Nabii Nuuh (alayhis-salaam) Na Kubashiriwa Ajenge Safina

 

Nabiy Nuwh (alayhis-salaam) Na Kubashiriwa Ajenge Safina

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

Nahitaji kujua kuhusu Nabiy Nuwhu. (Radhwiyah Allaahu 'anhum).Hasa kuhusu kubashiriwa atengeneze safina. 

 

Wabillah taufiq.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu aliyeulizwa swali hili kuhusu Nabiy aliyekuwa Uwlul-‘Azmi (wenye azima kubwa). Manabii hawa wakiwemo Nuwh, Ibraahiym, Muwsaa, ‘Iysa na Muhammad (‘Alayhimu-salaam) walipata mitihani mikubwa nao wakasubiri subra za kipekee.

Kawaida sifa uliyotaja kwa Nabiy Nuwh kwa kusema, Radhwiya Allaahu 'anhu ni kwamba sifa hiyo inatumika kwa Swahaba. Na  'anhum' ni wingi wa 'anhu' lakini unampomzungumzia Nabii mmoja basi unasema 'Alayhis-salaam', na wengi utasema 'Alayhim-Salaam'.

 

Swali linaonekana halikumalizika na huenda muulizaji alifanya haraka kulituma. ‘Alaa kulli haal tutajaribu kuelezea kulingana na ufahamu wetu wa swali hilo. NabiyNuwh (‘Alayhis-salaam) alitumwa na Allaah kwa watu wake, naye akawaelezea wazi kabisa kuwa yeye ni muonyaji anayewabainishia kila kitu. Jambo la kwanza alilowalingania ni wamuabudu Allaah Mmoja tu kwani wao hawana Rabb Mlezi mwengine. Na lau hawatafanya hivyo basi watakuwa ni wenye kupata adhabu kali sana.

 

Lakini kama kawaida wale makafiri wakubwa walikuwa ni wenye kumkejeli kwa kumwambia yeye ni mtu tu wa kawaida. Kwa hiyo, wakawa ni wenye kumkanusha na hasa kuwa wafuasi wa Nabiy (‘Alayhis-salaam) walikuwa ni wanyonge katika jamii hiyo. Aliwalingania kwa miaka 950 mpaka tufani ikawa ni yenye kuwafikia wakiwa katika hali hiyo ya dhulma na ukafiri. Nabiy Nuwh (‘Alayhis-salaam) hakutaka chochote kutoka kwao ila wamuamini Allaah lakini walikataa katakata. Walipochoshwa na Nabii Nuwh (‘Alayhis-salaam) walimwambia: "Umejadiliana nasi na umezidisha majadiliano yako nasi, basi tuletee unayotuahidi (adhabu); ukiwa miongoni mwa wanaosema kweli. Yeye aliwajibu kuwa Allaah Akitaka hilo ni jepesi kwake wala nyinyi hamtaweza kuzuilia hilo wala kumshinda.

Nabiy Nuwh (‘Alayhis-salaam) hakuchoka bali alizidi kutia juhudi kwa kuwalingania usiku na mchana, kwa siri, kwa kelele na dhahiri lakini walizidi kumkimbia na kuziba masikio yao ili wasimsikie kabisa.

 

Katika hali hiyo aliamriwa kuunda jahazi naye atakuwa ni mwenye kulindwa na wala asizungumze nao tena. Wakubwa wa kikafiri kila walipokuwa wakipita wakimcheka kwani waliona ajabu huyu Nabiy ataiendesha jahazi yake sehemu gani kwa kuwa nchi yao ilikuwa ni bara isiyokuwa na ziwa, mto wala bahari. Wakati Allaah Aliyetukuka Alipotaka kuleta adhabu Yake ardhi ilianza kufoka maji. Hapo aliamriwa apakie humo (katika jahazi) jozi moja ya kila mnyama (dume na jike), na watu wa nyumbani kwake ila wale watakaopitiwa na hukumu Yetu na walioamini. Walioamini pamoja naye walikuwa wachache sana.

 

Baada ya hapo waliamriwa wapande katika jahazi hilo kwa jina la Allaah. Mbingu ziliteremsha maji na pia mengine yalitoka chini ya ardhi na jahazi ikawa inakwenda kwenye mawimbi kama majabali. Wakati huo Nabiy Nuwh (‘Alayhis-salaam) alimwona mwanawe aliyekuwa akighariki, naye akamwambia aingie katika hiyo jahazi lakini mtoto akawa ni mwenye kukataa huku anasema atapanda juu ya mlima, lakini akawa ni mwenye kughariki na hiyo ndiyo iliyokuwa hatima yake kwa kukanusha pamoja na wale wote waliokufuru

 

Baada ya muda ardhi iliamriwa kumeza maji yote na mbingu nazo zikaamriwa zizuie kuteremsha mvua. Jahazi yenyewe ilisimama kwenye Mlima Judi ambako baada ya muda waliweza kutoka katika jahazi na kuanza maisha yao tena. Kulingana na baadhi ya tafsiri mlima huo upo kaskazini mwa Mosul au kaskazini mashariki mwa Jazirah ibn ‘Umar katika nchi (eneo) ya Kurdistan.

 

Mazingatio kwetu ni mengi lakini yaliyo muhimu ni:

 

  •       Allaah Aliyetukuka ni Muweza wa kufanya jambo lolote.
  •       Hatima ya makafiri mbali na nguvu zao, ni mbaya, hapa duniani na kesho Aakhirah.
  •       Ujamaa na watu wema hautakufalia kitu ikiwa wewe mwenyewe hutakuwa mwema.
  •       Waumini wasiwe wasivunjike moyo na kujiona kuwa wao ni wanyonge.

 

Kwa ziada tunaweza kutazama Suwrah zifuatazo:

Huwd: 25-48

Al-A'raaf: 59 -64

Al-Muuminuun: 23 - 30

Ash-Shu'araa: 105 – 122

Nuwh: 71

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share