Vidani Vya Fedha Vinafaa Kuvaliwa Na Wanaume Na Kuswali Navyo?

Vidani Vya Fedha Vinafaa Kuvaliwa Na Wanaume Na Kuswali Navyo?

 

 www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam aleykum,

 

Natumai hali zenu zote ni nzuri, nimefurahi sana waislam kupata website hii inayotupa mafunzo mbalimbali ya dini yetu. Swali langu ni kuhusu vidani vya madini ya silver ambavyo vijana wengi wa kiislam wanavivaa, je ni halali kuvaliwa? Na ikiwa kuruhusiwa kuswali navyo? Au kuna uzito Fulani (grams) ni ruhusa?

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Vidani aina yoyote ile kama ni dhahabu, fedha, shaba na kadhalika havifai kwa mwanamme kwani hayo ni mapambo kwa wanawake. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza pamoja na kuwalaani wanaume wote wanaojifananisha na wanawake na kinyume chake. Mbali na hivyo uvaaji wa vidani ni ‘amali ya makafiri ambao pia sheria imetutaka tuwe tofauti nao.

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake na wanawake wanaojifananisha na wanaume” [al-Bukhaariy, Abuu Daawuwd, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

Hivyo, ni vyema kabisa kwa Muislamu mwanamme aachane na kuvaa vidani. Kwa hiyo, haifai kuvivaa katika Swalaah au wakati mwingine wowote.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share