014-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Mume Wangu Ni Bakhili...Nifanyeje?!!

 

MUME WANGU NI BAKHILI…NIFANYEJE?!!!

 

Baadhi ya wake hushitaki na kulalama kwa ubakhili wa waume zao juu yao, malalamiko haya mengi yake si ya kweli, kwani mke hutaka fedha kwa mumewe na ikikosekana kutokana na hali ngumu ya maisha aliyonayo mume basi mke atamtuhumu mumewe kwa ubakhili.

 

Hata hivyo ikiwa mume ni bakhili kweli kwa mke wake na kuto kumpa na kumhudumia mke wake kwa yale aliyoruzukiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa wakati huo mume yule huipelekea nyumba yake katika mawimbi na dhoruba, kwani mke kuhitaji mali humpelekea mwanamke yule katika hatari.

 

Tunamwambia mume huyu, je, hukusoma kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) akiwaelezea waja wake waumini?

“Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.” (25:67)

 

Kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu suala hili,

“Mwenyezi Mungu Atamuuliza kila mchunga kwa alichokichunga, je, amekiweka mahala pake na kuhifadhi au amepoteza, itafikia hadi mtu kuulizwa kuhusu watu wake wa nyumbani”[1]

 

Fahamu ewe mume mkarimu kuwa kutoa kwako kwa ajili ya mke wako na watu wa nyumbani kwako ni sadaka utakayolipwa na Mwenyezi Mungu, katika Hadiyth tukufu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

“Mtu atakapotoa kwa kuwapa watu wa nyumbani kwake akitaraji kulipwa na Allaah itakuwa ni sadaka aliyotoa (atalipwa kwa sadaka hiyo na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala))”[2]

 

Ni juu ya mke kuchunguza na kutafiti ni kwa nini mume wake anakuwa bakhili kwake, huenda akawa anafanya hivyo kutokana na kujua ufujaji wa mke wake, akipewa mali hufuja anachopewa, au huenda kuna sababu zingine binafsi azijuazo kutoka kwa mke wake. ikiwa ubakhili ni katika sifa ya mume wake, basi ni juu ya mke kusubiri na kutaka msaada wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kujaribu kwa wema kumfanya mume wake aache ubakhili na kumbadilisha kuwa ni mtu karimu mwenye kujitolea.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa ruhusa Hind bint ‘Utbah kuchukua mali kutoka kwa mume wake kiasi kinachotosheleza mahitaji yake na wala asizidishe.  Mtume alimwambia hayo kulingana na swali aliloulizwa na Hind,

“Ewe Mtume wa Allaah, kwa hakika Abu Sufyaan ni mtu bakhili hanipi cha kunitosheleza na mtoto wangu ila kile ninachokichukua kutoka kwake bila ya yeye mwenyewe kujua, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia, ‘Chukua kwa wema kile kinachokutosheleza wewe na mwanao’”[3]

 





[1] Imepokewa na Ibn Hibaan

[2] Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim

[3]Imepokewa na Al-Bukhaariy

 

Share