Wudhuu Unavunika Ikiwa Hukujifunika Vizuri?

 

SWALI:

Assalamu Alaykum.

Swali langu.

unapotia udhu ukiwa umevaa Bukta au suruali kipande imekufika mapajani tu. Udhu unaingia

Na vile vile kama   uko tumbo wazi kitovu kinaonekana una hio suruali kipande tu. Udhu Unaingia.

Waasala Alaykum

 


 

   

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaana wa Ta'aala)  Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Kutokujifunika vizuri sio miongoni mwa vitu vinavyovunja wudhuu. Yafutayo ni mambo yanayovunja wudhuu na yasiyovunja:

Yanayovunja wudhuu:  

1-Kutokwa na mkojo, kinyesi  au hewa katika sehemu za siri kutokana na dalilikatika Qur-aan:

 ((أَوْ جَاء أَحَدٌ مَّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ))

((au mmoja wenu ametoka chooni)) [Al-Maaidah:6]

Vile vile Hadiyth:

         ((لا يقبل الله صلاة أحدكم إذا أحدث حتى يتوضأ )) البخاري   وسنن أبي داود  

((Allah Haikubali Swalah ya mmoja wenu akitokwa na haja hadi atawadhe)) [Al-Bukhaariy na Sunan Abu Daawuud]

 

2-Kutokwa na manii, madhii na wadii kutokana na dalili:

 ما رواه علي بن أبي طالب رضي الله عنه قال : كنت رجلا مذّاء فأمرت المقداد أن يسأل  رسول الله صلى الله عليه وسلم فسأله فقال : ((فيه الوضوء ")) متفق عليه  

Kutoka  kwa  'Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu 'anhu)   ambaye amesema: "Nilikuwa ni mtu niliyekuwa nikitokwa sana na maji ya urethra (madhii). Nikamuambia Miqdaad amuulize Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    kuhusu hilo. Akamuuliza na akasema : ((Inahiitajika kufanya wudhuu)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

3-Usingizi mnono.

 

كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَأْمُرُنَا إِذَا كُنَّا سَفَرًا أَنْ لا نَنْزِعَ خِفَافَنَا ثَلاثَةَ أَيَّامٍ وَلَيَالِيهِنَّ إِلا مِنْ جَنَابَةٍ  وَلَكِنْ مِنْ غَائِطٍ وَبَوْلٍ وَنَوْمٍ  -  

 رواه الترمذي   وحسنه الألباني -   فذكر النوم من نواقض الوضوء .

Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituamrisha tunapokuwa safarini, tusivuwe khufu (viatu vya ngozi) zetu kwa muda wa masiku matatu, isipokuwa katika hali ya janaabah, lakini sio katika hali ya kuwa na kinyesi au mkojo au kulala)) [At-Tirmidhiy na amesema Shaykh Al-Abaaniy ni Hadiyth hasan].

Kwa hiyo Hadiyth hiyo inaonyesha kwamba usingizi ni mojawapo ya yanayovunja wudhuu.

 

4-Kupotewa na akili kwa sababu yoyote.

5-Kugusa sehemu za siri bila ya kukamatia kitu kwa  dalili ya Hadiyth ifuatayo:

           

بسرة بنت صفوان أنها سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم  يقول : (( من مسّ ذكره فليتوضأ ))

 رواه أبو داود  قال الألباني في صحيح سنن أبي داود صحيح   

Busra bin Swafwaan kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Atakayeshika utupu wake atawadhe)) [Abu Daawuud na amesema Shaykh Al-Albaaniy katika Sahiyh Sunan Abu Daawuud, Sahiyh]  

 

Yasiyovunja wudhuu:

1-Kumgusa mwanamke kwa ngozi

   Tafadhali ingia katika kiungo kifuatacho kupata maelezo zaidi kuhusu hili:

Wudhuu Unatenguka Akimgusa Mkewe?

2- Kumwagikwa damu sehemu yoyote ya mwili isipokuwa damu ya hedhi au nifaas. Lakini kama kidonda, damu kutoka puani na kadhalika haivunji wudhu.

3-Kutapika ikiwa ni matapishi mengi au kidogo.

4-Unapokuwa na shaka ya kutokwa na kitu kama mkojo au hewa kutoka sehemu za siri baada ya kufanya wudhuu. Shaka hiyo ikiwa ni katika Swalah au nje ya Swalah. Lakini ukiwa una hakika kuwa umetokwa na kitu basi wudhuu utakuwa umevunjika.

ولذلك بوب البخاري رحمه الله بباب " لا يتوضأ من الشك حتى يستيقن " وجاء فيه حديث

عَبَّادِ بْنِ تَمِيمٍ عَنْ عَمِّهِ أَنَّهُ شَكَا إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الرَّجُلُ الَّذِي يُخَيَّلُ إِلَيْهِ أَنَّهُ يَجِدُ الشَّيْءَ

فِي الصَّلَاةِ  فَقَالَ : (( لا يَنْفَتِلْ أَوْ لا يَنْصَرِفْ حَتَّى يَسْمَعَ صَوْتًا أَوْ يَجِدَ رِيحًا ))"  الوضوء/134) ،

 فكل هذه الوساوس والتخيُّلات لا تنقض الوضوء

Al-Bukhaariy (Rahimahu Allah) ametenga mlango katika kitabu chake kauita 'Mtu asifanye wudhuu kwa ajili ya shaka hadi awe na uhakika'. Ametoa humo Hadiyth ya 'Abbaad bin Tamiym kutoka kwa ami yake kwamba, mtu alilalamika kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alidhania kwamba amehisi kitu kimemtoka wakati wa kuswali. Akasema: ((Usiache kuswali) ila kama umesikia sauti au harufu))

        Wasi wasi na dhana kama hizi hazivunji wudhuu. 

        5-Kucheka kwa nguvu akiwa katika Swalah haivunjui wudhuu bali inavunja  Swalah.

6-Kuosha maiti hakuhitaji kufanya wudhuu ila inapendekezeka tu pamoja na kukoga josho (ghuslu)

 

Na Allaah Anajua Zaidi

Share