Kuvaa Niqaab Ni Fardhi? Nini Hukmu Ya Mwanamke Kuvaa Suruwali?
Kuvaa Niqaab Ni Fardhi? Nini Hukmu Ya Mwanamke Kuvaa Suruwali?
Swali:
Assalm aleikum warahmatullahi wabarakatu.
In shaa Allaah Allaah atuongoze sote waisilamu tuwe wenye kuongoka. Swali langu ni kuhusu hijab ya mwanamke. Nimefanya utafiti sana kuhusu jambo hili na wengine wanasema kuwa uso wa mwanamke sio awra wengine wanasema ni awra. Na pande zote mbili wanatoa evidence ya kusupport msimamo wao. Jambo hili limenitatiza sana naomba ufafanuzi zaidi. Pili je mwanamke kuvaa suruali ambayo haimbani, haionyeshi umbo lake wala sio ya kitambaa chepesi na juu ya suruali hiyo akavaa ngou au blauzi ya kufikia magotini inafaa?
Jibu:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Awali ya yote tungependa kuweka wazi masharti yanayohitajika kwa kivazi cha mwanamke wa Kiislamu. Nadhani kubainisha kwetu huko kutaondoa utata mwingi na kutuweka sawa katika baadhi ya nadharia. Masharti yenyewe ni kama yafuatayo kama yalivyodondolewa na wanazuoni wetu kutegemea Qur-aan na Sunnah ya Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nayo ni kama yafuatayo:
i) Kivazi ni lazima kisitiri mwili mzima. Wanazuoni wanatofautiana kuhusu uso na vitanga vya mikono. Kuhusu nukta hii Allaah Aliyetukuka Anasema:
وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾
Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 31.]
Na Amesema:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾
Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahzaab: 59].
Wanazuoni wameafikiana kuwa ni wajibu kwa mwanamke kusitiri mwili wake mzima, tofauti imepatikana katika kufunika au kutofunika uso na vitanga vya mikono.
ii) Vazi lisiwe lenyewe ni pambo: Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) pale Aliposema: "Wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika." [An-Nuwr: 31].
Hii kwa ujumla inachanganya nguo kwa dhahiri zikiwa na mapambo yenye kuvutia wanaume. Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Watu watatu hata usiwaulize (kwani wameangamia): Mtu aliyetengana na Jama‘ah na akamuasi kiongozi wake na akafa akiwa katika uasi; kijakazi au mtumwa aliyetoroka akaaga dunia; na mwanamke ambaye mumewe hayupo (mjini) lakini kamuachia mahitaji yake yote ya dunia, naye akawa anaonyesha mapambo baada yake. Hao usiwaulize kabisa" [Ahmad na al-Haakim].
Kusudio la amri ya kuvaa jilbaab (nguo pana yenye yenye kufunika kiwiliwili vizuri) ni stara kwa mwanamke, hivyo haiwezi kuingia akilini kuwa stara hiyo iwe tena ni mapambo na vivutio!
iii) Nguo iwe nene isiyoonyesha kilichopo chini yake: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Watu aina mbili ni wa motoni bado sijawaona: Watu wenye viboko kama mikia ya ng’ombe wanapigia nayo watu, na wanawake waliovaa lakini wapo uchi (wanaonyesha sehemu za miili yao ili kuonyesha uzuri wao au wanavaa nguo nyepesi inayoonyesha vilivyomo ndani yake) wanatembea kwa kuonyesha mapambo yao … Hawataingia Peponi wala hawatasikia harufu yake japokuwa harufu yake inasikika masafa kadhaa na kadhaa" [Muslim].
iv) Nguo iwe pana siyo inayobana hivyo kuonyesha maungo yake: Usaamah bin Zayd (Radhwiya Allaahu ‘Anhumaa) amesema: "Alinivisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Qubtwiyah (nguo kutoka Misri) aliyopewa hadiya na Dihyah al-Kalbiy (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), nami nikamvisha mke wangu. Akaniambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Una nini, mbona huvai Qubtwiyah?” Nikamwambia: “Ee Rasuli wa Allaah! Nimepatia mke wangu". Akaniambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Muamrishe ajaalie chini yake Ghulaalah (nguo ya ndani), kwani nahofia isije ikaonyesha kiasi cha mifupa yake" [Ahmad na Abu Daawuud]. Kwa dada zetu Waislamu! Haitoshi kusitiri nywele zenu na vifua vyenu kisha baada ya hapo mkawa mnavaa mavazi yanayobana na mafupi yenye kuonyesha miguu yenu.
v) Nguo zisitiwe manukato: Imepokewa na Abu Muusa al-Ash‘ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwanamke yeyote anayepaka manukato, kisha akawapita watu ili wapate harufu yake (ya manukato), ni mzinifu” [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy kwa Isnadi iliyo Hasan [nzuri]). Al-Haythamiy katika az-Zawaajir ametaja kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa kwa mwanamke kutoka nyumbani kwake akiwa amepaka manukato na amejipamba hata kama mumewe amempatia ruhusa.
vi) Isishabihiane (isifanane) na kivazi cha mwanamume: Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) amesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake na wanawake wanaojifananisha na wanaume" [Al-Bukhaariy, Abu Dawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].
