Kuvaa Mkufu Miguuni Inafaa?
Kuvaa Mkufu Miguuni Inafaa?
SWALI:
Asalam Alaykum,
Mie nilikuwa napenda kuuliza hivi jee inafaa kwa mwanamke kuvaa mkufu wa dhahabu au fedha ktk mguu wake kwa ajili ya mume wake?
In shaa Allaah
Naomba jawabu,jazakallahul kheir.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakuna ubaya kwa mwanamke kuvaa mkufu miguuni ikiwa ni kwa ajili ya kujipamba kwa mumewe. Na wala asidhihirishe mapambo hayo nje kwa wasiomhusu, yaani wasio maharimu zake. Dalili tunapata katika Aayah ya hijaab inayomalizia kukataza wanawake wanaovaa mikufu miguuni mwao wasitembee kwa kupiga miguu yao hadi ijulikane kuwa wamevaa mapambo hayo miguuni mwao:
وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ
Wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha.. [An-Nuwr: 31]
Hii ni wazi pia kuwa hijaab ya sheria inampasa mwanamke ajifunike hadi miguuni mwake. Tunaona dada zetu wengi wanajifunika tokea juu lakini miguu yao iko wazi hata katika Swalah utawaona wanaswali na miguu, vidole vya miguu vinaonekana. Swaalah zao hawa zinakuwa hazikukamilika kwani mwanamke anatakiwa ajifunike kote isipokuwa uso tu na viganja vya mikono.
Na Allaah Anajua zaidi