Nini Kifanyike Iwapo Mume Anaamua Kuongeza Mke Wa Pili na Mke Wa Kwanza Haridhii?
SWALI:
Assalam alaykum, natarajia unahali njema kwa baraka za allah karimu.
Ninahitajia mafundisho yatakayo nielimisha juu ya swali langu kwani ninahitaji kuelimishana na ndugu yangu ambaye amekutwa na mtihani wa mumewe kuoa mke wa pili bila kumjulisha na baadae kujua jambo hilo takribani miezi 7 hivi toka kutokea kwa jambo hilo na ndoa aliyofunga huyo mumewe kiasi sababu zake na maana halisi aliyomjulisha mkewe kuwa ni yenye kutatanisha na hivyo hivi yuko kwenye hali ngumu kifikra na ninaomba tumsaidie ufahamu na aweze kuishi maisha ya ndoa yake kwa wema na subra ktk kipindi hichi yeye akionacho ni kigumu na mtihani kwako.
Nitafurahi iwapo utanipatia maelezo haya na kwa lugha ya kingereza ili na mumewe apate kuyasoma na kuyaelewa sababu yeye hajui kiswahili,
nashukuru, inshaallah tutafanikiwa kuelimishana sote, amin.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kuoa mke wa pili bila kumjulisha mkewe wa kwanza. Hakika ni kuwa suala la uke wenza ni suala tatanishi kwa wasichana na wanawake wetu wa Kiislamu wanaoishi katika kila upande wa hii dunia.
Wanawake wetu ni kama kwamba hawajakubali rukhsa hii ya Allaah Aliyetukuka kwa namna moja au nyingine. Ni hakika isiyopingika kuwa haki ya kuoa mke zaidi ya mmoja amepewa mwanamme na Muumba wa mwanaadamu. Yeye (Allaah) Ndiye mwenye kujua katika maslahi ya mwanaadamu na amri Yake haitolewi na Yeye isipokuwa ni kumtakia kheri mwanaadamu huyo huyo. Huu kwa hakika si mtihani kabisa kwa dada yetu huyo bali yeye mwenyewe ndiye mwenye kujitia katika mtihani huo pasi na sababu yoyote ile.
Ingia katika kiungo kifautacho upate makala inayotaja Hikma Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuhusu wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja:
Na hayo maswali na majibu yam as-ala haya:
Hukmu Ya Mke Kuhama Nyumba Na Asiyemtii Mumewe Kwa Sababu Kaoa Mke Mwengine
Mwanamke Anayo Haki Kumzuia Mumewe Asioe Mke Zaidi Ya Mmoja?
Mume kuoa mke wa pili hahitaji idhini ya mkewe wa mwanzo japokuwa mume kumwambia mkewe ni katika ihsani na wema. Ingekuwa ni vyema kwa mume kumfahamisha mkewe kuhusu hilo. Sasa ikiwa mume ameoa bila kumjulisha mkewe wa kwanza inatakiwa mke asijitie katika huzuni wala babaiko ambalo halina maana yoyote bali ni dhiki na mashaka kwake. Mwanamke ambaye mumewe ameoa mke wa pili atajikuta katika furaha ikiwa atapuuza hilo la kuudhika na kusumbuliwa kwa kuwa na mwenzake wa kisheria. Asitilie maanani hilo bali anafaa yeye ajipendekeze kwa mumewe kwa kumfanyia yaliyo mazuri, kumwandalia, kumpatia utulivu, mapenzi na starehe. Akija mumewe nyumbani siku ya zamu yake ajitahidi awe ameiandaa nyumba na kumpambia mumewe kwa kiasi kikubwa sana.
Inaweza kuwa makosa anayofanya mke ndio yaliyompelekea mumewe aoe mke wa pili. Kwa hiyo, anatakiwa ajipinde sana katika kurekebisha kasoro zake ambazo anazo na awe na mahusiano mazuri na mema na mumewe. Kitu muhimu ni kwa dada yetu kuweza kupata haki zake zote kama mke, mfano malazi, mavazi, chakula, matibabu, kugawiwa siku yake na mambo yote ambayo anafaa afanyiwe.
Pia kujitoa katika dhiki na matatizo inabidi dada yetu huyo aongeze ‘Ibaadah, kusoma Qur-aan na du‘aa hasa katika nyakati ambazo du‘aa zinatakabaliwa na pia ajihimu katika kusubiri. Allaah Aliyetukuka Anasema:
“Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kuswali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu” (2: 45).
Ama ombi lako la kujibu swali lako kwa Kiingereza halina haja kwani mume hakuna sehemu anayohusika katika swali hili bali zaidi ni matatizo ya mke upande wa mume kumuolea. Kitu kinachotakiwa ni kuweza kukaa na dada yetu na kumfahamisha haya na kumuomba azidi uvumilivu kwani Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanatuarifu kuwa hakuna dhiki kwa dhiki kwani baada ya dhiki ni faraja.
Tunamtakia kila kheri na fanaka katika mambo yake dada yetu, na Allaah Ampe faraja na Amuondolee kila dhiki na balaa in shaa Allaah.
Na Allaah Anajua zaidi