Mjane Anaweza Kwenda Kwa Jamaa Zake Apate Kuhudumiwa? Uzushi Kuhusu Malaika Kumpelekea Habari Mume

 

Mjane Anaweza Kwenda Kwa Jamaa Zake Apate Kuhudumiwa? Uzushi Kuhusu Malaika Kumpelekea Habari Mume

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

SWALI

 

Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh

 

Sheikh, Naomba kuuliza masuala haya yafuatayo yanayohusiana na Eda ya kufiwa na mume:

 

-Je inaruhusika kwa mwenye kukaa eda kuonana na mwanamme ambaye si mahrim wake ikiwa atatimiza hijabu yake vizuri?

 

-Kwa upana gani sheria imempa fursa ya kutoka mwenye kukaa eda ikiwa

hakuna mtu wa kumuhudumia?

 

-Mwenye kukaa Eda haruhusiki kutumia manukato,Vipi kuhusu sabuni za

kukogea ambazo zinaharufu? 

 

-Ikiwa mwenye kukaa Eda yuko mbali na nchi yake mfano yuko Uingereza nayeanauraia wa huko,Je inaruhusika kukaa pekee yake huko wakati ipo njia yakurudi kwa ndugu zake au kwao yaani vipi ni bora kisheria kukaa huko huko kwa vile serikali inamgharimia mahitajio yake au arudi nchi yake au kwa jamaa zake?

 

-Ni kweli kwamba Mwenye kukaa Eda hujiwa na Malaika na kumuangalia,ikiwa kakaa kama sheria inavyotaka Malaika wanampeleka habari mumewake.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Tutakujibu maswali yako kwa mpangilio wa nukta kama ifuatavyo:

 

1-  Kuonana Na Mwanamume Asiye Mahram. 

Mwanamke aliyefiwa na mumewe haimpasi kisheria kuonana na mwanamume yeyote asiye Mahram wake akiwa katika Eda. Hii kutokana na hikma Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ambazo ni kujihifadhi mwanamke na kuhakikisha kwamba hakutatokea fitna yoyote.

 

2-  Mwanamke Kutoka Nje Ikiwa Hana Mtu Wa Kumhudumia

 

Mwanamke aliyefiwa na mumewe akiwa na dhurufu ya kutoka nje kwa vile hana mtu wa kumhudumia, basi hakuna ubaya kufanya hivyo ila tu lazima atimize masharti ya Eda ambayo yamo katika makala tunayokuwekea kiungo chini. Mfano kama yeye ndiye mwenye kufanya kazi na kuingiza masarufu ya nyumba na pindi asipokwenda kazini atakosa kuwalisha watoto wake na mwenyewe basi anaruhusiwa kwenda kazini ikiwa atafuata sheria za Eda. Kadhalika anaruhusiwa kutoka kwa kufuata mahitaji ya nyumbani kwake kama chakula n.k.

 

3- Kusafiri Kwa Jamaa Ili Upate Kuhudumiwa

 

Inapendekezeka mwanamke abakie nyumbani kwake hadi amalize Eda yake. Lakini ikibidi katika hali kama hiyo kwamba huna mtu wa kukuhudumia, au uko pekee yako huna watu wa kukusaidia, basi itakuwa ni hali ya dharura na utaweza kusafiri kwenda kwa jamaa zako.  

 

Itambulike kwamba hikma ya kukaa Eda ni kumpatia mwanamke fursa ya kujikurubisha kwa Rabb wake, kukumbuka mauti, kudhihirisha heshima kwa maiti wake, kumkumbuka sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Qur-aan, Swaalah za Sunnah za ziaida, na kila aina ya Adkhaar ili impatie utulivu wa moyo na aweze kukinaika na Qadhwaa na Qadr ya Rabb wake na huzuni iwe khafifu kwake. Hivyo ikiwa kwenda kwako nyumbani kutakukosesha haya, kwa kuwa utakuwa kutwa kucha na mazungumzo pamoja na jamaa bila ya kuwa na muda wa kufanya hayo,  itakuwa hukupata manufaa. Kwa hiyo ni kupima mwenyewe lililo busara na manufaa, na la sahali kwako. Lakini kwa hali uliyoieleza hapo juu, basi ni bora kubaki ulipo.

 

4- Malaika Kumpelekea Habari Mume Pindi Mwanamke Akikaa Katika Eda Ipasavyo

Hakuna dalili ya jambo hili. Na madamu hakuna dalili inabakia kuwa ni jambo la kuzushwa na sio la kweli.

 

 

Nukta nyinginezo zote utazipata katika maelezo marefu yaliyomo katika makala ifuatayo:

 

EDA - Hikma Yake, Hukmu Zake, Yanayopasa Na Yasiyopasa

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share