Inafaa Kujimai Na Mke Baada Hedhi Lakini Kabla Ya Ghuslu?

 

 

Je, Inafaa Kujimai Na Mke Baada Hedhi Lakini Kabla Ya Ghuslu?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalaam aleykum

Je kuna makatazo yoyote ya kumuingilia mkeo baada ya kumaliza hedhi kabla hajaoga josho, hali yuko msafi ?

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

 

Kuna ikhtilaaf za ‘Ulamaa kuhusu jambo hili. Kuna waliosema kuwa haimpasi mume kumuingilia mkewe akimaliza hedhi hadi afanye ghuslu nao wamechukua kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾ 

Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara; basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike. Watakapotwaharika basi waendeeni kupitia pale Alipokuamrisheni Allaah.”  Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha  [Al-Baqarah: 222]

 

    

Hivyo wameona kuwa kujimai baada ya mwanamke kumaliza hedhi kabla ya  kufanya ghuslu ni dhambi na itabidi kuomba maghfirah na tawbah. 

 

Kuna ‘Ulamaa walioona kwamba inafaa kujimai baada ya mwanamke atakapokuwa amesafika kutokana na damu ya hedhi yote na kumwagika kwake kumesimama kabisa, hapo anaruhusiwa kurudia kitendo cha jimai baada ya: (1) kuosha sehemu inayotoka damu, (2) au kufanya wudhuu au (3)  akakoga josho kamili (Ghuslu). Yoyote kati ya haya matatu atakayofanya itaruhusiwa kwao kurudia kitendo cha jimai kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾ 

Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara; basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike. Watakapotwaharika basi waendeeni kupitia pale Alipokuamrisheni Allaah.”  Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha  [Al-Baqarah 2:222]

 

Huo ni msimamo wa Ibn Haazim, 'Atwaa, Qataadah, Al-Awzaa'iy na Daawuwd Az-Zaahiriyy na wa Mujaahid kama alivyosema Ibn Haazim, "Zote tatu hizi ni Twahara, kwa hiyo, iwapo mwanamke atafanya moja ya njia hizo zilizotajwa, basi atakuwa ni halaal kwa mumewe"

 

Kauli hiyo hiyo inatumika kumaanisha kuwa ni kuosha sehemu ya siri katika Aayah iliyoteremshwa kuhusu watu wa Qubaa:

 

  ۚ فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا ۚ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ﴿١٠٨﴾

Humo mna watu wanaopenda kujitwaharisha. Na Allaah Anapenda wanaojitwaharisha.  [At-Tawbah 9:108]

 

 

Na wameona kwamba hakuna popote ima kwenye Aayah au Sunnah panaposhurutisha mojawapo kati ya maana tatu hizo zilizotajwa. Na kwa hali hiyo, panabaki kufanya moja ya aina hizo kuwa ni rukhsa ingawa kufanya Ghuslu baada ya mwanamke kumaliza hedhi yake na kabla ya kujimai ndiyo bora zaidi.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:

 

Mwanamke Anapomaliza Hedhi Anaweza Kufanya Wudhuu Pekee Kisha Afanye Jimai Na Mumewe Kabla Ya Kuoga Ghuslu?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share