Isbaal: Vazi La Mwanamme Lenye Kuvuka Mafundo Ya Miguu (Uburuzaji) - 2
Imetayarishwa Na
Abuu 'Abdillaah
BismiLlaahi Rahmaani Rahiim
Hapa chini tutaona hoja au madai tata za wanaotetea kuburuza/kuburura nguo na majibu dhidi ya madai hayo.
Hoja Mojawapo:
Kuwa Isbaal Inawahusu Wenye Kuvaa Kwa Kiburi Au Kwa Fakhari Tu
Baadhi ya watu wanarukhusu Isbaal kwa kudai kuwa makatazo yaliyokuja katika Hadiyth mbalimbali ni kwa wale tu wanaovaa kwa kiburi au kujifakharisha. Ima kwa wale wanaovaa tu bila kukusudia kiburi basi inafaa na hakuna ubaya wowote. Wakitoa hoja kwa kutumia baadhi ya Hadiyth, mojawapo ya Hadiyth hizo ni Hadiyth maarufu ya kumhusu Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa nguo yake ilikuwa ikiburuza, ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
“Mwenye kuburuza nguo yake kwa kiburi, Allaah Hatomtazama siku ya Qiyaamah” Abuu Bakr akasema: Ee Rasuli wa Allaah! Upande mmoja wa kikoi changu unashuka hadi niuvute na kuuzuia, Mtume akamjibu: Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi” [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy]
Majibu Ya Hoja Hiyo:
Kwa kujibu hoja yao ya kutegemea Hadiyth hiyo kuonyesha kuwa Abuu Bakr alikuwa akiburuza nguo yake, tunajibu kwa maneno ya Wanachuoni ambao wameunganisha Hadiyth za pande zote kuhusiana na suala hilo na kuweka ufahamu ulio sahihi:
1- Ametaja Mwanachuoni Ibn Hajar kuwa, katika masimulizi ya Imaam At-Tirmidhiy kuna ziada baada ya maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Atakayeburuza nguo yake kwa fakhari (kiburi), Hatomtazama Allaah mtu huyo siku ya Qiyaamah), akasema Ummu Salamah: Je, watafanyaje wanawake na mikia yao (nguo zao zenye kuburuza)? Akasema (Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Waongeze shibri (kiasi cha kiganja kimoja), Akasema (Ummu Salamah): Hata hivyo bado miguu yao itakuwa wazi. Akajibu (Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Basi wazidishe dhiraa na si zaidi ya hapo.”
Ibn Hajar akasema: Alivyofahamu – yaani Ummu Salamah – ni kuwa makatazo ya kuburuzwa kwa nguo makusudio yake ni kwa hali zote; iwe kwa kiburi au bila kiburi. Ndipo alipomuuliza Mtume hukumu ya wanawake kuhusiana na hilo kwa kuhitajia kwao kuburuza ili waweze kujistiri vizuri miguu yao ili isiwe uchi… kisha akaendelea kusema Ibn Hajr katika uchambuzi wake: Na Qaadhi ‘Iyaadhw amenukuu ‘Ijmaa’ (makubaliano) ya kuwa makatazo ya Isbaal ni kwa wanaume na si wanawake, na makusudio yake ni kuwa kukatazwa kwa Isbaal ni kwa kukariri kwake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Ummu Salamah ili kumfahamisha. [Fat-hul Baariy Mj. 10, uk. 259].
2- Na akasema Ibn Hajar (Allaah Amrehemu): Ama Isbaal bila ya kiburi, ni wazi kutokana na Hadiyth mbalimbali kuwa ni Haraam. Kisha akasema: Na ikiwa nguo ni ndefu kuliko urefu wa mtu mwenyewe basi hiyo huenda ikapelekea kwenye makatazo kwa ajili ya israfu na kufikia kwenye uharamu. Na vilevile inapelekea makatazo kwa kufanana nako na mavazi ya wanawake, na hii inawezekana zaidi kuliko sababu ya mwanzo. Na kadhalika ameeleza Al-Haakim usahihi wa Hadiyth iliyopokelewa na Abuu Hurayrah kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanamme anayevaa mavazi ya mwanamke. Vilevile yanapelekea makatazo ya Isbaal kwa mwenye kuvaa kutosalimika na kupatwa vazi lake na najisi kwa upande mwengine. [Fat-hul Baariy Mj. 10, uk. 263].
