040-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kusujudu Juu Ya Ardhi Na Juu Ya Jamvi, Vikao Vyake Na Utulivu Ndani Yake

 

KUSUJUDU JUU YA ARDHI NA JUU YA JAMVI ([1])

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم)   sana akisujuud juu ya ardhi (tupu).([2])

 

Na Maswahaba zake walikuwa wakiswali pamoja naye katika joto kali, hivyo anapokuwa mmoja wao hawezi kumakinisha kipaji chake ardhini, hutandaza nguo yake na kusujudia juu yake.([3])

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم)   akisema: ((…. Imejaaliwa ardhi yote kuwa ni (sehemu ya kuswalia) Msikiti – mtu anaweza kuswali popote juu ya ardhi inapomkutia Swalah kama hapana najsi - na twahara –inatwaharisha: kuitumia kwa kujitwahirisha kutayammam- kwangu na kwa Ummah wangu. Hivyo basi Swalah inapomkutia mtu yeyote katika Ummah wangu, huwa anao Msikiti (mahali pa kuswali) na anayo twahara, (Ilikuwa) kabla yangu wakidhania kuwa ni jambo kubwa, kwani hakika walikuwa wakiswali makanisani na kaika masinagogi yao)).([4])

 

Mara nyingine alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم)   akisujuud katika matope na maji. Na yalimtokea hayo katika asubuhi ya usiku wa ishirini na moja katika Ramadhaan, iliponyesha mvua, na paa la Msikiti lililojengwa na majani ya mtende liliezuliwa. Hivyo Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alisujuud katika matope na maji. Abu Sa'iyd Al-Khudriyy alisema: "Nimemuona kwa macho yangu, Mjumbe wa Allaah  (صلى الله عليه وآله وسلم)  akiwa na alama za matope na maji katika kipaji chake cha uso na pua".([5])

 

Pia mara nyingine alikuwa akiswali katika khumrah([6]),  au mara nyingine katika zulia/ jamvi([7]), na mara aliswali juu yake na ilikuwa ishageuka nyeusi kutokana na utumiaji wa muda mrefu.([8])  

 

 

 

 

KUINUKA KUTOKA KWENYE SUJUUD

 

Kisha, alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم)akiinua kichwa chake kutoka kwenye sujuud huku akileta Takbiyr([9]) na alimuamrisha aliyeswali vibaya kufanya hivyo kwa kusema: ((Swalah ya mtu haikamiliki hadi …. Asujuud, hadi mifupa yake itue, kisha aseme 'Allaahu Akbar', na anyanyue kichwa chake mpaka atulizane hali ya kuwa amekaa (sawa sawa)).([10]) Pia, mara nyingine, alikuwa akinyanyua mikono yake pamoja na Takbiyr hii.([11])

 

Kisha alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم) akiutandika mguu wake wa kushoto (ardhini) na kuukalia [hali ya kuwa ametulia]([12]), na alimuamrisha aliyeswali vibaya kwa kumwambia: ((Unaposujuud, jimakinishe kwa sujuud yako, na (kisha) unapoinuka, kalia paja lako la kushoto)).([13])

 

Alikuwa akiusimamisha mguu wake wa kulia([14]) na akielekeza vidole vya mguu wa kulia Qiblah.([15]) 

 

 

 

KIKAO BAINA YA SAJDAH MBILI (KIKAO CHA IFTIRAASH)([16])

 

Kisha alikuwa  (صلى الله عليه وآله وسلم) akiutandika mguu wake wa kushoto na kuukalia [hali ya kuwa ametulia]([17]), na alimuamrisha aliyeswali vibaya kwa kumwambia: ((Unaposujudu, jimakinishe kwa sujuud yako, na (kisha) unapoinuka, kalia paja lako la kushoto)).([18])

 

Alikuwa akiusimamisha mguu wake wa kulia juu([19]), na akielekeza vidole vya mguu wa kulia Qiblah. 

 

 

 

AL-IQ-AA'U (KUSIMAMISHA MIGUU HUKU UMEKALIA VISIGINO) BAINA YA SAJDAH MBILI

 

Alikuwa mara nyingine akifanya 'iq-aau' (kupumzika kwa kukalia visigino vyote viwili na vidole vyake [vyote].([20])

 

 

 

WAJIBU WA KUTULIA BAINA YA SAJDAH MBILI

 

Alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akitulia mpaka kila mfupa unarudi mahali pake sawa sawa.([21]) Na alimuamrisha aliyeswali vibaya hivyo kwa  kumuambia: ((Swalah ya mtu haitotimia hadi afanye hivyo)).([22])

 

Pia, alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) akikirefusha - hichi kikao baina ya Sajdah mbili- kiasi cha kukaribiana na urefu wa Sajdah yake([23]), na mara nyingine, alibakia katika (kikao hiki) mpaka mtu akasema: "Amesahau".([24])



[1] Al-Haswiyr – jamvi au mkeka uliotengenezwa kutokana na majani ya mtende au nyasi n.k.

[2] Hii ni kwa sababu Msikiti wake haukufunikwa na majamvi n.k. Hii ni dalili ya Hadiyth nyingi kama ifuatayo na ya Abu Sa'iyd itakayofuatia.

[3] Muslim na Abu 'Awaanah.

[4] Ahmad, Siraaj na Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh.

[5] Al-Bukhaariy na Muslim.

[6] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni. "Khumrah" ni kipande cha jamvi, makumbi ya mtende, au nyenzo kama hizo za miti ambazo ni kubwa kiasi cha mtu kuweka uso wake katika Sajdah. Istilahi hiyo haitumiki kwa vipande vikubwa.

