Mirungi - 2: Historia, Madhara Na Mikasa
Mirungi - 2 (Historia, Madhara Na Mikasa)
Abuu 'Abdillaah
BismiLlaahi Rahmaani Rahiym
Historia Yake
Inaaminika kuwa Ethiopia ndio asli yake kuanzia karne ya 15, na ikaenea katika milima ya Afrika Mashariki na Yemen. Ingawa vilevile kuna wanaoamini kuwa ilianzia Yemen katika karne ya 13 kabla ya kuenea hadi Ethiopia na nchi za jirani.
Kutoka Ethiopia na Yemen, mti au mmea huo ulienea sehemu mbalimbali za Arabuni, Somalia, Sudan, Kenya, Tanzania, Uganda. Congo, Malawi, Zimbabwe, Zambia hadi Afrika ya Kusini.
Baadhi hudai kuwa matumizi yake yanarejea miaka ya nyuma sana tokea wakati wa Wamisri wa kale ambao inasemekana walikuwa wakiitumia kama madawa ya jadi kwa baadhi ya magonjwa.
Anaeleza mwandishi wa Kimalaysia ‘Abdullaah bin ‘Abdil-Qaadir kuwa alipokuwa Yemen mwaka 1854, aliona ada na tabia ya utafunaji Mirungi huko Al-Hudaydah. Anaeleza: “Niliona jambo la ajabu katika mji huu –kila mtu anatafuna majani kama mbuzi anavyokula akameza na kisha kucheua kisha hutafuna tena kile alichokicheua. Kuna aina ya tawi, si pana sana kiasi cha urefu wa vidole viwili, ngumu kiasi, watu hutumia aina hii ya tawi au jani na kutia mdomoni na hutumiwa na viambatanishio vingine kuila, tawi hili hutiwa lote mdomoni na kutafunwa. Wanapokuwa wengi na kula kwa pamoja, utaona mabaki ya majani hayo yamerundikana mbele yao. Wanapotema mate, mate yao huwa ya rangi ya kijani. Kisha nikawauliza kuhusu hicho wanachokula: ‘Ni faida gani mnayopata kwa kula majani hayo?’ Wakajibu, ‘Hakuna chochote, ni jambo tulilolizoea lenye kutugharimu ambalo tumekulia nalo’. Wale wanaokula majani haya inawabidi watumie sana mafuta na asali, kwani wasipofanya hivyo wanaweza kuugua. Hayo majani hujulikana kama Kad (Mirungi).”
Wasifu Na Kilimo Chake
Mirungi ni mti unaoota polepole ambao unakuwa kwa urefu wa mita 1.5 hadi mita 20, kutegemea na eneo kijiografia na pia hali ya mvua ya eneo. Likiwa na majani ya kijani yaliyokoza ambayo yana urefu wa sentimeta 5 hadi 10 na upana wa sentimeta 1 hadi 4.
Ina ladha ya uchachu mkali na utamu wa mbali kwa wakati mmoja. Hufungwa katika majani ya migomba ili kuhifadhi ubichi wake. Kawaida huvunwa asubuhi sana na kuuzwa mchana wake au usiku wake, kila inavyokaa sana hupunguza ubora wake kwa walaji na thamani yake. Na kwa sababu walaji wa Tanzania hutegemea zaidi Mirungi kutoka Kenya, huwa hawapati ule ubora unaotakikana kutokana na umbali na kutofika kwa haraka; ingawa walaji wa Arusha hupata haraka zaidi kwa ukaribu wake na Nairobi kuliko wale wa Dar na Zanzibar au miji ya bara ya mbali kama Mwanza na kwengineko.
Kwa hivyo, majani ya Mirungi yanapoanza kukauka, kemikali ile kali ya aina ya cathinone inakauka pia na inabakia ile ambayo sio kali: cathine, na ndio maana mirungi inaposafirishwa inawekwa katika mifuko maalum ya plastiki au kufunikwa na majani ya migomba ya ndizi ili ihifadhike vizuri.
