Zingatio: Muinamishie Mama Bawa La Huruma Maisha Yako Yote (Mother’s Day, Ni Nini?)
Zingatio: Muinamishie Mama Bawa La Huruma
Maisha Yako Yote (Mother’s Day, Ni Nini?)
Naaswir Haamid
Uislamu umemfadhilisha Mama juu ya jamaa yeyote ndani ya familia. Ni bora kuliko baba, mke/mume, mtoto na wengineo. Naye ahitaji kuinamishiwa bawa la rehma kipindi chote cha uhai cha mwanawe. Na chini ya unyayo wake ndiko kwenye jannah.
Mama kwa maneno ya shukurani utakayompa, kwa matendo utakayomfanyia na ihsani yoyote utakayompatia haitafikia uzito wa malezi yake juu yako. Yeye ndiye aliyekuweka ndani ya tumbo lake kwa kipindi cha miezi tisa. Afya yake ikazoroteka na akala vyakula hata visivyoweza kuliwa na fakiri. Hayo hayajaishia hapo tu, akakushusha kutoka tumboni mwake na kukuleta ulimwenguni, akakufuta machozi yako wakati unapolia, akakosa usingizi wakati unapougua.
Bado Mama hakukuacha mkono na akakuenga ulipofikia baleghe, akakutaza usifuate vikundi viovu, na badala yake akakuhimiza ushikamane na yenye manufaa na wewe. Leo umekuwa mtu mzima, na umekuwa na familia yako, unamtembelea Mama na kumlaghai kwa zawadi siku moja katika mwaka?!!! Hakika kitu kinachoitwa Mother’s Day dharau na kashfa kwa Mama aliyekuzaa.
Kuwatii wazazi ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na hivyo kuwaasi ni kujikurubisha katika ghadhabu za Muumba:
وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ
Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni ihsaan wazazi wawili na jamaa wa karibu [Al-Nisaa: 36]
Pia kuna Hadiyth chungu nzima ambazo zinamtanguliza Mama kuliko Baba, na jambo hili halitaki majadiliano kwani Mama ndiye aliyechukua taabu zaidi katika kukuzaa mpaka ukapata akili ya kujua vitu mbali mbali.
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) amesema kwamba alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: "Ee Rasuli wa Allaah, nani mwenye haki zaidi mimi kumfanyia wema?" Akasema: ((Mama yako)). Akauliza: "Kisha nani?” Akasema: ((Mama yako)). Akauliza: "Kisha nani?" Akasema: (Mama yako) Akauliza: "Kisha nani?" Akasema: ((Kisha baba yako)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na miongoni mwa mambo ya uzushi yaliyozuka enzi hizi, ni kutenga siku maalumu kwa ajili ya kumkumbuka Mama. Hapana shaka yoyote mila hii imetokea Magharibi na ikasafirishwa kwa Waislamu. Katika siku hii, Mama mzazi hukaa kama opereta wa kupokea simu za wanawe wakimuuliza hali, wengine walete maua na zawadi za kila namna. Hio sio njia ya Uislamu kabisa kabisa, kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekukataza kumtupa Mama yako:
Kutoka kwa Al-Mughiyrab bin Shu'ubah amesema: Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika Rabb (Mtukufu) Amekuharamishieni kuwatupa Mama zenu.. )) [Imaam Ahmad].
Basi kwa hakika kumtii Mama na kumhurumia ni katika jambo la maumbile. Kama ambavyo Mama anavyokuwa na mapenzi kwa mwanawe, basi na mtoto anatakiwa kuwa na mapenzi kwa Mama yake. Si asili ya mapenzi kuoneshwa kwa siku moja na ukamtelekeza huyo unayempenda kwenye siku zengine.
Huyu ni Mama, iwapo utamtendea maasi, utambue utalipwa ama hapa duniani kwa kupatiwa kizazi kitakachokutovukia adabu, ama utalipwa katika Siku ya Hesabu. Na hakika kutenga siku moja tu ndani ya mwaka mzima kwa ajili ya kumkumbuka Mama ni uasi.
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atuongoze katika njia ya haki.