Ndoa Ya Mkeka Inajuzu Japo Watoto Wamezini Na Wamezaa Kisha Tunawaozesha?

SWALI:

 

Suali langu ni kama ifutavyo; 'Katika Jamii zetu Sasa hivi (siku hizi) tuna utaratibu wa kuwaozesha watoto wetu (Waume au wake) katika njia ya Kuwakamatia (Ndoa za Mkeka), na hii kwa kiasi kikubwa hutokezea wakati Watoto hawa Wameshazaa (kwa kuzini kabla ya kuoana) Jee Ndoa ya aina Hii ni halali (Inaswihi) na kama si halali au haswihi Baada ya watoto hawa kuthibitika kua wamezini na wamezaa, Jee kabla ya kuwaozesha tunatakiwa tuwanye kitu gani au kama hatutowaozesha tuwafanye nini juu yao? Ahsante sana. Wabillahi Tawfiiq


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa ya mkeka.

Kabla ya kuingilia kuwa ndoa hiyo inaswihi au la, inabidi labda tutazame ni kwanini watoto wazini kabla ya kushitukiziwa na kuozwa. Tunaona huenda sababu kubwa ikawa ni wazazi wenye kuweka vikwazo juu ya hilo pale kijana anapokuja kutaka kuposa akakataliwa na hivyo kuwafanya watoroshane na wakae katika hali ya kuzini hadi kuzaa watoto. Sababu nyingine inawezekana ikawa ni gharama ya ndoa zetu ambao imepanda kwa kiwango cha kushtusha. Inabidi wazazi wafanye mikakati ya kuona kwamba matatizo hayo yametatuliwa kwa njia nzuri kabisa. Na sababu nyingine ambayo ni kubwa, ni mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu kutokana na kukosekana kwa malezi bora ya Kiislamu katika nyumba nyingi za Waislamu.

 

Ama ndoa ya Kiislamu inaswihi ikiwa yatapatikana masharti yafuatayo:

 

1.     Idhini ya kijana anayeoa kuwa amekubali kwa ndoa hiyo kwa hiyari  yake. Na vile vile kukubali kwa msichana kuolewa.

2.     Kuwe na idhini ya walii (baba au mlezi) wa msichana kuhusu ndoa hiyo.

3.     Kuwe katika ndoa mashahidi wawili waadilifu.

4.     Kusomwe khutba ya kuozesha.

 

Na ikiwa kijana na msichana wamekaa pamoja na wakawa wamezini kwa muda mfupi au mrefu inabidi kuwe na sharti jingine la kuwetanganisha wawili hawa kwa muda ili kupata uhakika kama msichana ana mimba au la. Na katika kipindi hicho wanatakiwa vijana hao warudi kwa Allaah Aliyetukuka kwa kuomba msamaha, kujuta kwa waliyoyafanya, kutia azma ya kutorudia, kuacha maasiya haya na kufanya mema mengi.

 

Ikiwa hayo yatapatikana basi ndoa itaswihi. Hata hivyo, wanafaa wakumbushwe kuwa wale watoto waliozaliwa nje ya ndoa si watoto wa baba bali ni wa mama. Watoto hao hawawezi kurithiana na baba, ilhali wanaweza kurithiana na mama.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share