Mirungi ni zao lenye kuwaingizia wakulima Yemen kipato kikubwa na ndio maana wengi wameanza kuacha kilimo cha kahawa, na hutumika asilimia 40 ya matumizi ya maji ya nchi nzima kwa kilimo chake, pamoja na uzalishaji wake kuongezeka kiasi cha asilimia 10 hadi 15 kila mwaka. Matumizi ya maji yamekuwa makubwa kiasi cha hifadhi ya maji ya San’aa mji mkuu wa Yemen kupungua na ikiendelea namna hii basi baada ya miaka kumi tu maji yatakauka na kwa hali hiyo imefikia serikali kugawa maeneo kwa kuwahamisha wakazi wa San’aa kwenda kuishi maeneo ya pwani ya Bahari nyekundu.
Shamba La Mirungi Huko Yemen
Matumizi ya Mirungi aghlabu hutumika katika maeneo yanayolimwa zaidi na maeneo ya jirani na yale ambayo hufika Mirungi haraka ingali bado mpya mbichi na safi kwa sababu ya mzimuo wake. Kila inavyokaa mzimuo wake na upandishaji wa ‘handasi’/ ‘nakhwa’ yake hupungua.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza ya kwamba zaidi ya masaa 14.6 milioni yanapotezwa kila siku katika ulaji wa Mirungi huko Yemen. Ripoti hiyo, iliotolewa katika tovuti ya WHO, inaonyesha ya kwamba asilimia 80 ya watu wazima (male adults) wanatafuna Mirungi kila siku kwa muda wa masaa matatu mpaka manne hadi matano wakati ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wamo pia katika tabia hii yenye hatari.
Mirungi ni kileo kinachotumika sana kama ‘mkusanyiko wa kijamii’ katika maeneo mengi, na huwajumuisha zaidi wanaume ingawa baadhi ya sehemu na kwa miaka ya karibuni wanawake wamevamia sana uraibu huo haswa maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki kama Mombasa, Tanga na Dar-es-Salaam na mji kama Arusha ambao pia umekumbwa na ugonjwa huo kwa vijana wengi wa mjini. Na hupendelewa na madereva wa magari makubwa wanaosafiri safari ndefu, madereva wa abiria na hata wa magari ya kukodishwa kwa kuamini kuwa inawafanya wawe macho na makini. Vilevile hutumiwa na wanafunzi wakiamini kuwa inawafanya wasome muda mrefu na kukesha, kadhalika walinzi wa usiku huona inawasaidia kuwa macho usiku. Na baadhi ya watu hutumia kwa kisingizio cha kukesha kwa ajili ya kufanya ‘Ibaadah za usiku.
Nchi kama Tanzania, imepigwa marufuku lakini serikali kwa kutofuatilia kwa karibu kumefanya kuwe kunaliwa hadharani na bila woga wowote. Hufuatwa sheria pale maaskari wanapotaka kupata chochote kutoka kwa walaji na ni nadra kusikia mla Mirungi katiwa ndani, na akitiwa ndani basi hutolewa mara moja bila kufikishwa mahakamani.
Huko Somalia, waliposhika madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na kuleta amani ambayo haikuwahi kuonekana Somalia, Baraza La Juu La Mahkama Ya Kiislam, walipiga marufuku kuliwa mwezi wa Ramadhaan na kusababisha maandamano na upinzani huko Kismayo. Na mwaka huo huo katika mwezi wa Novemba, Kenya ilipiga marufuku ndege kwenda Somalia wakitaja ni sababu za kiusalama, hali ambayo ilisababisha upinzani kutoka kwa walimaji Mirungi. Mbunge wa Ntonyiri, Meru ambayo ndio eneo lenye kutegemewa sana Afrika Mashariki kwa ulimaji wa Mirungi, alieleza kuwa imetengwa ardhi maalum ya kulimia Mirungi, ambapo tani 20 zenye thamani ya Dola Laki 8 ($800, 000) husafirishwa kila siku kuelekea Somalia na hivyo kizuizi cha serikali kitailetea taifa madhara ya kiuchumi na kipato kama hicho kwa siku.