3- Ibn Al-‘Arabiy (Abuu Bakr) naye kasema: Haijuzu kwa mwanamme kuachia nguo yake kuvuka mafundo ya miguu, na akasema: Siburuzi kwa kiburi, kwa kuwa makatazo yanaweza kuhusu hali hiyo kimatamshi, na wala haijuzu kwa mwenye kuchukulia matamshi hayo ya makatazo kwa kiburi kuwa ndio hukumu akasema: Mimi hukumu hiyo hainihusu kwa kuwa ‘illa (sababu) yake hainihusu. Hakika anayesema hivyo, ajue kuwa madai hayo hayajasalimika, bali ni kuwa kurefusha nguo na kuvuka mafundo kunaonyesha kiburi chake (huyo mwenye kurefusha). [Fat-hul Baariy Mj.10, uk. 264].
4- Isbaal ni mwelekeo wa kiburi. Anasema Ibn Hajar (Allaah Amrehemu): Isbaal inalazimu kuburuzika kwa nguo, na kuburuzika kwa nguo kunalazimu kiburi japo ikiwa mwenye kuvaa hajakusudia kiburi. Na yanaungwa mkono maneno yake hayo na aliyosimulia Ahmad bin Muniy’i kwa upande mwengine kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kutoka katika Hadiyth ambayo inasema:
“Ole wako na kuburuza nguo (kuvuka mafundo ya miguu), kwani kuburuza nguo ni alama ya kiburi”. [Fat-hul Baariy Mj.10, uk. 264].
5- Amesema Mwanachuoni Imaam Muhammad bin Swaalih bin Al-‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) kuhusu Hadiyth hii,
“Mwenye kuburuza nguo yake kwa kiburi, Allaah Hatomtazama siku ya Qiyaamah” na Hadiyth hii, “Chenye kuwa chini ya mafundo ya miguu katika mavazi, basi ni motoni”: Kwa kuwa kumekhitilafiana adhabu hizo mbili, basi kunakatazika kuifanya hukumu hiyo (ya Isbaal) kuwa ‘Mutwlaq’ (ya jumla) ni yenye kuwa juu ya ‘Muqayyad’ (iliyofungamanishwa na kitu), kwani kanuni ya kubeba ‘Mutwlaq’ juu ya ni sharti kukubaliana ‘Nasw’ (maandiko) mbili katika hukumu. Ama ikitofautiana hukumu (kama ilivyo kwenye hizo Hadiyth mbili juu) basi haibebeshwi mojawapo juu ya mwenzake. Na hivyo ndivyo hata Aayah ya kutayamamu ambayo Amesema Allah:
“Na mpanguse nyuso zenu na mikono yenu kwayo” haikufunganishwa na Aayah ya Wudhuu ambayo Allaah Amesema:
“Na muoshe nyuso zenu na mikono yenu hadi kwenye viwiko” maana haiwi Tayammum hadi kwenye viwiko.
6- Naye Mwanachuoni Imaam Al-Albaaniy (Allaah Amrehemu) katika baadhi ya vikao vyake kwamba haijuzu Muislam kukusudia kurefusha vazi lake miguuni kwa madai kuwa hafanyi hivyo kwa kiburi, na anaunganisha hayo kwa maneno ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyomwambia Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu), “Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi”, kwa sababu Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuwa akivaa nguo ndefu, na Nabiy(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia, “Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi”, ila hayo majibu ya Mtume kwa Abuu Bakr yalikuwa ni kwa sababu Abuu Bakr vazi lake lilikuwa lamshuka lenyewe, na akawa akionekana ni kama mwenye kurefusha nguo. Na Mtume akamjibu kumwambia kuwa hilo ni jambo ambalo huchukuliwi kwalo, kwani hujakusudia na wala hukulifanya kwa kiburi. Hivyo, ni makosa kabisa watu kuuunganisha tukio la Abuu Bakr na kuburuza kwao nguo kwa makusudi kisha wakadai kuwa: ‘Sisi hatufanyi kwa kiburi’! Tukio la Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) haliwezi katu kuwa hoja ya wanayoyafanya.
