Mke Kafiwa Na Mume Kabla Hajaingiliwa; Je, Atalipwa Mahari Yake Kamili Na Kukaa Eda Na Kurithi?
Mke Kafiwa Na Mume Kabla Hajaingiliwa;
Je, Atalipwa Mahari Yake Kamili Na Kukaa Eda Na Kurithi?
SWALI:
Mume ameoa Siku ya ijumaa,na akadhamiria kumfuata mkewe siku ya j/pili, ila kwa qadar za allaah yule mume akafariqi siku ya jumaa mosi na hali ya kua hajamaliza mahari,na hajamuingilia mkewe,je (1)mke huyo IPO haja amaliziwe mahari yake,au yeye ndie arejeshe mahari?
(2)je mke huyo atakaa EDA?na ni EDA gani?
(3)je mke huyo atarithi kwa marehemu?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tunashukuru kwa maswali yako mazuri.
Majibu tunayaweka kwa vipengele kama yalivyokuja maswali yake.
1. Mke atakamilishiwa mahari yake kamili.
Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliulizwa kuhusu mwanamme ambaye alimuoa mwanamke na hakutaja mahari yake au kumuingilia kabla ya kufa (mwanamme). Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) akajibu: "Anapaswa kupewa mahari yake kama wanawake mfano wake; si ziada wala pungufu, na vilevile anapaswa kukaa eda, na ana haki ya Miyraath.
Ma'quwl bin Sinaan Al-Ashja'iy (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisimama (baada ya kusikia hukmu (fatwa) ya suala hilo kutoka kwa Ibn Mas'uwd) na kusema: Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa hukmu kuhusiana na Birwa' bint Waashiq, mmoja katika wanawake wetu, na hiyo hukmu (fatwa) ilikuwa kama ambayo umeitoa wewe.
Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) alifurahi kwa habari (taarifa) hiyo (ya kufahamishwa kuwa hukmu yake imewafikiana na hukmu iliyowahi kutolewa na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
[At-Tirmidhiy, na amesema Shaykh Al-Albaaniy kuwa ni sahihi katika Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy]
2. Mke atakaa eda ya kufiwa sawa na mwanamke aliyeingiliwa.
Atakaa eda kama mwanamke yeyote mwengine aliyefiwa na mumewe; ikiwa hajaingiliwa au ameingiliwa kabla ya mume kufariki.
Na hiyo ni kwa ujumla wa maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyosema:
وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا ۖ ... ﴿٢٣٤﴾
Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na wakaacha wake, hao wake wangojee peke yao (eda) miezi minne na siku kumi...
[Al-Baqarah: 234].
Na dalili nyingine ni riwaaya ya Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) iliyotangulia hapo juu katika jibu namba 1.
Kwa faida ya nyongeza, ikiwa mwanamke alipewa talaka kabla hajaingiliwa na mumewe, basi huyo hatokaa eda kwa dalili ya maneno Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ ... ﴿٤٩﴾
Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu… [Al-Ahzaab: 49]
Hii ni dalili ya kuthibitisha kuwa mwanamke aliyepewa talaka bila kuingiliwa (bila kufanyika Jimaa') hatokaa eda kwa makubaliano ya Wanachuoni.
Ama mwanamke ambaye alikuwa kaishaingiliwa na mumewe kisha akapewa talaka, huyo atakaa eda kwa makubaliano ya Wanachuoni vilevile.
3. Mke atamrithi mume aliyefariki hata ikiwa hakuwahi kuingiliwa.
Rejea dalili juu kwenye jibu la swali namba 1.
Na kiwango cha Miyraath kinategemea na hali aliyokuwa nayo mume aliyefariki. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
... وَلَهُنَّ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْتُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّكُمْ وَلَدٌ ۚ فَإِن كَانَ لَكُمْ وَلَدٌ فَلَهُنَّ الثُّمُنُ مِمَّا تَرَكْتُم ۚ مِّن بَعْدِ وَصِيَّةٍ تُوصُونَ بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ ... ﴿١٢﴾
...Nao wake zenu watastahiki robo katika mlichoacha ikiwa hamna mtoto. Na ikiwa mna mtoto basi watastahiki thumni katika mlichoacha, baada ya kutoa wasia mliousia au kulipa deni...
[An-Nisaa: 12]
Na Allaah ni Mjuzi zaidi.