Kuwa Na Rafiki Mwanamume Asiye Na Maadili Mazuri Ya Dini
Kuwa Na Rafiki Mwanamume Asiye Na Maadili Mazuri Ya Dini
Swali:
Ni msichana wa miaka 22 nasomea udaktari katika chuo kimoja hapa cha udakatri hapa Tanzania. muda wote nilikuwa sina uhusiano na rafiki wa kiume kwa sababu dini hairuhusu nikajitunza kwa muda wote ingawa vishawishi vilikuwa vingi na mazingira hayakuwa mazuri lakini alhamdulilah nimestirika, nilivyomaliza 4m 6 mwaka juzi nilikuwa nyumbani katika likizo fupi nikapata kazi stationary huko nikapata rafiki wa kiume. nilitokea kumpenda ghafla sikumchunguza tabia zake. By the tym nakuja kugundua hana vigezo ninavyovitaka ikawa too late kwani nilimpenda mno. Tabia zake hazikunipendeza ila nilitegemea kuwa nitambadilisha na atakuwa na hulka na tabia za kiislam kama ninavyaotaka, akanitolea barua lakini wazazi walichelewa kujibu barua eti wakitaka mimi nisome, ingawa nahisi there is somethng beyond ol ths hings. Baadae nikja kugundua kuwa alikuwa na msichana mwingine na siku alikuwa akinidanganya. Nikaamua kuachana nae ili wawe pamoja na huyo msichana, sababu kubwa ni kuwa hana vigezo vile ninavyovihitaji. sasa hivi ananiambia eti wameachana na yule msichana anataka tuwe pamoja. Lakini nafsi yangu haitaki kwasababu hana tabia na vigezo nivitakavyo.
Sasa ninachohofia je, nikiamua kutokuridiana nae baadae nitakosa mwingine, naogopa isije kuwa Allaah kapanga tuwe pamoja. plz nishauri juu ya hili.
Jibu:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika hii ni tahadhari kwa wasichana na dada zetu wasiwe ni wenye kudanganywa na wavulana ambao haja yao kubwa ni kuwaharibia maisha yao hapa duniani na Kesho Akhera. Mara nyingi roho zenu zinakuwa laini na hafifu kiasi ambacho kwamba haraka kumuamini mvulana ambaye atakudanganya na kukupa maneno mazuri ya kukupendezesha na kukusifu hadi ulainike na umuamini kisha ujikute umevaliwa na mapenzi naye na hata kujikuta umeanza kuingia katika maasi ya zinaa. Ukimsikia mvulana anakuanzia kwa sifa na maneno mazuri tahadhari naye na umkimbie mvulana huyo kama unavyomkimbia simba au nyoka. Mara nyingi utakuwa wewe si wa kwanza kusifiwa na kuambiwa hayo na mvulana huyo huyo … Tahadhari kabla ya athari kukufika. Tambua kuwa maji yakishamwagika hayazoleki tena.
Wasichana wengi wameingia katika mtego huu kisha ikawa vigumu kujiondolea janga hilo. Mara nyingi msichana anaachwa na mimba na huyo mvulana anamruka baina ya ardhi na mbingu.
Kitu kinachojitokeza ni kuwa huyo mvulana hana kigezo chochote cha mume wa Kiislamu – maadili yake ni mabaya (muongo). Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuleza kuwa Muislamu hawezi kuwa muongo. Nasiha yetu ambayo tunaweza kukupa ni kuwa usirudiane wala kuwasiliana naye tena au utajiingiza katika janga ambalo utajuta baadaye. Mawasiliano kawaida yanaleta maafa makubwa na maovu zaidi. Yale maasi mliyofanya kwa kuwa pamoja faragha hata kama haukufanya kitu au lolote yanatosha usizidishe maasiya mengine. Kwa ule urafiki mliofanya ambao umekatzwa na Uislamu unatosha. Lile lililobaki ni wewe kurudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) kwa kuomba msamaha na kuweka azma ya kutorudia tena katika maisha yako hapa duniani. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) kwa nia yako nzuri Akusaidie kuweza kutorudia hilo.
Dada yetu usitie hofu kabisa kuwa hutopata mume ukimkosa huyo. Kwa ajili ya kuacha kwako maasi ya urafiki na ambao umekatazwa na kurudi kwa Allaah. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) pale Aliposema:
“Wale kuwaweka wanawake kinyumba” [5: 5]
Urafiki huo ni chanzo cha kufikia hilo. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Akuepushie mbali na hilo. Yeye (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Atakupatia kheri iliyo kubwa zaidi, kwani ni Yeye Aliyetueleza:
وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ ۚ
Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza... [Atw-Twalaaq: 3].
Anasema tena Aliyetukuka:
وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾
Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni khayr kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216].
Hili la kumjua kuwa yeye ana mpenzi (msichana) kabla hamjaoana ni kheri kwako japokuwa unachukia. Hivyo, jaribu kumsahau kwa kumtoa mawazoni na akilini na kwa uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) utapata aliye bora na mwenye vigezo vya Dini na maadili mema. Insha’Allaah hutakosa mwengine, nasi tutakuwa pamoja nawe katika kukuombea kila la kheri.
Na Allaah Anajua zaidi.