Tawassul Kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Inajuzu?

 

SWALI:

 

Assalam alaikum,

 

Hadithi ya wasila ni hii, kwa mujibu wa Sheikh Albany ni sahihi,

 

19 الترغيب في صلاة الحاجة ودعائها

681(1) (صحيح) عن عثمان بن حنيف رضي الله عنه أن أعمى أتى إلى رسول الله صلى الله عليه وسلم فقال يا رسول الله ادع الله أن يكشف لي عن بصري قال أو أدعك قال يا رسول الله إنه قد شق علي ذهاب بصري .قال فانطلق فتوضأ ثم صل ركعتين ثم قل اللهم إني أسألك وأتوجه إليك بنبيي محمد صلى الله عليه وسلم نبي الرحمة يا محمد إني أتوجه إلى ربي بك أن يكشف لي عن بصري اللهم شفعه في وشفعني في نفسي فرجع وقد كشف الله عن بصره رواه الترمذي وقال حديث حسن صحيح غريب. والنسائي واللفظ له وابن ماجه وابن خزيمة في صحيحه والحاكم وقال صحيح على شرط البخاري ومسلم وليس عند الترمذي ثم صل ركعتين إنما قال فأمره أن يتوضأ فيحسن وضوءه ثم يدعو بهذا الدعاء فذكره بنحوه ورواه في الدعوات.

 

 

ikiwa hii ni sahihi Je? Kutawassal kwa kusema kama alivyosema huyu mja alokuwa anaulemavu wa macho, kwamba "ewe Allah ninatawassal kwako kwa nabiy Muhammad Swalla llah alaihi wasallama........." kama hadithi inavyo jieleza (kwa kutumia maneno hayo hayo kwa kiarabu ama ukafasiri) itakuwa sio bid'aa.

 

 Wabillah taufiq

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

 

Mwanzo ni vyema tujue maana ya neno lenyewe kabla ya kuingia katika maelezo mengine. Al-Wasiylah, inatokana na Tawassul nayo ina maana ya anapofanya mwanadamu amali ya kujileta karibu na Allaah Aliyetukuka. Na al-Wasiylah ni matarajio na kutaka, na pia ina maana nyengine yenye mafungamano na asili, nayo ni cheo na daraja.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mnaposikia mwadhini semeni kama anavyosema, kisha mtaniswalia, kwani mwenye kuniswalia mara moja Allaah Humswalia kwayo mara kumi. Kisha muombeni Allaah Anipatie al-Wasiylah, kwani hicho ni cheo Peponi ambacho hakifikii ila mja miongoni mwa waja wa Allaah, na nadhani kuwa mimi ndiye mwenye cheo hicho …" (Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaaiy).

 

Ama ufahamu wa al-Wasiylah katika Qur-aan Tukufu haitoki nje ya hapo. Amesema Aliyetukuka:

"Hao wanaowaomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno – na wanataraji rehema Zake na wanaikhofu adhabu Yake. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi yafaa kutahadhari nayo" (al-Israa' [17]: 57).

Kuhusu Aayah hii, Imaam Ibn Kathiyr amesema yafuatayo katika Tafsiyr yake:

"Na kauli Yake Aliyetukuka: 'Hao wanaowaomba'. Amepokea al-Bukhaariy kutoka kwa Hadiyth ya Sulaymaan bin Mahraan al-A'mash kutoka kwa Ibraahiym kutoka kwa Abu Ma'mar kutoka kwa 'Abdullaah (Radhiya Allaahu 'anhu) katika kauli Yake: 'Hao wanaowaomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi'. Baadhi ya majini walikuwa wakiabudiwa, kisha wakasilimu'. Kulingana na riwaya nyingine: 'Baadhi ya wanaadamu walikuwa wakiwaabudu baadhi ya majini, baadaye hao majini wakasilimu, lakini wale wanaadamu walishikilia dini yao (ya kuwaabudu majini)'. Na kauli Yake Aliyetukuka: 'Na wanataraji rehema Zake na wanaikhofu adhabu Yake'. 'Ibaadah haitimii wala kukamilika ila kwa khofu na matarajio. Khofu humzuilia mtu kufanya yaliyokatazwa na matarajio humfanya afanye mambo ya utiifu (na mema)".

 

Hakika nasw za kisheria zinazo tilia mkazo wa Tawassul kutoka katika Qur-aan na Sunnah hazitoki katika vipengele vitatu. Navyo ni kama vifuatavyo:

 

1.  Kutawassal kwa Allaah Aliyetukuka kwa kutumia jina miongoni mwa majina Yake yaliyo mazuri au sifa miongoni mwa sifa Zake zilizo juu na tukufu. Mfano ni kama kauli: "Ewe Allaah! Hakika mimi nakuomba kwa kuwa wewe ni ar-Rahmaan, ar-Rahiym, al-Latwiyf, al-Khabiyr unipatie afya, siha na mambo yote mema". Allaah Aliyetukuka Amesema: "Na hakika Allaah ana majina mazuri, hivyo muombeni kupitia kwayo" (al-A'raaf [7]: 180). Na katika Sunnah ni kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika baadhi ya du'aa zake kabla ya salamu katika Swalah zake: "Allahumma bi-'ilmikal ghayb wa Qudratika 'alal khalq ahyiniy maa 'alimtal hayaat khayran liy wa tawaffaniy idhaa kaanatil wafaat khayran liy – Ee Allaah! Kwa elimu Yako ya ghaibu na uwezo Wako juu ya viumbe nihuishe ukiona uhai ni bora kwangu na unifishe ikiwa kufa ni bora kwangu" (Ahmad, an-Nasaa'iy, Ibn Hibbaan. Imesahihishwa na al-Haakim na kukubaliana naye adh-Dhahabiy).

 

 

2.  Mwanaadamu kutawassal kwa 'amali zake njema kama kusema Muislamu: "Allahumma As-aluka Bi-iymaaniy bi-Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) an tufarrija 'anniy – Ee Allaah! Nakuomba kwa Imani yangu kwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) unifariji mimi". Na hii si tawasuli kwa waliokufa bali kwa 'amali, nayo ni ile imani yako barabara kwa Mtume wa mwisho, Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Anasema: "Wale ambao kwamba wanasema: Ee Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumeamini, hivyo tusamehe madhambi yetu na utuepushe na adhabu ya Moto" (aal-'Imraan [3]: 16). Na ama katika Sunnah ni kile kisa cha watu watatu waliofungiwa na jabali pangoni, hivyo kushindwa kutoka kama kilivyopokewa na al-Bukhaariy na Muslim (pia tazama Riyaadhw asw-Swaalihiyn, Hadiyth namba 12, mlango wa kwanza wa Niyah).

 

3.  Kutawassal kwa du'aa ya mtu mwema aliye hai. Kwa mfano, Muislamu anapopatwa na tatizo na akaenda kwa mtu anayeitakidi kuwa ni mcha Mngu amuombee kwa Mola wake Mlezi ili Amfariji katika shida zake. Na kuhusu kipengele hichi zipo dalili nyingi. Miongoni mwazo ni yule Bedui aliyemtaka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye yupo juu ya Minbar amuombe Mola wake ili awapatie mvua (al-Bukhaariy na Muslim). Na katika hilo ni Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) kumtaka 'ami yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), al-'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhu) awaombee mvua kulipokuwa na ukame (al-Bukhaariy).

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share