Anatokwa Na Upepo Wa Mbele Katika Swalaah Je Unabatilisha Wudhuu?
SWALI:
Assalaam Alaykum Wahmatullah Wabarakatuh ama baada ya maamkizi haya kwanza namshukuru Allah Azza wa Jalla kwa kuniwezesha kuwa hai leo hii na kuweza kuwasiliana nanyi.
Pili shukrani zangu ziende kwenu Alhidaaya kwa kutupa mafunzo yanayohusiana na dini yetu ya Kiislam na Inshaallah Mungu atawalipa malipo mema.
Swali langu ni kuwa ktk mambo yanayotengua udhu kutokwa na upepo sehemu za siri ni mojawapo, sasa hapo ningependa kutolewa utata je ni sehemu moja tu ya nyuma au zote mbili Maana mimi mwenzenu nina matatizo ya gesi niwapo ktk swala sana hutokwa na upepo sehemu ya mbele na hulazimika kukata swala kila baada ya rakaa moja na kwenda kutia udhu ni hivyo hivyo mpaka muda wa swala unakwisha ile swala husika sijaiswali je sheikh nifanyaje na wengine wanasema ukitoka upepo sehemu ya mbele haitengui udhu na wengine wanasema inatenguwa je nishike wapi naomba unitowe wasiwasi Alhidaaya ili angalau niwe na uhakika.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutokwa upepo sehemu ya mbele.
Kutokwa upepo wa mbele kwa wanawake ni jambo ambalo halitengui wudhuu wake. Hivyo ukitokwa na upepo sehemu za mbele basi hakuna tatizo na Swalah yako ni sahihi na huhitaji kwenda kuchukua wudhuu.
Na Allaah Anajua zaidi