Anauza Pesa Za Kigeni, Kampa Mteja Bei Ya Jana Iliyokuwa Juu Badala Ya Ya Leo Ambayo Iko Chini Ili Apate Ziada Yeye

 SWALI:

 

Assallam Alaykum Warahmatullah Wabarakat, Ama baada ya salamu naomba kuuliza swali kama ifuatavyo, nafanya kazi katika duka la germstone siku hii ya leo kuna mteja amekuja kununua kitu nikabadilisha pesa kutoka kwa $dollar kwenda kwa Tshs sikuwa nimeangalia exchange rate nikawa nimetumia ile ya jana yake ambayo ilikuwa 1300 nikampigia kwa bei hiyo lakini kuja kuaangalia ilikuwa 1250. Sasa nauliza je nikipiga kwa bei hiyo halafu inayobaki nichukue inakua ni riba au rushwa tafadhali naomba kufahamishwa kwani katika hiyo pesa sijatumia hata shilingi moja mpaka nipate ufafanuzi.


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu kubadilisha pesa za kigeni.

 

 

Hakika hiyo haitakuwa ribaa wala rushwa kwani wewe ulipiga mahesabu kimakosa. Hata hivyo, baada ya kujua makosa yako inatakiwa uwe muadilifu na Uislamu ni uadilifu. Ukikosa kufanya uadilifu, utakuwa umeingia katika dhulma na udanganyifu. Na mambo yote hayo mawili ni madhambi makubwa kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Anayetudanganya si katika sisi” (Muslim) na “Ogopeni dhulma, kwani dhulma ni kiza Siku ya Qiyaamah” (Muslim).

 

Suluhisho kwa tatizo hilo ni kuwa muaminifu kwa kumpigia mteja huyo kama una namba yake. Ikiwa huna namba inabidi mwanzo uziweke usizitumie ukingojea huenda akarudi yule mtu kubadilisha pesa tena. Zikipitiwa na mwaka na hajatokea ndio unaweza kuzitumia. Pia unatakiwa uwaambie unaofanya kazi nao kwa kuwajulisha yaliyotokea na kuwa watamuona mtu huyo wampe salamu aje kuchukua amana yake.

 

Tunamuomba Allaah Akuzidishie Iymaan yako hiyo hadi kuja kuuliza hilo, inaonyesha jinsi gani ulivyo na khofu ya kutumbukia katika dhulma. Allaah Akuzidishie Iymaan na ucha Mungu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share