Mume Anamfanyia Uchawi – Je Adai Talaka?

SWALI:

 

Asalam Aleykum. Natumai kwa uwezo wa Allah Aaza wa Jaala ni wazima wa afya njema.

 

Mama yangu mdogo, mume anatabia ya kumfulia usiku wa manane kila siku hata kama wataenda ugenini, kuna siku aliporudi kazini mumewe akamkata kucha za mikono na miguu huyo mama yangu. Baada ya siku tatu amezikuta kucha zake zimewekwa chini ya tendegu la kitanda chumbani na hirizi mbili nyekundu, alishtuka sana na amenifata mimi nimpe ushauri, na mimi elimu yangu ni ndogo sana ndio naomba ushauri wenu je afanye nini, Je adai talaka kwani amemwambia mumewe kuhusu hirizi hizo na kucha zake akajitia kulia tu wala hajamwambia kitu.

 

Tafadhali sana naomba mnisaidie tatizo hili ili asiende kinyume na maarisho ya dini.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume anayefanya uchawi.

 

Haifai kwa mke kuomba talaka kwa mumewe mara moja hivi mpaka afuate mkondo na mfumo wa sheria kuhusu tatizo ambalo linatokea baina yake na mumewe.

 

Yataka tufahamu kuwa shirki ni dhambi kubwa katika Uislamu ambalo lau mwenye kufanya hatotubia basi ataingia Motoni. Na pia mwenye kufanya shirki ‘amali zake zote huwa bure na ni yenye kuangamiza. Anaonya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

 

((إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللّهُ عَلَيهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَار))

((Kwani anayemshirikisha Allaah hakika Allaah Atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru)) [Al-Maaidah: 72]

 

((إِنَّ اللّهَ لاَ يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَلِكَ لِمَن يَشَاء وَمَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدِ افْتَرَى إِثْمًا عَظِيمًا))

 

 

 

((Hakika Mwenyezi Mungu Hasamehe kushirikishwa, na Husamehe yaliyo duni ya hilo kwa Amtakaye. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi kubwa)) [An-Nisaa: 48]

 

 

Kwa hiyo mama yako mdogo anataka afanye yafuatayo:

 

  1. Ajaribu kuzungumza naye kwa njia mzuri, wakati ambao anaona mumeweametulia na ana makini ya kuweza kumsikiliza. Haitakiwi kwake kutumia maneno mabaya, bali anafaa atumie busara na maneno ya upole na laini kuhusu tatizo hilo.

 

 

  1. Ikiwa mumewe hakukubali na ameshikilia hilo lake la uchawi na ushirikina basi anatakiwa aitishe kikao baina yake (mke), mumewe, wazazi au wawakilishi wake na wa wa mumewe. Ikiwa kweli wanataka suluhu Allaah Aliyetukuka Anawahakikishia kuwa hilo litapatikana bila ya wasiwasi wowote. Ikiwa bado mume amekaidi na hataki kuacha tabia hiyo mbaya, itabidi aende katika njia ya tatu.

 

  1. Hii ni kwenda kwa Qaadhi au yule Shaykh aliyewaozesha au Shaykh yeyote mwenye ucha Mngu, elimu na uadilifu kuweza kumshitakia hilo la mume. Na bila shaka ikiwa mume hataki kubadilika itabidi Qaadhi awaachishe. Na Allaah Aliyetukuka Atakupatia subira katika wakati huu wa dhiki na shida.

 

 

Nasaha yetu kwake ni kuwa anatakiwa ajikinge na hayo ya mumewe kwa kusoma adhkaar za asubuhi na jioni na kusoma Suratul Ikhlaasw, Suratul Falaq na an-Naas mara tatu tatu wakati wa asubuhi na jioni na anapokwenda kulala. Nyiradi hizo zinapatikana katika viungo vifuatavyo:

 

 

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

 

027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni

 

 

Ruqyah: Kinga Na Tiba Katika Shariy'ah

 

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Amkinge na hayo ya mume na Amuongoze mumewe.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share