Isbaal: Vazi La Mwanamme Lenye Kuvuka Mafundo Ya Miguu (Uburuzaji) - 1

 

Imetayarishwa Na

 

Abuu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Bismillaahi Rahmaani Rahiim

 

 

Isbaal ni urefushaji wa kitu na makusudio hapa katika makala hii ambayo itazungumzia vazi la mwanamme, makusudio yake kishari’ah ni kuvaa kivazi chochote chenye kuvuka chini ya mafundo ya miguu kwa mwanamme; iwe ni kikoi, shuka, kanzu, joho au suruali.  Nalo ni jambo lenye kukatazwa na limeharamishwa kwa nuswuus (maandiko) mbalimbali ya kishari’ah kutoka katika Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Lengo la makala haya, ni kuwatanabahisha Waislam wanaume kuhusiana na ubaya na madhara ya jambo hilo na pia kuweka sawa ufahamu wa makatazo hayo kuwa hayawahusu tu wenyye kuvaa kwa kiburi au kwa fakhari, bali ni kwa wanaume wote wa hali zote.

 

Kwa kumkumbusha aliyesahau, kumjuza asiyejua, na kumweka sawa mwenye ufahamu wa kinyume wa Hadiyth hizo za Nabiy wetu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tutakuwa tumesaidiana katika kuyaepuka makatazo ambayo yanaweza yakawa sababu ya kutupwa motoni kwa jambo ambalo si zito kabisa kuliepuka. Na pia kwa kukumbushana huku, kutatusaidia kufuata mafunzo ya kipenzi chetu na kufanana naye pamoja na Maswahaba zake wema kama tutakavyoona katika makala haya in shaa Allaah.

 

Na kwa kuwa wengi wetu wanaliona jambo hili la Isbaal ni jambo dogo sana na halina maana hata ya kulizungumzia au kukumbushana, tunapenda kumkumbusha mwenye fikra finyu kama hiyo kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitujulisha kuhusu watu wa makaburi mawili ambayo alipita katikati yake, akasema:

 

“Hakika hawa wanaadhibiwa na hawaadhibiwi kwa mambo makubwa; ama mmoja wao alikuwa hajilindi na chembe chembe za mkojo, na mwengine alikuwa akipita na kuhamisha maneno (umbea)” [Al-Bukhaariy na Muslim.]

 

Makusudio hapo ya kuwa walikuwa hawaadhibiwi kwa mambo makubwa, ni kuwa kwa mtazamo wao au dhana zao, hayo waliyokuwa wakiyafanya yalikuwa si makubwa kwao. Lakini kiuhakika hayo ni makubwa na ndio maana wakawa wanaadhibiwa.

 

Hivyo, ndugu Waislam, wale wenye mawazo ya kuwa suruali yake ikiwa ndefu na kuvuka mafundo yake ya miguu, kuwa  ni jambo dogo sana, basi ni bora ajihadhari tena ajihadhari na amche Mola wake mapema. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) singeweza kutoa makemeo makali kama tutakyosoma huko chini ikiwa jambo hilo si zito na kubwa. Suruali zetu, kanzu zetu, majoho tunayovaa ya kuolea au kutolea khutbah za Ijumaa na siku ya ‘Iyd au suti za ofisini na za harusini, zisije kuwa ni sababu ya kututumbukiza kwenye moto na kufanya tusitazamwe na Allaah, au kusemeshwa Naye au kutakaswa Naye na mwisho kupata adhabu iumizayo.

 

Hadiyth zifuatazo zinatoa kwa uwazi makatazo ya mtu kufanya Isbaal (kuburuza/kuburuta nguo yake):

 

1- Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Chenye kuvuka chini ya mafundo ya miguu katika vazi hupelekea motoni” [Al-Bukhaariy]

 

2- Kutoka kwa Abu Dharr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Watu watatu Hatowasemesha Allaah siku ya Qiyaamah, na  Hatowatazama, na Hatowatakasa, na watakuwa na adhabu iumizayo. Akarudia mara tatu. Abu Dharr akasema: Wameangamia na wamekhasirika hao ni nani ee Rasuli wa Allaah? Akasema (Nabiy): (Hao ni) Al-Musbil – Mwenye kuburuza nguo yake, Mwenye kutoa na kukizungumzia (kusimbulia) alichokitoa, Na mwenye kuuza bidhaa zake kwa kutumia kiapo cha uongo” [Muslim]

 

3- Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) anasema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Mtu mmoja alipokuwa anatembea, huku anaburuza nguo yake kwa kibri, alifanywa amezwe na ardhi na ataendelea kudidimia ndani yake mpaka siku ya Qiyaamah” [Al-Bukhaariy]

 

Pamoja na makatazo yote hayo yaliyotangulia yaliyoambatana na makemeo, makaripio, na maonyo ya mwisho mbaya wa jambo hilo,  na pamoja na kuwa Isbaal – kuburuza nguo ni katika madhambi makubwa, lakini utakuta watu wengi wanatumbukia katika madhambi hayo ima kwa wengi kutokujua ubaya wake, wengine kwa kughafilika, na wengine wanaojua hayo bado wanaendelea kubaki katika hali hiyo wakidai kuwa makatazo hayo yanahusu wenye kuvaa nguo ndefu (wanaoburuza au kuburuta) kwa kiburi wakitegemea baadhi ya Hadiyth zinazoonyesha hivyo.

 

Hata hivyo, mtu huyo huyo anayetoa hoja hiyo; awe ni Mwanachuoni, mtafutaji elimu au mtu wa kawaida, anajua wazi kabisa kuwa, ikiwa mwenyewe ameamua kuvaa kwa kuburuza vazi lake hilo pamoja na kufahamu maelezo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au utamkuta amekwenda mwenyewe dukani na kuchagua vazi refu lenye kuburuza, au aende kwa fundi na kumtaka amshonee suruali au kanzu yenye urefu huo unaovuka mafundoni na labda wakati fundi akiteremsha utepe wake wa kupimia kwenye mafundo yake, atamwambia teremsha kidogo chini ya mafundo…je, hapo ataweza kudai kuwa hicho si kiburi na hali ameshasikia au kuziona au kujulishwa Ahaadiyth zote za Mtume zenye kukemea, kukaripia, na kukataza jambo hilo? Na kama hicho si kiburi basi kiburi kitakuwa kipi?

 

 

Itaendelea in shaa Allaah…/2

 

Share