Maana ya Hadiyth hii ni kuwa haifai kwa wanaume kujishabihisha na wanawake katika kivazi na mapambo ambayo ni hasa kwa wanaume na kinyume chake. Amesema Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu): “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanamume anayevaa nguo za kike na mwanamke anayevaa nguo za kiume” [Ahmad na Abu Daawuud kwa Isnadi iliyo sahihi].
vii) Isishabihiane na kivazi cha makafiri: Imekariri Shari‘ah kuwa haifai kwa Muislamu – wanaume kwa wanawake – kushabihiana na makafiri sawa katika ‘Ibaadah zao, ‘Iyd na sherehe zao au katika mavazi yao hasa. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona ‘Abdillaah bin ‘Amr (Radhwiya Allaahu ‘Anhumaa) akiwa amevaa nguo fulani, akamwambia: “Hakika hii ni nguo ya makafiri, hivyo usivae” [Ahmad, Muslim na an-Nasaa’iy].
viii) Isiwe ni kivazi cha fakhari (umaarufu na mitindo yenye kwenda na wakati): Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhuma) aliyesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote mwenye kuvaa nguo ya kutaka umaarufu hapa duniani, Allaah Atamvisha nguo ya udhalilifu Siku ya Qiyaama, kisha Ataiwashia moto” (Abu Daawuud na Ibn Maajah). Nguo ya kutaka umaarufu na kujionyesha ni kila kivazi kinachokusudia kutaka kujulikana na watu.
Tukirudia nukta ya kwanza kama tulivyotangulia kusema ni kuwa kuna tofauti baina ya wenye kuunga rai hizi mbili – kufunika uso na vitanga vya mikono au kutofunika, kila kimoja kina dalili zake kutoka kwa Qur-aan na Sunnah. Rai hizo mbili zina vigogo nyuma yake kama kwa muhtasari ufuatao:
- Uso na vitanga vya mikono ni lazima vifunikwe: Hii ni rai ya Ibn Mas‘uud (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), Imaam Ahmad na miongoni mwa wanazuoni wa zama zetu ni Ibn Baaz, Ibn ‘Uthaymin, na wengineo.
- Inafaa kutofunika uso na vitanga vya mikono: Hii ni rai ya Ibn ‘Abbaas, Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘Anhum), Imaam Maalik na ash-Shaafi‘iy na miongoni mwa wanazuoni wa zama zetu ni Imaam al-Albaaniy na wengineo.
Kwa maoni yetu tunaweza kuhitimisha mada hii kwa maneno mazuri yaliyoandikwa na wanazuoni wetu mashuhuri katika karne ya 14 na 15 Hijri. Mmoja wao ni Allaamah Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy katika kitabu chake Jilbaab al-Mar-at al-Muslimah amesema: “Mwanamke amepewa ruhusa kutofunika uso na vitanga vya mikono lakini akitaka mwenyewe kufunika (sehemu hizo mbili) hakatazwi na Shari‘ah”. La muhimu sana ni kuwa wafuasi wa makundi haya mawili yenye miono tofauti yasiwe ni yenye kuzozana wala kukufurishana wala kuwaona wengine wako katika makosa.
Na tunashauri kwa mwenye uwezo wa kuvaa Niqaab ikiwa haitamsobabishia matatizo na kunyanyaswa katika jamii anayoishi, basi ni bora zaidi kufanya hivyo kwani ndivyo walivyofanya wake za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Kwa maelezo zaidi ingia katika kiungo kifuatacho upate manufaa zaidi ya mas-ala haya:
Hijaab Ya Sheria Inahusu Kufunika Uso Na Miguu?
Ama kuhusu kuvaa suruali kwa mwanamke ni jambo ambalo litafahamika vyema ikiwa tumefahamu masharti ya kivazi cha Kiislamu tuliyoyaeleza hapo juu. Hakika ni kuwa ni suruali chache sana zinazovaliwa na wanawake ambazo hazibani wala kuwa na mapambo. Ni jambo linalojulikana kuwa washoni (fashion designers) wa nguo za kike ni wananume ambao haja na kusudio lao ni kutaka kuonyesha sehemu moja au nyengine nyeti ya mwanamke. Hivyo, uzuri wa suruali za wanawake ni zile zenye kubana na kuvutia zenye kuonyesha umbile lake. Hakuna katazo la kuvaa suruali ikiwa mshono wake ni tofauti na ule wa wanaume, na lau itakuwa kweli halibani, halionyeshi umbile lake wala kilichomo chini yake sharti tu juu yake uvae jilbaab kwani blauzi pekee haitoshi juu ya suruali au kuvaa koti refu. Kuvaa hijabu (Jilbaab) juu ya suruali hiyo ya kike ambayo ni pana na isiyoonyesha ndani, kutamsaidia kutoonekana uchi wake hasa anapopanda gari, kukimbia, kufanya mazoezi, na harakati zinginezo ambazo zinaweza kusababisha vazi la juu kunyanyuka au kupanda wakati wa harakati hizo.
Na Allaah Anajua zaidi