013-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Ni Wakati Gani Wivu Wako Kwa Mumeo Unakuwa Haufai?

 

NI WAKATI GANI WIVU WAKO KWA MUMEO UNAKUWA HAUFAI?

 

Katika hali ya kawaida kabisa wivu ni jambo linalokubalika, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Huona wivu, Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inasema,

“Kwa hakika Allaah Huona wivu, na Muumini huona wivu, ama wivu wa Allaah ni Muumini kufanya aliyoharamishiwa na Allaah”[1]

 

Na kama sio wivu tabia nzuri zote na stara katika maisha yangepotea, na mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ingekiukwa mbele za watu na katika masikio ya watu. Ama ghera ya mke kwa mume wake ni kule kufanya yaliyoharamishwa na Allaah, hii ni ghera inayokubaliwa kishari’ah na ni yenye kupendeza ama nyinginezo ni katika jumla za ghera zenye kukatazwa na haswa ikiwa hazina shaka na tatizo.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Katika ghera kuna ambazo Anazipenda Allaah, na zingine Anazichukia Allaah, ama ghera Anazozipenda Allaah ni zile ghera zilizojengwa kwa shaka. Ama ghera Anazozichukia ni zile ghera zisizokuwa katika shaka”[2]

 

Jambo la kusikitisha ni kuwa nyumba nyingi zimeangamia na kuanguka kwa sababu ya baadhi za ghera; nayo hutokana na dhana na shaka ambazo si za msingi kabisa, hufuatiwa baada ya dhana na wivu wa namna hiyo ni kujuta nayo ni katika kukhasirika. Asili ya ndoa ni kuwa mwanamke huchagua mwanamme mwema, mwenye kuaminika, kwa maana hiyo hakuna njia au nafasi ya kutia shaka au kumchunguza kila wakati na kumfuatilia kwa kila kitu kwa hoja ya wewe kuwa na wivu. Jihadhari usije ukaiangamiza nyumba yako kwa nafsi yako.

 

Hili ni kwa upande wako kama mke, ama kwa upande wa mume wako na ghera yake juu yako ni juu yake kutekeleza majukumu yako kwa ukamilifu na wakati huo hiyo ghera haitokuwa na nafasi tena.

 

Moja katika majukumu haya ni kujilazimisha kwako na stara, heshima na kulinda utu wako, kisha kutotoka nyumbani kwako bila idhini yake, kisha baada ya hapo, usikae hata mara moja na asiyekuwa maharimu wako. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth yake anasema,

“Jihadharini na kuingia kwa wanawake, Mtu mmoja akauliza ewe Mtume wa Allaah: Je, nikikaa pamoja na shemeji yangu au ndugu wa mume wangu? Mtume akasema, “Shemeji ni mauti.”[3]

 

 


[1] Imepokewa na Al-Bukhaariy

[2] Imepokewa na Ahmad na wengineo

[3] Al-Bukhaariy na Muslim - Mpitiaji

Share