7- Amesema Mwanachuoni Faqiyh Shaykh Muhammad bin Swaalih bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu):
“Hakika Abuu Bakr katakaswa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akatoa Mtume ushahidi kuwa Abuu Bakr si katika wale wanaofanya hivyo (kuvaa nguo ikaburuza) kwa fakhari. Sasa je, hao wanaovaa nguo zikavuka mafundo (zikaburuza) wamepata utakaso au ushuhuda kama huo wa Abuu Bakr?!
Lakini Shaytwaan anawafungulia baadhi ya watu milango ya kufuata yale maandiko yenye utata kwenye Qur-aan na Sunnah ili yaendane na matashi yao na yale wayafanyayo, na Allaah Ndiye Humuongoza Amtakaye katika njia nyoofu, tunamuomba Allaah Atupe sisi na wao hidaaya”
Na tunakhitimisha jibu la hoja hiyo ya watetezi wa Isbaal kwa Fatwa ya Mwanachuoni mkubwa wa miaka ya karibuni, aliyekuwa Mufti wa Saudi Arabia, Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz (Allaah Amrehemu) kuhusiana na maudhui hii, alipojibu swali lifuatalo:
Swali:
Katika Hadiyth ambayo maana yake inakusudia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema kuwa mwenye kuburuza vazi lake basi ni motoni, na sisi mavazi yetu yanazidi chini ya mafundo ya miguu na hatukusudii kuvaa kwa kiburi au kwa fakhari bali ni ada ambayo tumeizoea, je, kuvaa kwetu namna hiyo ni Haraam? Na je, vipi yule mwenye kuburuza vazi lake na hali yeye ni mwenye kumuamini Allaah. Naomba faida?
Jibu:
Imethibiti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa kasema:
“Chenye kuvuka chini ya mafundo ya miguu katika vazi hupelekea motoni” [Ameisimulia Imaam Al-Bukhaariy katika Swahiyh yake].
Na akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Watu watatu Hatowasemesha Allaah siku ya Qiyaamah, na Hatowatazama, na Hatowatakasa, na watapata adhabu iumizayo; (Hao ni) Al-Musbil – Mwenye kuburuza nguo yake, Mwenye kutoa na kukizungumzia alichokitoa, Na mwenye kuuza bidhaa zake kwa kutumia kiapo cha uongo” [Imesimuliwa na Imaam Muslim katika Swahiyh yake].
Na Hadiyth zenye maana hizi ni nyingi nazo zinakataza (zinaharamisha) Isbaal (kuburuza nguo) moja kwa moja japo mwenye kuburuza atadai kuwa yeye hajavaa kwa kiburi au kwa fakhari, kwani japo mvaaji atakataa hilo, lakini ajue kufanya hivyo ndiko kunakopelekea kwenye kiburi. Na pia katika hilo kuna israaf na kuzipelekea nguo kupata uchafu na kukomba najisi. Na ikiwa aliyevaa makusudio yake ni kiburi, basi hatari inakuwa kubwa na madhambi yanazidi kama anavyosema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Atakayeburuza nguo yake kwa kiburi Allaah Hatomtazama siku ya Qiyaamah”.
Na mipaka ya nguo ni kufika kwenye mafundo mawili ya miguu.
Haijuzu kwa Muislam mwanamme kuachia nguo yake kuvuka chini ya mafundo ya miguu kama zilivyotaja Hadiyth zilizotangulia.
Ama mwanamke yanatakiwa mavazi yake kishariy’ah yafunike miguu yake.
Kuhusiana na Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) yeye alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa vazi lake linamteremka na yeye si mwenye kutaka hivyo, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Wewe si mwenye kufanya kwa kiburi” Na makusudio yake ni kuwa mwenye kushuka nguo yake bila makusudio na huku akijitahidi kuizuia isishuke kama alivyokuwa Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) basi anakuwa haingii katika yale maonyo na makemeo yaliyokuja kwenye Hadiyth kwa sababu hakuacha nguo ishuke kwa makusudi. Na pia hakukusudia kiburi na hali hiyo ni kinyume na ile hali ya yule ambaye anaachia nguo yake iburuze kwa makusudi bila kuonyesha juhudi zozote za kuipandisha au kuizuia isiburuze, na kwa hivyo, mtu wa aina hii ataingia katika kundi la wanaofanya kwa kiburi na Allaah Anajua yaliyomo kwenye nyoyo za watu (japo watu watakuwa wanatoa visingizio mbalimbali).
Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vilevile ametoa maelezo (Hadiyth) mbalimbali kuonya kuhusu Isbaal na akasisitizia sana, na hivyo ni waajib kwa Muislam kujihadhari na yale Aliyoyaharamisha Allaah, na ajiepushe na vile vyenye kusababisha ghadhabu ya Allaah, na akome katika mipaka ya Allaah na ataraji thawaab na akhofu adhabu Zake kwa kuyafanyia kazi maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾
Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Hashr: 7]
Na kauli Yake Aliyetukuka:
وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٤﴾
Na yeyote atakayemuasi Allaah na Rasuli Wake na akataadi mipaka Yake Atamuingiza motoni, ni mwenye kudumu humo na atapata adhabu ya kudhalilisha. [An-Nisaa: 14]
Allaah Awawafikishe Waislam katika yale yenye Radhi Zake na yenye manufaa kwenye mambo ya Dini yao na dunia yao, Naye ni Mbora wa Usimamizi. [Mwisho wa kumnukuu Shaykh Ibn Baaz].
Wasiya Wa ‘Umar Bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) Baada Ya Kuchomwa Upanga Kabla Hajafariki:
Amesimulia [Imaam Al-Bukhaariy] katika Swahiyh yake kutoka kwa ‘Amru bin Maymuun – kuhusiana na kisa cha kuuliwa Khaliyfah Mwongofu ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) – amesema: “Mimi nikiwa nimesimama baina yangu na yake (yaani ‘Umar [Radhwiya Allaahu ‘anhu]) ila ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) (akiwa katikati) asubuhi aliyoshambuliwa, na alikuwa akipita baina ya Swaff mbili akisema: Nyookeni, hadi akawa haoni penyo, akatangulia (kuswalisha) akapiga Takbiyrah na nikamsikia akisema: Ameniua - wakati alipodungwa – kisha akataja kisa cha kubebwa na kupelekwa nyumbani kwake kisha akasema: Wakaja watu huku wanamuombea. Akaja kijana mmoja akamwambia: Kuwa na bishara njema Ee Amiyrul Muuminiyn kwa bishara ya Allaah kwako kuwa utasuhubiana na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); umetangulia katika Uislam kadiri nielewavyo, ukapewa uongozi na ukafanya uadilifu, kisha mwisho umepata Shahaadah (umekufa shahidi). Akasema (‘Umar): Napendelea yangekuwa hayo yananitosha si kwangu tu au dhidi yangu. Na wakati kijana huyo alipogeuka kuondoka, huku vazi (kikoi) lake kinavuka mafundo kwa urefu na kuburuza chini, (‘Umar [Radhwiya Allaahu ‘anhu]) akasema mrudisheni huyo kijana, na (aliporudishwa) akamwambia: Ee mwana wa ndugu yangu, nyanyua (pandisha) kikoi chako; kufanya hivyo kunaidumisha nguo yako, na kunakupa uchaji Allaah.
Ndugu Muislam, tuzingatie wasiya huu wa ajabu na wakati ambao umetolewa! Wakati damu yake Amiyrul Muuminiyn ikiwa inavuja kwa wingi baada ya kuchomwa upanga na Abuu Luuluu Al-Majuusiy Mfursi adui wa Allaah, na akiwa anayakabili mauti, lakini pamoja na yote hayo hakuweza kuvumilia pindi alipoona vazi la kijana yule likiburuza na akampatia wasiya huo ilihali yeye taabaan na yuko kwenye kuhudhuria mauti! Tukio hili linatujulisha kuwa kitendo cha Isbaal (kuburuza vazi) ni tendo zito na ovu ambalo halipasi kunyamaziwa.
Isbaal – Vazi La Mwanamme Lenye Kuvuka Mafundo Ya Miguu (Uburuzaji Au Kuburura) - 1