Aina Zake
Alenle (yenye majani mapana mengi, na ni ghali) – Yemen, Ethiopia na Kenya
Kangeta – Kenya
Giza (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ndogo) – Kenya
Mbaga (ni aina ya mirungi iliyo ndogo ya aina duni ambayo aghlabu ni ya bei ya chini -japo kuna baadhi ya mashamba machache sana hutoa aina yenye afadhali- na huliwa na wasiomudu kununua aina za ghali) – Tanzania
Madhara Yake
“Familia nyingi zinateketea, wake kukimbia waume zao, waume kutojali familia zao; hawataki kufanya kazi, jamii kujaa wavivu waombaji, wazazi na wakwe kulea wajukuu wasiongaliwa na wazazi wao, ulaghai na maasi kuzidi, ‘Ibaadah kupuuzwa, uchumi kuporomoka…”
Naam, tukiyaunganisha maneno hayo na tunavyoona hali ya walaji, hakika yana ukweli mtupu usiopingika kwa wanaojua hali hiyo katika jamii.
Tutajaribu kuyaorodhesha madhara mbalimbali yanayosababishwa na ulaji Mirungi.
Madhara Ya Kidini Na Kimaadili
1. Kupitwa na vipindi vya Swalah au kutokuswali kabisa;
2. Swawm haikamiliki – katikati ya mchana wa Ramadhaan watu huhangaika kutafuta Mirungi na kucheza bao, keramu, dhumna, kutazama mipira na sinema. Jambo la kwanza baada ya futari, watu huanza kusaga Mirungi. Hakuna Swalah za usiku, hakuna ‘Ibaadah nyingine yoyote, hata Swalah ya Alfajiri huwapita walaji wengi kwa sababu Shaytwaan wa Mirungi huwaambia wakalale muda mchache tu kabla ya Swalah ya Alfajiri! Kuamka kwao ni mchana au Alasiri, Ramadhaan inakuwa haina uzito wowote kwa maisha ya mla Mirungi;
3. Mchanganyiko baina ya wanaume na wanawake;
4. Uongo – hii ni kawaida kwa wengi ili wafikie malengo ya kupata wakitakacho; ima kudanganya wengine kwa kuwakopa pesa za kununulia Mirungi na kisha hawarejeshi madeni hayo. Na pia wanapokopa husingizia matatizo makubwa waliyonayo wao au jamaa zao kama maradhi, matibabu, ada za shule, n.k. ili waweze kukubaliwa kupata mikopo hiyo. Aghlabu wanapokopa hawasemi ukweli kuwa wanataka pesa za kununulia Mirungi; maana hakuna atakayewakopesha;
5. Usengenyaji – vikao vingi vya walaji huwa ni mazungumzo ya kidunia, mipira, filamu, kujadili mambo ya siasa, jamii, na kujadili maisha ya watu, maingiliano ya kindoa, na wao kwa wao kutoa siri zao za ndani na kutaja maovu yao waliyowahi kuyafanya;
6. Uropokaji, uchache wa adabu, ujuaji wa kila kitu, mlaji akiongelea siasa basi hakuna mwanasiasa kama yeye, akija kwenye mpira wa miguu na hususan ligi ya Uingereza, basi hakuna anayeichambua ligi hiyo kama yeye… na mtihani mkubwa na msiba ni kuwa hata mas-ala ya Diyn wao pia ni wataalam wakioongelea Taariykh na kwanini fulani aliuliwa na wangapi waliritadi baada ya Mtume na kwanini fulani walikuwa hawastahiki Ukhalifa walimdhulumu fulani n.k.;
7. Upungufu wa hayaa;
8. Kupoteza muda mkubwa katika vikao hivyo;
9. Kuomba omba – wengi huwa hawana uwezo wa kununua Mirungi kukidhi mahitaji ya uraibu wao, na hivyo kuwapelekea kuwa waombaji kwa wengine ima wa pesa za kununulia au uombaji wa Mirungi kwa walaji wenzao;
