Halaal Kula Samaki Wanaokula Watu?
SWALI
Asalam alaykum warahamatullahi taala wabarakatu. Kwanza kabisa na mshukuru Allah kwa kutujaalia kuwa na website
A- SWALI LANGU NIKAMA IFUATAVYO:- JE, SAMAKI WANAOWEZA KULA NYAMA YA BINAADAMU, AU WANAOKULA NYAMA YA BINAADAMU (mfano: PAPA) NI HALALI KULIWA?
JIBU
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.)
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kula samaki wenye kula nyama ya binaadamu.
Hakika ni kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia muongozo kuwa maji ya bahari ni twahara na maiti yake ni halali kuliwa. Kwa hivyo, tusiwe na shaka kula chochote cha bahari ikiwa ni dagaa wadogo wenye kuliwa na samaki wakubwa wanaokula samaki wenzao au kula papa anayekula watu, ifahamike kuwa papa haishi na wanaadam na hivyo kuwa wao ndio mlo wake, au ndio mawindo yake, bali papa huishi majini na hupata mawindo yake humo na lishe yake, ama ikitokea kwa nadra sana kumpata binaadam, basi hapo huwa ni hali isiyo ya kawaida na hali hiyo huwatokea hata wanyama wengine wanaoliwa hata kuku, bata, ndege n.k. wanapopata mzoga wa binaadam. Lakini pamoja na hali hizo, kwetu tushawekewa rukhsa ya kuwala isipokuwa tu wale ambao Shari’ah imetutajia kutowala.
Na Allaah Anajua zaidi