012-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kutoa Siri Ni Khiyana Ya Amana

 

KUTOA SIRI NI KHIYANA YA AMANA

 

Bila ya shaka kuwa mwanamke Muumini ndiye mtu wa karibu sana kwa mume wake, mwanamke huyu, anakuwa ndiye mwanamke aliyefanikiwa katika uhusiano wake wa mapenzi na mume wake. Mtu akiwa na siri kubwa ndani ya moyo wake, pindi anapoibeba siri ile peke yake huhisi kuwa kabeba kitu kizito sana moyoni mwake hadi atakapomuhadithia mtu mwengine ndipo atakapohisi kuwa amepumzika.

Hivyo basi, suala la kuhifadhi siri ni jambo zito kwa mtu na ni amana aliyoichukua. Imepokewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa ikiwa mtu atazungumza na mtu mwengine kisha wakaachana basi huwa ni amana (yaani mazungumzo yale waliyozungumza huwa ni amana kwa kila mmoja). Katika Hadiyth Mtume anasema,

“Hakika katika watu wabaya wenye shari siku ya Qiyaamah ni mtu aliyefanya tendo la ndoa na mke wake kisha mume au mke akatoa siri ile ya mume wake au ya mke wake”[1]

 

Jambo la kuhifadhi siri ni la wajibu kwa mume na mke na ni jambo lililokuwa muhimu sana katika jamii na ndilo linalohifadhi amani na maadili mema katika jamii husika. Kwa hakika kutoa siri za mwanamme ndani ya nyumba yake au mwanamke, matengamano ya mume kwa mkewe, watoto wake, na kila alichokuwa nacho katika mali yake na mengineyo itakuwa ni fedheha kwa watu wengi. Uislamu umemuusia Muislamu kumsitiri na kumfichia siri nduguye Muislamu, na ya kuwa, Muislamu atakayemsitiri nduguye Muislamu basi Mwenyezi Mungu Atamsitiri yeye siku ya Qiyaamah.

 

Pamoja na kuwa kuhifadhi siri kwa ujumla ni jambo muhimu sana na ni wajibu, hata hivyo kuhifadhi siri ya unyumba baina ya mume na mke ni jambo la wajibu zaidi na ni jambo tukufu ambalo halifai kutolewa kwa hali yoyote ile. Ama wajinga wa zama zetu leo hii hawapendezwi na maneno isipokuwa ni maneno haya na yote hayo yanatokana na ukosefu mkubwa walionao wa imani na udhaifu wao.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha hali hii ya kutoa siri ya jimai kwa watu, aliposema,

“Huenda mtu akasema anachomfanyia mke wake, na huenda hilo likafanywa na mwanamke pia (watu wakanyamaza baada ya maneno hayo) mwanamke akauliza[2], ee, kweli kabisa na wengi hufanya hivyo katika wanawake na wanaume, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, ‘Basi msifanye hivyo, mfano wa jambo hilo ni kama Shaytwaan aliyekutana na Shaytwaan mwenzake wa kike na akawa anamuingilia hapo njiani na watu wakiwa wanamwangalia”[3] 

 

 





[1] Imepokewa na Muslim

[2] Mwanamke huyu aliyeuliza jina lake ni, Asmaa bint Yaziyd, nae ndiye mpokezi wa Hadiyth hii.

[3] Imepokewa na Ahmad

Share