Kutoa Nywele Za Uso Na Za Mwilini
Kutoa Nywele Za Uso Na Za Mwilini
Swali La Kwanza:
Asalam Alaykum,
Mie naomba kuliiza kusafisha uso au mwili ktk miguu, mikono ukatowa nywele (malaika) tunasema. hii inafaa au haifai
Swali La Pili:
Asalamu Aleikum
Naomba unifahamishe kwa vizuru ngugu yangu muislam. Jee mwana mke aruhusiwa kunyoa nyewele za mikona na miguu? Na nipe hukmu zake pamoja na kukata nyusi?
Jibu:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Ni hakika kuwa Uislamu unawaamuru wafuasi wake wawe ni wenye kuwa wasafi katika kila hali. Usafi na utohara ni miongoni mwa sifa za kipekee zinazopatikana kwa Uislamu. hata katika jangwa la Makkah wakati ambao kulikuwa na uhaba wa maji Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Alimuamuru kipenzi Chake kwa kumwambia:
وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ﴿٤﴾
Na nguo zako toharisha. [Al-Muddaththir: 4].
Kwa ajili ya hiyo ndio Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuamuru kuwa tuwe ni wenye kunyoa nywele za makapwa na za kinena. Hivyo, ikiwa nywele za mwilini zitakuwa ni zenye kuleta uchafu au vigumu kuweka usafi basi zinaweza kunyolewa bila ya tatizo lolote. Nywele ambazo mwanamme hafai kunyoa ni ndevu zake. Hizo zinafaa zifugwe na kukirimiwa kwa kutunzwa.
Ama swali la pili, kutoa nywele za mikono na miguu kwa mwanamke ni jambo linaruhusiwa. Tofauti imekuja katika kutoa nywele za uso kwa mwanamke.
Wanazuoni wa Hanbali wamesema: "Mwanamke ameruhusiwa kutoa nywele za uso, ikiwa kwa idhini ya mume kwani ni katika mapambo."
Imaam an-Nawawiy yeye amekataa hilo kwani kwake amechukulia kuwa kutoa nywele hizo ni sawa na kuchonga nyusi.
Abu Daawuwd yeye amesema kuwa kutoa nywele za uso hakuingii katika kukata nyusi.
Kule ambako kumekatazwa na Uislamu ni kuchonga nyusi, kwani wenye kufanya hivyo wamelaaniwa kwa kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema: “Wamelaaniwa wanawake wenye kutoa nyusi na mwenye kutolewa” [Abu Daawuud kwa Isnadi iliyo nzuri].
Naye atw-Twabariy ameeleza kuhusu mke wa Abu Ishaaq ya kuwa alikwenda kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha), naye alikuwa ni mwanamke kijana mwenye kupenda uzuri, akamuuliza: "Mwanamke anatoa nywele za usoni kwa ajili ya mumewe". ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) akajibu: “Jiondoshee yanayokukera kiasi unavyoweza” [Fat-hul Baariy].
Kwa hiyo, kunyoa nywele za mikono, miguu na uso inaruhusiwa lakini kuchonga nyusi au kupunguza ni haraam.
Na Allaah Anajua zaidi