039-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kukatazwa Kusoma Qur-aan Katika Sujuud, Kuirefusha, Na Fadhila Zake

 

KUKATAZWA KUSOMA QUR-AAN KATIKA SUJUUD

 

Alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)akikataza kusoma Qur-aan katika rukuu na sujuud, na alikuwa akiamrisha kujitahidi na kuleta kwa wingi du'aa humo kama ilivyoelezewa kabla katika rukuu. Pia alikuwa akisema: ((Mja huwa karibu zaidi na Mola wake anaposujudu, hivyo leteni kwa wingi du'aa [humo])).([1])

 

 

 

KUREFUSHA SUJUUD

 

Alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)akiirefusha sujuud yake kiasi cha kukaribiana na rukuu katika urefu, na mara nyingine aliifanya ndefu mno kwa kutokea jambo lisilotegemewa, kama alivyosimulia mmoja wa Maswahaba akisema:

 

Mjumbe wa Allaah Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alitutokea katika moja kati ya Swalah mbili za jioni (Adhuhuri na Alasiri) akiwa amembeba Hasan au Husayn. Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alitangulia mbele na akamuweka chini [karibu na mguu wake wa kulia], kisha akaleta Takbiyr ya Swalah, na kuanza kuswali, alisujudu –sajdah- kati ya sajdah za Swalah yake, sajdah aliyoirefusha akasema: Hivyo nikainua kichwa changu [baina ya watu] kumbe alikuweko mtoto juu ya mgongo wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) hali ya kuwa amesujudu. (Kisha) nikarudi katika sajdah yangu [hii]. Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alipomaliza Swalah, watu wakasema: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Kwa hakika ulisujudu kati ya sajdah za Swalah yako, sajdah uliyoirefusha, mpaka tukadhania kuwa kuna jambo limetokea au ulikuwa unapokea wahyi". Akasema: ((Haikuwa lolote katika hayo, bali mwanangu alinipandia, nikachukia kumharakisha mpaka atapomaliza haja yake))([2]).

 

Katika Hadiyth nyingine, alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)akiswali, aliposujudu, Al-Hasan na Al-Husayn walimrukia mgongoni kwake. Watu walipojaribu kuwazuilia, aliwaashiria wawaachilie mbali. Alipomaliza Swalah, aliwaweka katika mapaja yake na akasema: ((Yeyote anayenipenda, basi na awapende na hawa wawili)).([3])

 

 

 

 

FADHILA ZA SUJUUD

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Hakuna yeyote katika Ummah wangu isipokuwa nitamtambua siku ya Qiyaamah)). Wakasema: "Vipi utawatambua ewe Mjumbe wa Allaah miongoni mwa umati mkubwa wa viumbe?" Akasema: ((Huoni kama ungeliingia katika boma ambako kuna farasi mweusi tii([4]) na farasi mwenye weupe katika kipaji chake na miguu([5]). Je, hutoweza kumtambua ni yupi baina yao?)). Wakasema: "Bila shaka". Akasema: ((Basi hakika Ummah wangu siku hiyo, watakuwa na weupe katika nyuso ([6]) kwa sababu ya sujuud, na wenye weupe katika mikono yao na miguu yao([7])  kwa sababu ya wudhuu)).([8])

 

Alikuwa akisema pia: ((Allaah Atakapotaka kumshushia Rahma Amtakaye katika watu wa motoni, Huwaamrisha Malaika wamtoe yeyote aliyekuwa akimuabudu Allaah, hivyo watawatoa, kwani wanawatambua kwa alama za sujuud. Kwa vile Allaah Ameuharamishia moto kuunguza alama za sujuud, hivyo watatoka kutoka motoni, kila binaadamu ataunguzwa na moto isipokuwa alama za sujuud)).([9]) 

 





[1] Muslim, Abu 'Awaanah na Al-Bayhaqiy. Imetolewa katika Al-Irwaa (456).

[2] An-Nasaaiy, Ibn 'Asaakir (4/257/1-2) na Al-Haakim ambaye amekiri kuwa ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali.

[3] Ibn Khuzaymah katika Swahiyh yake ikiwa na isnaad nzuri kutoka kwa Ibn Mas'uud (887) na Al-Bayhaqiy katika hali ya Mursal. Ibn Khuzaymah ameifasiri katika Mlango: "Dalili za kwamba kuashiria katika Swalah inavyofahamika katika Swalah haivunji wala kuharibu Swalah".  Hichi ni kitendo kilichoharamishwa na Ahlul-Ra-y (watu wa rai).  Hakuna Hadiyth katika Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo kuhusu jambo hili.

[4] Yaani rangi nyeusi safi isiyochanganywa na rangi nyingine yoyote. (An-Nihaayah)

[5] Weupe unakusudiwa sehemu ya farasi ambako minyororo na bangili zinavikwa pamoja na miguu ya chini lakini sio magoti.

[6] Yaani zinazong'ara usoni kutokana na nuru ya sujuud.

[7] Yaani sehemu zitakazong'ara kutokana na wudhuu: uso, mikono na miguu. Alama za kung'ara za wudhuu usoni, mikononi na miguuni za binaadamu kulinganisha na weupe wa uso farasi na miguu.

[8] Ahmad, ikiwa na isnaad Swahiyh. At-Tirmidhiy amesimulia baadhi yake na kakiri kuwa ni Swahiyh. Imetolewa katika Silsilatul-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah.

[9] Al-Bukhaariy na Muslim. Hadiyth inaonyesha kuwa wanaoswali lakini wana dhambi, hawatabakia motoni milele bali hata ambao wameacha Swalah kwa sababu ya uvivu hawatobakia motoni milele. Hii ni Swahiyh – taz. Asw-Swahiyhah (2054).

Share