[7] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni. 

[8] Muslim na Abu 'Awaanah. Al-labisa kawaida ina maana 'kuvaa', lakini hapa imetumika kumaanisha 'kutumia', yaani kukalia n.k. Hivyo 'kuvaa' inajumuisha pia 'kuikalia'. Hii inaonyesha kwamba imekatazwa (haraam) kukalia hariri, kwa sababu ya kuharamishwa kuvaa kulikothibitishwa katika Swahiyh Al-Bukhaariy na Muslim na wengineo. Bali ni makatazo ya dhahiri kukalia hariri yamesimuliwa humo kwa hiyo asichanganywe mtu na kauli za Maulamaa wakubwa kuruhusu.

[9] Al-Bukhaariy na Muslim.

[10] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh, na Adh-Dhahabiy amekubali.

[11] Al-Bukhaariy katika Juzuu Raf' Al-Yadayn, Abu Daawuud ikiwa na isnaad Swahiyh, Muslim na Abu 'Awaanah. Imetolewa katika Al-Irwaa (316).

 

Kunyosha mikono hapa kwa kila Takbiyr imetajwa na Ahmad, kama ilivyo katika Al-Badaa'i ya Ibn Al-Qayyim (3/89). Athram (ibnul Athram) amenukuu kutoka kwake (Imaam Ahmad) alipoulizwa kuhusu kunyanyua mikono, alisema: "Kwa kila harakaat ya juu na chini". Athram kasema: "Nimemuona Abu 'Abdillaah (yaani Imaam Ahmad) akinyanyua mikono katika Swalah kwa kila harakaat ya chini au ya juu".

 

Hii pia ilikuwa ni rai ya Ibn Al-Mundhir na Abu 'Aliy wa Ash-Shaafi'iy, na pia rai ya Maalik na Ash-Shaafi'iy mwenyewe kama ilivyo katika Twarh At-Tathriyb. Kunyanyua mikono hapa pia kumesimuliwa kwa usahihi kutoka kwa Anas bin Maalik, Ibn 'Umar, Naafi', Atw-Twaawuus, Hasan al-Baswriy, Ibn Siyriin na Ayyuub As-Sikhtiyaaniy, katika Muswannaf Ibn Abi Shaybah (1/106) ikiwa na usimulizi Swahiyh kutoka kwao.

 

[12] Ahmad na Abu Daawuud ikiwa na isnaad nzuri.

[13] Al-Bukhaariy na Al-Bayhaqiy.

[14] An-Nasaaiy ikiwa na isnaad Swahiyh. 

[15] Muslim, Abu 'Awaanah, Abu Shaykh katika (Aliyopokea Abuz-Zubayr kutoka katika njia isiyo ya Jaabir) (Namba 104-6) na Al-Bayhaqiy.

[16] Ni kukalia tumbo la mguu wa kushoto na kuusimamisha unyayo wa mguu wa kulia.

[17] Ahmad na Abu Daawuud ikiwa na isnaad nzuri.

[18] Al-Bukhaariy na Al-Bayhaqiy.

[19] An-Nasaaiy ikiwa na isnaad Swahiyh. 

[20] Muslim, Abu 'Awaanah, Abu Shaykh katika (Aliyopokea Abuz-Zubayr kutoka katika njia isiyo ya Jaabir) (Namba 104-6) na Al-Bayhaqiy.

Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni.  Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesahau katika hili, hivyo baada ya kutaja "Iftiraash" ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) baina ya Sajdah mbili, amesema: "Hakuna aina nyingine ya kikao cha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kilichohifadhiwa isipokuwa hiki". Vipi hii iwe sahihi na hali 'iq-'aau' imetufikia kutoka Hadiyth ya Ibn 'Abbaas katika Muslim, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy ambaye amekiri ni Swahiyh na wengineo. (Taz. Silisilatul-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah 383), Hadiyth ya Ibn 'Umar ikiwa na isnaad nzuri kutoka kwa Al-Bayhaqiy na Ibn Hajar amekiri ni Swahiyh. Pia Abu Is-haaq Al-Harbiy amesimulia katika Ghariby al-Hadiyth (5/12/1) kutoka kwa Atw-Twaawuus, aliyemuona Ibn 'Umar na Ibn 'Abbaas wakifanya 'iq-'aa', sanad yake ni Swahiyh. Allaah Amteremshie Rahma Zake Imaam Maalik ambaye amesema: "Kila mmoja wetu anaweza kukosea na kukosolewa isipokuwa mwenye kaburi hili". Aliashiria kaburi la Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Sunnah hii imetekelezwa na Maswahaba mbali mbali, Salafus Swaalih na wengineo na nimeipambanua katika Al-Aswl.

 

Bila shaka, 'iq-'aa' hii ni tofauti na ile iliyokatazwa kama itakavyofuatia katika  Tashahhud.

 

[21] Abu Daawuud na Al-Bayhaqiy ikiwa na isnaad Swahiyh.    

[22] Abu Daawuud na Al-Haakim ambaye amekiri ni Swahiyh na Adh-Dhahabiy amekubali.

[23] Al-Bukhaariy na Muslim.

[24] Kifungu kile kile kilichotajwa hapo mbeleni. Ibn Al-Qayyim amesema: "Sunnah hii imeachwa na watu baada ya zama za Maswahaba. Lakini anayefuata Sunnah na haangazi kwengine kunakoipinga, hana wasiwasi wa kupinga uongofu.

Share