Wudhuu Unatenguka Akimgusa Mkewe?

 

SWALI:

Ninalo swali: nikiwa nimesha tawadha naweza kumgusa mume wangu/au mume kumugusa mke wake inateuwa uthu???? Naomba jibu

Asante

 


 

JIBU:

  بسم الله الرحمن الرحيم الحمد لله والصلاة والسلام على أشرف الأنبياء والمرسلين وعلى آله وصحبه أجمعين و بعد

Maulamaa wamekhitilafiana katika jambo hili kama kumgusa mke kunatengua wudhuu. Na rai iliyo sahihi kabisa ni kwamba wudhuu hautenguki kwa kumgusa mtu mkewe au mke kumgusa mumewe.

Na dalili ni kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ambaye alikuwa akiwabusu wake zake baada ya kutawadha na hakurudia kufanya wudhuu tena, kwani bila shaka hii ingelileta mashaka.

Vile vile wamesema maulamaa kwamba kumgusa huko sio tu baina ya mume na mke bali hata kugusana baina ya mwanamke na mwanamume wasiokuwa na uhusiano hakuvunji wudhuu kama kwenye kupeana pesa kwenye biashara au wanapopishana majiani au kupewa na kupokea kitu n.k.

Ulamaa wachache walioona kwamba kumgusa mwanamke wudhuu unatenguka, wamechukua kauli ya Allaah سبحانه وتعالى iliyotajwa katika aya zifuatazo:   

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تَقْرَبُواْ الصَّلاَةَ وَأَنتُمْ سُكَارَى حَتَّىَ تَعْلَمُواْ مَا تَقُولُونَ وَلاَ جُنُبًا إِلاَّ عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىَ تَغْتَسِلُواْ وَإِن كُنتُم مَّرْضَى أَوْ عَلَى سَفَرٍ أَوْ جَاء أَحَدٌ مِّنكُم مِّن الْغَآئِطِ أَوْ لاَمَسْتُمُ النِّسَاء فَلَمْ تَجِدُواْ مَاء فَتَيَمَّمُواْ صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُواْ بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ إِنَّ اللّهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا))

((Enyi mlioamini! Msikaribie Swalah, hali mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema, wala hali mna janaba - isipokuwa mmo safarini - mpaka mkoge. Na mkiwa wagonjwa, au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni, au mmewagusa wanawake - na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kughufiria)) [An-Nisaa:43]

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُواْ بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَينِ وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُواْ وَإِن كُنتُم مَّرْضَى أَوْ عَلَى سَفَرٍ أَوْ جَاء أَحَدٌ مَّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لاَمَسْتُمُ النِّسَاء فَلَمْ تَجِدُواْ مَاء فَتَيَمَّمُواْ صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُواْ بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ مَا يُرِيدُ اللّهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَكِن يُرِيدُ لِيُطَهَّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ))

 ((Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swalah basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali Anataka kukutakaseni na kutimiza neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru))  [Al-Maaidah:6]

Lakini kauli hizi wengi wa maulamaa wameona kwamba kugusa huku kulikotajwa kumekusudiwa ni kujamiiana na sio kumgusa tu mwanamke ngozi kwa ngozi. Na hivyo wametoa tena dalili kutokana na kauli ya Allaah سبحانه وتعالى aliposema Bibi Maryam عليها السلام mama yake 'Iysa عليه السلام baada ya kubashiriwa kuwa atapata mtoto wa miujiza yaani bila ya kuolewa:

((قَالَتْ أَنَّى يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ وَلَمْ أَكُ بَغِيًّ))ا

((Akasema: Nitampataje mwana hali mwanaadamu yeyote hajanigusa, wala mimi si kahaba?)) [Maryam: 20]

Kwa hiyo imedhihirika kuwa kuguswa huko Alivyokusudia Allaah سبحانه وتعالى ni kujimai (kitendo cha ndoa).

Wa Allaahu A'alam

 

 

Share