10. Maasi – baadhi ya vikao vya Mirungi hutawaliwa na kutazamwa sinema za uchi ili kusukumia handasi zao. Hali hiyo ya uchafu wa maadili na kujitumbukiza katika uharamu, huwakutanisha wazee kwa vijana na matokeo kupoteza heshima baina yao, na pia nyumba hizo kupoteza hadhi katika jamii na nyakati nyinginezo kuwatukanisha wake za wenye nyumba hizo kwa machafu yanayoendelea hapo. Baadhi ya nyumba waume wamepoteza wake zao kwa marafiki zao kutokana na maingiliano huru yasiyo na mipaka baina ya wake kwa waume;
11. Kuharibiwa itikadi zao – mji kama Arusha, vijana wengi wamebadili itikadi zao za Diyn baada ya kujiunga na uraibu huo na kushiriki vikao vyake. Ndani ya vikao hivyo kuna kundi la wakongwe ambao wameweza kuwashawishi vijana kutoka katika itikadi waliyozaliwa nayo na kujiunga na itikadi ya kukufurisha na kulaani Maswahaba na wema waliopita. Imefikia hali ya kusikitisha sana kwa kuona kundi kubwa la watu likiwa limekaa barazani likicheza Dhumna (Domino) na huku Swalah ya Jama’ah ikiadhiniwa, kuqimiwa, na kuswaliwa ubavuni mwao kwenye Msikiti na wala hawana wasiwasi tena wakifanya zogo na kelele na kuzipigisha kete zao kwa nguvu kana kwamba wanashindana na sauti ya Mnadi Swalah. Maskini na wao wanajiona wako sawa kabisa kwenye haki! Na wanapotanabahishwa waache lahwu zao na waende kuswali, husema kuwa wao wanajumuisha Swalah kutokana na Itikadi yao. Ukweli wengi hata kuswali hawaswali;
12. Haki za kifamilia kukiukwa – haki za kinyumba; waume wanakuwa hawatoa haki zao ima kwa kukesha nje ya nyumba zao, au kwa kudhoofika nguvu zao za kiume na pia kumaliza haraka wanapofanya tendo la ndoa na hivyo kusababisha wake kukosa haki za msingi;
13. Talaka kuzidi – kwa sababu tulizotaja katika kipengele kilichotangulia, wake wengi hushindwa kuvumilia katika ndoa zao na kuamua kudai talaka;
14. Haki za watoto hazitekelezeki – kwa kuwa walaji wengi hawafanyi kazi, na wanaofanya kazi hutumia gharama nyingi kwenye ulaji, hivyo hakupatikani matumizi nyumbani au matumizi kubanwa na haki kutotimizwa. Walaji wengine hulelewa watoto wao na wakwe zao au wazazi wao;
15. Kutoka nje ya ndoa – baadhi ya walaji wanakuwa si waaminifu kwenye ndoa zao, kadhalika baadhi ya wake wanashindwa kuvumilia kuwa wapweke kila mara kwa kuwa waume zao hukesha nje ya nyumba zao, na wakirudi ni usingizi, wakiamka ni kutafuta Mirungi, na hivyo hupelekea wake hao kukosa uvumilivu na kwa kuzidiwa kwao na matamanio yao –na kwa uchache wa Iymaan- kunawapelekea wao kuyahamisha matamanio yao pengine.
16. Walaji wa uraibu huu hukesha kuorodhesha mambo watakayoyafanya siku ifuatayo, pasi na kuyatekeleza, na kuendelea katika hali hiyo kila mara bila ya mafanikio yoyote.
17. Wengine husingizia eti wanakesha kwa ajili ya ‘Ibaadah, lakini ni aina gani ya ‘Ibaadah inayofanyika wakati mashavu yametuna kwa kujaa majani hayo?
