Kuchanganya Vyombo Pamoja Na Vile Vinavyotumika Kwa Nguruwe

SWALI:

 

Asalamu Aleikum

    

Kama ilivyokawaida yangu mimi hupenda kubeba chakula nikienda kazini, siku moja tulikua tunakula meza moja na mkristo naye amebeba chakula chake kutoka nyumbani anakula wali na mchuzi, akanikaribisha nikamwambia asante, nami nikamkaribisha akachota kwa kijiko alichokua ameshaanza kulanacho chakula chake.

 

Tukaendelea kula hadi tukamaliza. Akawa anaviosha vyombo vyangu na vyake kwa pamoja, ikanijia fikra asijekua alikua anakula ngurue na ametumbukiza kijiko chake kwenye chakula changu na tena anaviosha pamoja. Je vile vibakuli vyangu nivitupe au nifanye vipi

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu vyombo vilivyotumiwa kulia nguruwe. Jambo hili mara nyingi hututatiza kwa kiasi kikubwa kwa sababu moja au nyingine. Sababu kubwa ni uchache wa elimu ya Dini yetu. Pamoja na kuwa tumeruhusiwa kula vyakula vya Ahlul Kitaab, lakini ukijua anakula nguruwe hufai kula akikukaribisha.

 

Hii inatokana na Aayah ambayo kwayo Allaah Aliyetukuka Anasema:

Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao” (5: 5).

 

Wala hutakiwi kutia wasiwasi mpaka ujue kwa yakini. Wakati mmoja Amiri wa Waumini, ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa anatembea na mtu mmoja mara yakashuka maji kutoka kwa mojawapo ya nyumba. Yule bwana akawa na wasiwasi isiwe ikawa ni najisi akataka kwenda kuuliza lakini ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamkataza kwani najisi inajulikana kwa sifa zake.

 

Wakati wa safari za jihadi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwapa ruhusa kutumia vyombo vya Wakristo na Mayahudi ikiwa vimeoshwa. Kwa hivyo, maadamu vyombo hivyo vimeoshwa hata kama vilitumiwa kupikia au kulia nguruwe vinakuwa twahara na unaweza kuvitumia bila ya wasiwasi wowote.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share