Gelatini Katika Madawa Na Vyakula Nini Hukmu Yake?
Hukmu Ya Gelatini Katika Madawa Na Vyakula
SWALI:
Asalam aleykum warahmatullah wabarakat shukrani sana kwa kuanzisha hii website ambayo inatufundisha mengi sana kuhusu Dini yetu. Allaah awape kheri ya hapa duniani na ya akhera amin.
Swali langu linahusu dawa za vitamin ambazo nimenunua ni za kumeza na nilivyozisoma ziko na gelatin na gelatin yenyewe haijaandikwa kama imetokana na mnyama au mimea je ni haramu kama nikizitumi?
Asalam aleykum
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia Alhidaaya.com kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn
Wanaoishi nchi za Kimagharibi ndio aghlabu watakuwa wanapambana na matatizo haya yenye mashaka ya vitu vya haraam katika vyakula au madawa.
Hebu tujue kwanza nini Gelatin na inatokana na nini?
Gelatin ni protini iliyokuwa kama jeli inayotokana na ima ngozi ya nguruwe, mifupa ya ng'ombe, ngozi ya ndama au ngozi ya samaki.
Hivyo lipasalo kwanza kutambua ni: Je, gelatin hiyo iliyomo katika chakula au dawa inatokana na nguruwe au wanyama wa halali? Ikiwa inatokana na nguruwe bila ya shaka ni haraam.
Kisha ikiwa kutoka kwa wanyama wa halali, je hao wanyama wamechinjwa kama ipasavyo Shariy’ah ya Kiislamu? Ikiwa hawakuchinjwa kihalali basi pia haifai kutumia gelatin hiyo ila tu ikiwa itapitia mabadiliko kamili ya metamofosisi (metamorphosis) ndipo itakuwa halaal kutumia. Na ikiwa haikupitia mabadiliko hayo basi haifai kutumia kwa njia yoyote.
Hivyo inampasa Muislamu anapoiona gelatin imo katika chakula au dawa aulize kwanza katika hilo shirika lake. Aghlabu huwekwa namba za simu katika paketi au chupa. Na ikiwa atajibiwa kuwa hawawezi kutambua inatokana na nini au hawana hakika inatokana na mnyama gani basi itampasa aepukane nayo.
Tanbihi muhimu kuhusu madawa ya vitamini na khaswa yenye madini ya chuma (Iron) kwamba ichunguliwe kiambato (ingredient) inayoitwa 'magnesium stearate' kwani hiyo aghlabu huwa wanaitoa kutoka katika damu ya nguruwe.
Na Allaah Anajua zaidi