Madhara Ya Kiafya
Matatizo na madhara ya Mirungi yaligunduliwa mwanzo katika mwaka 1935 na League Of Nations, Mwaka 1970 taasisi ya tiba ikaitenga madhara ya cathinone yanayopatikana katika Mirungi ambayo kikemikali inafanana na amphetamine, na hivyo katika mwaka 1971 ikaorodheshwa na United Nation kuwa ni miongoni mwa madawa ya kulevya.
Bwana mmoja kutoka Canada ajulikanaye kama Mathew Bryden aliyekuwa akifanya kazi na mashirika ya msaada kwa miaka mitatu huko Somalia anasema, “Watumiaji wengi wa Mirungi wamejikuta wakipambana na msisimko wake ili waweze kupata usingizi au hata kufanya kazi kisawasawa. Wanaelekea kwenye pombe au madawa ili kupata mapumziko au kupunguza hali ya wasiwasi. “Hali ilivyo Mogadishu ni watu kutawaliwa na nguvu za Mirungi, madawa au pombe,” Bwana Bryden anaendelea, “Unakuwa umevurugikiwa kabisa. Ima uharibikiwe kikamilifu au upoteze mwelekeo wa hali halisi.”
Utumiaji wa Mirungi husababisha madhara mbalimbali kiafya kama:
1. Magonjwa ya vidonda vya tumbo (ulcers);
2. Ukosefu wa haja kubwa (constipation);
3. Utumiaji wa muda mrefu husababisha kuharibu utendaji kazi wa ini, na pia kusababisha ubadilikaji rangi meno, kudhoofika, na fizi kuuma na harufu ya mdomo;
4. Upungufu wa msukumo wa kufanya jimaa (sex drive). Na pia kuwahi kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu;
5. Kupatwa na ugonjwa wa futuru/futuri/bawasiri/baasili – nyama inayoota kwenye utupu wa nyuma;
6. Upungufu wa usingizi;
7. Humpelekea mlaji kutawaliwa nayo (Addiction);
8. Walaji wengi huvuta na sigara, hata yule aliyekuwa havuti kabla ya kuanza kula Mirungi, hujikuta akizama kwenye uvutaji, na madhara huwa maradufu;
9. Madhara ambayo bado kinamama walaji Mirungi hawajagundua ni kwamba mtoto anayezaliwa na mama mlaji Mirungi mara nyingi hukataa kunyonya titi la mama yake kwa sababu ladha ya maziwa inabadilika kwa ajili ya utumiaji wa madawa (pesticides) unaotumiwa na wakulima wa Mirungi kama inavyoeleza utafiti uliofanyika na Chuo Kikuu Cha Aden (Aden University). Utafiti huo unazidi kueleza ya kwamba aina ya madawa yanayotumiwa na wakulima ni zaidi ya 118 (na nyingi katika hizo ni katika zile zilizokatazwa kisheria [illegal pesticides]) na ambazo zinasababisha asilimia 70 ya ugonjwa wa saratani (cancer) huko Yemen;
10, Utafiti mwengine kule Ethiopia unatueleza ya kuwa mtoto wa mama mwenye kula Mirungi kwa wingi huwa hana uzito wa kawaida wakati wa kuzaliwa;
