042-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Rakaa Ya Pili, Na Ulazima Wa Kusoma Al-Faatihah Katika Kila Rakaa
RAKAA YA PILI
Na alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم) anaposimama katika rakaa ya pili, bila ya kunyamaza, huanza kwa kusoma 'AlhamduliLlaahi [Al-Faatihah 1:1] (bila ya kupumzika).([1])
Na hufanya katika rakaa hii kama alivyofanya katika ya kwanza, isipokuwa alikuwa akiifanya fupi ukiilinganisha na ya kwanza
ULAZIMA WA KUSOMA SURATUL-FAATIHAH KATIKA KILA RAKAA
Alimuamrisha (صلى الله عليه وآله وسلم) aliyeswali vibaya kusoma al-Faatihah katika kila rakaa wakati alipomwambia baada ya kumuamrisha aisome hiyo al-Faatihah katika rakaa ya mwanzo([2]): ((…kisha fanya hivyo katika Swalah yako yote)).([3]) [katika usimulizi mwengine] ((...katika kila rakaa))([4]). Na alisema: ((katika kila rakaa kuna kisomo)).([5])
[1] Muslim na Abu 'Awaanah. Kipumziko kilichokanushwa katika Hadiyth hii inaweza kuwa ni kipumziko cha kusoma du'aa ya kufungulia na hakijumuishi kipumziko cha kusoma isti'aadhah, au inaweza kumaanisha zaidi ya hivyo. Naona kwamba uwezekano wa kwanza unakinaisha zaidi. Kuna rai mbili baina ya Maulamaa kuhusu isti'aadhah na tunachukulia iliyo sahihi ni kuisema katika kila rakaa. Maelezo yametolewa katika Al-Aswl.
[2] Abu Daawuud na Ahmad ikiwa na isnaad iliyo na nguvu.
[3] Al-Bukhaariy na Muslim.
[4] Ahmad ikiwa na isnaad nzuri.
[5] Ibn Maajah, Ibn Hibbaan katika Swahiyh yake na Ahmad katika Masaail ya Ibn Haani (1/52). Jaabir bin 'Abdillaah (رضي الله عنه) amesema: "Atakayeswali rakaa bila ya kusoma Mama wa Qur-aan hakuswali, isipokuwa akiwa nyuma ya Imaam". Imesimuliwa na Maalik katika Al-Muwatwtwa.