Hijaab Ya Shari'ah Inahusu Kufunika Uso Na Miguu?
Hijaab Ya Sharyi'ah Inahusu Kufunika Uso Na Miguu?
SWALI:
Naomba nifahamishwe hijabu ipasavyokuwa, je uchi wa wa mwanamke does it include miguu? since summer is nearing most of us are shoping for open shoes, is it allowed, I know other madh-habs say we should infact cover our whole faces but I don’t think the qur'an specifies that in particular?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kuhusu kufunika Miguu:
Naam miguu ya mwanamke inalazimu kufunikwa kwa dalili:
Imepokewa kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati lilipozungumzwa suala la kipimo cha nguo ya chini ya mwanamume (ambayo inatakiwa isivuke mafundo ya miguu): Ee Rasuli wa Allaah, na ipi hukumu ya kipimo cha nguo ya mwanamke? Akasema: "Ataiteremsha (kiasi cha) shubiri).” Akasema Ummu Salamah kwa maana hiyo si itaonekana (miguu yake)? Akasema: (Na aiteremshe) kiasi cha dhiraa moja wala asizidishe zaidi ya hapo." (Abuu Daawuwd: 4117 na Maalik katika Muwatwa: 2017).
Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyah (Rahimahu Allaah) amesema katika Majmuw’ Al-Fataawaa 22/110:
“…….Ni dhahiri kwamba rai ya Imaam Ahmad iko wazi kabisa kuwa kila kiungo cha mwanamke ni ‘awrah’ (uchi) hata pia kucha zake. Na hii pia ni rai ya Imaam Maalik.
Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ
Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao. [An-Nuwr: 31]
Imaam Ahmad amesema: “…. Mapambo ambayo yaliyodhihirika ni nguo ….. kila kiungo cha mwanamke ni ‘awrah’ hata kucha zake. Imesimuliwa katika Hadiyth “Mwanamke ni ‘Awrah”. Hii ni umbo lote la mwanamke. Na sio makruwh (haichukizi) kufunika mikono yake wakati wa kuswali, kwa hiyo pia ni sehemu ya ‘awrah kama ilivyo miguu. Hivyo Qiyaas imekusudiwa kwamba uso pia ni ‘awrah’ japokuwa haukutakiwa kufunikwa wakati wa Swalaah na sio kama mikono…” [Sharh Al-‘Umdah 4/267-268]
Dalili anayoichukulia Imaam Ahmad ni:
Imesimuliwa na ‘Abdullaah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwanamke ni ‘awrah’ na anapotoka nje basi matumaini ya shaytwaan huwa juu)) [At-Tirmidhiy, 1173 na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy 935]
Kuhusu kufunika uso:
Kuhusu kauli yako dada yetu kuwa Qur-aan haikutaja kuhusu kufunika uso, si sahihi kwa sababu imetajwa katika Suwrah Al-Ahzaab wanawake kujigubika jilbaab. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾
Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahzaab: 59]
Na kutokana na kauli iliyo sahihi kabisa ni kwamba jilbaab ni guo ambalo mwanamke anaivaa juu ya khimaar kutoka kichwani na inashuka kumfunika uso wake.
Ingawa ‘Ulamaa wamekhitilafiana katika swala hilo ila rai iliyo ya nguvu kabisa ni kujuzu kujifuniko uso. Na baadhi ya dalili ni kama ifuatavyo:
Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba ilipoteremeshwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ
Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao… [An-Nuwr: 31]
Wanawake wa Ki-Muhaajirina walichana na kukata gauni zao pembeni ili kufunikia nyuso zao )) [Al-Bukhaariy]
Na 'Aliy bin Abiy Twalhah amerepoti kwamba Ibn 'Abbaas amesema kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewaamrisha wanawake waumini wajifunike nyuso zao kutoka vichwani mwao wakiacha jicho moja tu, wanapotoka nje ya nyumba zao kwa ajili ya kutafuta mahitajio yao. [Tafsiyr Ibn Kathiyr: 8: 45].
Na dalili nyengine ni pindi mwanamke anayeingia katika ihraam amekatazwa kujifunika uso. Hii bila shaka ina maanisha kwamba mwanamke pindi akiwa hayuko katika ihraam, anapaswa kujifunika uso. Na pia dalili ni kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((لَا تَنْتَقِبُ الْمَرْأَةُ الْمُحْرِمَةُ وَلَا تَلْبَسُ الْقُفَّازَيْنِ))
((Mwanamke katika Ihraam asivae niqaab wala glavu)) [Al-Bukhaariy]
Na pia katika safari ya Hajj, 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: "Wapandaji (wanaume) walipita mbele yetu tukiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Walipokuwa sambamba mbele yetu tuliteremsha utaji (shungi) zetu usoni na vichwani mwetu, kisha walipotoweka tulijifunua)) [Abu Daawuwd na Ibn Maajah]
Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida zaidi:
Je, Inafaa Mume Kumlazimisha Mke Kuvaa Niqaab?
Mwanamke wa Kiislamu analazimika kuyafahamu masharti ya hijaab kama yafuatavyo:
1. Jilbaab liwe refu la kukufunika mwili mzima mpaka miguu, na kama halikufunika miguu basi mwanamke avae soksi.
2. Jilbaab liwe pana na sio lenye kuonyesha umbo, yaani lisiwe lenye kubana popote mwilini.
3. Jilbaab liwe zito na si jepesi la kuonyesha mwili.
4. Jilbaab lisiwe na marembo yoyote yale ya kuvutia.
5. Jilbaab halitakiwi lifanane na mavazi ya makafiri.
6. Jilbaab halitakiwi liwe ni katika mavazi ya fakhari.
7. Wanawake kutokuvaa nguo zinazofanana na nguo za kiume.
8. Kutotia manukato.
Na Allaah Anajua zaidi