11. Ukosefu wa hamu ya kula chakula na mengi mengine.
Madhara Ya Kiuchumi Na Kijamii
1. Kuwa na taifa la wavivu wapenda starehe wasiotumika;
2. Jamii ya Kiislamu iliyo chafu kimaadili na isiyosimamisha ‘Ibaadah;
3. Harakati za kunyanyua uchumi kuwa duni, harakati na juhudi zinazopatikana huwa ni za kuwazika na kutajika tu. Anapokuwa mtu amesha'khazin' fundo lake la Mrungi kwenye shavu lake linalovimba kama pulizo kwa kujaa ‘taksima’, hapo atakuwa anatoa mipango na mikakati mizito mizito ya kujenga maghorofa, kuanzisha miradi ya mamilioni..lakini yote ni mipango inayopangwa na ‘Handas’ na ‘Nakhwa’, baada ya kutemwa gomba, mipango yote iliyokuwa ikipangwa huyeyuka na kuwa kama ngano za Alinacha….hapo tena husubiriwa siku ya pili ya kusagwa na mipango yake mingine ya mamilioni ya kuwazika;
4. Kulala mchana kutwa – kukosekana harakati na michakato ya utafutaji rizki;
5. Kuzidi kwa omba omba – bila shaka ikiwa watu hulala mchana mzima na hawahangaiki kufanya kazi, kinachotarajiwa ni kuzidi kwa wanyanyua mikono na wainamisha vichwa wanaoongea kwa huzuni kama waliofiwa wakati wanatupa makombora yao ya maombi;
6. Vijana wa mjini hawataki kuajiriwa – kwa sababu wanajiona ni ma-alwatwan, kwa hiyo –kwa mtazamo wao- haiwezekani kwao kutumwa au kuajiriwa! Matokeo yake uchumi wa wakazi wa mjini kuporomoka na mwisho wake ni wao kukodisha nyumba zao kwa wageni (wanaotoka miji ya mbali) zikawa maduka, na mwisho wake hufikia kuuza hizo nyumba zao ambazo wamerithi kutoka kwa wazee wao waliokuwa wakihangaika na kuchapa kazi;
7. Huwapelekea baadhi yao kujidunisha na kuwatumikia mabwana wakubwa si kwa lingine ila kwa ajili ya kilo ya Mirungi.
Vituko Na Mikasa Vya Mirungi Na Walaji Mirungi
Kama inavyoitwa petroli “dhahabu nyeusi,” Mirungi inaitwa na walaji wake “dhahabu ya kijani”.
Matukio yafuatayo hapa chini ni ya kweli yamewahi kutokea na hakuna kilichozidishwa; yanathibitishwa na walaji katika sehemu hizo:
1. Mmoja wa wasagaji Mirungi alipohandasika alitundika koti lake pale alipo nzi ukutani akidhani ni msumari, na la kushangaza zaidi, ni pindi nzi yule aliporuka kuhamia kwengine, bwana yule alimfuata pale anapotua na kujaribu kutundika koti lake kwa mara ya pili.
2. Mwengine alijigonga kwenye mti wa stima barabarani na kuuomba msamaha akidhani amemgonga mpita njia mwenzake.
3. Na kuna tukio la kuhuzunisha huko Arusha na Mombasa, ni pale walipokuwa wakila Mirungi na kutazama sinema chafu, nyumba hiyo ambayo wamebandika Aayah za Qur-aan kwenye kuta –hali ya kuidhalilisha Qur-aan kuifanya ni mapambo na kupoteza lengo la kushushwa kwake-, baada ya kuwa wanatazama maasi yao, mmoja wao akashtuka na kusema ‘AstaghfiruLlaah!!’ na kukimbia kuigeuza ile fremu ya Aayah za Qur-aan kwa sababu aliona ni kuivunjia heshima! Na baada ya kumaliza maasi yao, wakaigeuza fremu ili zile Aayah zirejee kuonekana tena kama awali. Mwengine huko Mombasa alikuwa na gazeti lake la kufunika hizo Aayah pindi anapoanza kutazama balaa hizo, na akimaliza hutoa gazeti hilo ambalo huwa ni kwa kazi hiyo.
4. Kuna mmoja wa walaji Mirungi alikamatwa huko Arusha na kupelekwa kituoni – kama tulivyosema awali ni tukio la nadra mtu kutiwa ndani kwa kula Mirungi- na wenzake waliposikia, wakamfuata kituoni kumtoa, lakini hawakukumbuka kuwa mashavuni mwao wamejaza taksima ya Mirungi na hali wako kituoni.
5. Mlaji mmoja baada ya kupata ‘Nakhwa’ iliyomkolea, wakati walipomaliza kikao chao cha Mirungi akaondoka amevaa viatu vya mwengine; alipofika mbele ya safari na kutanabahi, tayari akabaki kwenye tahayuri ya kujiona kuwa atashukiwa kwa wizi na hali ilikuwa ni raha za ‘Nakhwa’.
