Kujishika Sehemu Za Siri Baada Ya Kutia Wudhuu Katika Ghuslu (Josho)

 

SWALI:

 

Naomba kuuliza hivi:  Nimesoma kuwa unapojitoharisha hedhi au janaba, unatakiwa kwanza ufanye udhu. Sasa ukishatia udhuu halafu tena ukawa unaoga na unajisafisha kwa sabuni mwili wako, kisha ukashika sehemu za siri kwa ajili ya kujisafisha, je inakuwaje josho lako? Je inabidi utie tena udhuu au unatosha ule ule wa mwanzo?  Na je nikitia udhuu mwishoni baada ya kufanya ghuslu haifai maana sikiniaiki nikijishika sehemu za siri nahisi kama udhu umeshatoka.

  


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako kuhusu kushika sehemu za siri wakati wa kufanya ghusl na hukmu yake.

 

Josho la janaba lina mfumo wake ambao tumefundishwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo kutufanya nasi tuwe ni wenye kufuata mfumo huo kisawasawa.

 

Katika mafunzo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuoga janaba, ni kuanza na viganja vya mikono na kuosha maeneo yote ya sehemu za siri na kisha ukachukua wudhuu na baada ya hapo ukajimwagia maji kichwani mara tatu na kuanza sehemu za kuliani na kisha za kushotoni hadi mwisho ukamalizia na kutawadha miguu yako.

 

Kugusa sehemu za siri bila matamanio ni jambo walilotofautiana Ma'ulamaa. Kuna wanaoona ni kutengua wudhuu japo mtu amejigusa bila matamanio. Na kuna wengine wanaona maadam hujajigusa kwa matamanio basi wudhuu wako uko palepale na hakuna haja ya kutawadha tena.

 

Kwa upande wako, ikiwa utakuwa umeshika sehemu zako za siri kwa bahati mbaya basi si lazima uchukue tena wudhuu ila ikiwa nafsi yako wewe ina wasiwasi, basi hapo unaweza kuchukua wudhuu upya kufuata lisilo shaka kwa kuacha lenye shaka kwako.

 

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo na manufaa zaidi:

 

027 Yanayotengua Wudhuu - 2

 

028 Yanayotengua Wudhuu - 3

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share