi hatopata wa kumkirimu. Hakika Allaah Anafanya Atakavyo.  [Al-Hajj: 18]

 

Hata makafiri walikuwa wakiathirika na Qur-aan walipokuwa wakiisikia hadi kwamba iliposomwa kwao Suwrah An-Najm Aayah za mwisho ambazo zimetaja kumsujudia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) walisujudu bila ya kujijua. Aayah hizo ni zifuatazo:  

 

أَفَمِنْ هَـٰذَا الْحَدِيثِ تَعْجَبُونَ ﴿٥٩﴾وَتَضْحَكُونَ وَلَا تَبْكُونَ ﴿٦٠﴾وَأَنتُمْ سَامِدُونَ ﴿٦١﴾فَاسْجُدُوا لِلَّـهِ وَاعْبُدُوا ۩﴿٦٢﴾

Je, mnastaajabu kwa Al-Hadiyth hii (ya Qur-aan)?Na mnacheka na wala hamlii? Na hali nyinyi mnaghafilika, mnadharau na kushughulika na anasa? Basi msujudieni Allaah na mwabuduni Yeye. [An-Najm: 59-62]    

 

Zilipoteremshwa Aayah hizo za Suwrah An-Najm, zilkiwaathiri Makafiri wakasujudu bila ya kujijua. Habari zilienea kote hadi kuwafikia Swahaba waliokuwa Abisynia (Ethiopia) kuwa Maquraysh wameingia Uislaam. Swahaba wakarudi Makkah. Walipokuwa wanakaribia Makkah kwa muda wa msafara wa saa moja tu kutoka Makkah ikawadhihirikia ukweli kuwa Makafiri waliaathiriwa tu na Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Baadhi ya Swahaba wakarudi Abisynia na wengine wao wakaingia kwa siri mjini Makkah [Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm]

 

Kwa faida zaidi bonyeza  kiungo kifuatacho:

 

Kusujudu Kwa Ajili Ya Kusoma Aayah

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

Share