6. Dereva mmoja wa Taksi huko Arusha alikuwa amembeba abiria mzungu aliyekuwa akielekea kituo cha ndege cha KIA (Kilimanjaro International Airport) ambacho kipo katikati ya mji wa Arusha na Moshi, kwa kupandwa na ‘Handasi’, alijikuta akikipita kituo hicho na kufika Moshi mjini. Akaanza kuuliza kituo kiko wapi – pamoja na kwamba anakijua kilipo kituo ila ni ulevi wa Mirungi umempoteza-, akaulizwa ‘Kwani wewe umetokea wapi?’ Akajibu, ‘Arusha’, akaambiwa, ‘Mbona kituo umekipita huko nyuma kabla hujaingia Moshi?’…akachanganyikiwa na kuanza kurudi kwa kasi, hata alipofika kituoni, mzungu keshakosa ndege!
7. Na huko Australia: Bwana na Bibi McDavitt wa huko Perth (Australia) walipewa “zawadi” ya mmea na rafiki yao wa Kiafrika ili wauoteshe katika bustani yao kubwa nzuri iliyopo mbele ya nyumba yao. Mti ulikuwa mkubwa na mzuri wa kuvutia. Mti ulipokuwa mkubwa kiasi, rafiki yake wa Kiafrika aliomba apunguze (pruning) majani na matawi ya huo mti huo ili uendelee kuwa mkubwa na wa kuvutia. Mtindo huu uliendelea mara kwa mara na kila mara mti unapoanza kuchipuwa vizuri, yule rafiki Mwafrika akawa anakuja na kuomba kupunguza matawi na majani kama ilivyo kawaida yake. Lakini siku moja, Bwana na Bibi McDavitt walishtuka walipoona watu wengine wa Kiafrika (na sio rafiki yao wa kila siku) wakikata matawi bila ya rukhsa yao. Hapo ndipo walipopatwa na wasiwasi kuhusu mti huo. Na baadaye wakagundua ya kuwa mti huo ni mti wa Mirungi! Wakaamua kuukata.
8. Na Djibouti: Tani kumi za Mirungi hupelekwa kila siku kwa ndege kutoka Ethiopia kuelekea Djibouti. Katika uwanja wa ndege, hakuna mgeni anayengojewa kwa hamu kama mgeni huyo (Mirungi). Zaidi ya magari 300 yanakuwa tayari kwenye kiwanja cha ndege kumpokea “mgeni” huyo wa thamani. Wafanya biashara wa Mirungi wanaitwa ‘Masultani wa Qaat.’ Ilitokea siku moja watu kushikwa na kiwewe kiwanja cha ndege walipopata habari ya kwamba huenda Mirungi isiwasili siku hiyo kwa sababu fulani fulani. Ilitokea fujo katika nchi na ilikuwa ni siku ya huzuni na watu waligoma kuondoka kiwanja cha ndege. Punde si punde, ndege iliwasili na watu walipopata habari hiyo, basi walikumbatiana kwa furaha na kupeana mikono kama vile ni Siku Kuu (‘Iyd). Djibouti imekataa kupiga marufuku mirungi kwa sababu inaingiza serikalini kila mwaka faida ya dollar 15,000,000.- Kwa hivyo, umefanya mkataba wa Kiserikali baina ya Djibouti na Ethiopia kuhusu kutochelewesha mirungi hata siku moja.
Hayo ni matukio machache kati ya matukio mengi yasiyo na idadi ambayo kurasa haziwezi kuorodhesha zote. Matukio yanayosemekana kutokea huko Yemen, Ethiopia, Kenya na Somalia yanawezwa kuandikwa vitabu kwa vitabu.
In shaa Allaah tutamalizia makala hii kwa kuona namna Wanachuoni mbalimbali walivyolieleza tatizo hili na kunyambua hukmu ya Uharamu wake kutoka katika viini vya Shari’ah ya Diyn yetu safi isiyo na nafasi ya uchafu na uraibu wowote wa kiwendawazimu.
Itaendelea in shaa Allaah…/3