Zingatio: Matamasha Ya Ibilisi
Zingatio: Matamasha Ya Ibilisi
Naaswir Haamid
Hakika dunia ya leo imekuwa ni uwanja wa fujo, na kwa asilimia kubwa hakuna wanaadamu wala Waislamu walioshughulishwa na kutekeleza masuala ya kheri. Tunashuhudia namna tunavyoingizwa kwenye mambo ambayo ni wazi wazi yanakwenda kinyume na maadili ya Uislamu pamoja na silka za binaadamu.
Imekuwa ni ada vyombo vya juu kusimamia mambo ambayo hayana manufaa katika jamii ila tu ni yenye ladha ndogo ya mali. Hapo hupeperushwa bendera ya kulinda maslahi hayo kwa njia yoyote inayowezekana.
Yareti kama watasimama Waislamu wenye uchungu na Uislamu wao kwa kutoshiriki kwenye masuala haya machafu. Basi, yasingelifikia kuwa makubwa kama yalivyo sasa. Matokeo yake, tunaona ngoma za ajabu kabisa pamoja na tamasha zisizokuwa na maana yoyote kwetu sisi, jamii yetu wala kizazi chetu. Vyovyote watakavyoyaita, hayo matamasha asili yake ni matamasha ya sauti za "punda" ama "jahazi la moto". Na ni vyema tuulizane: Kwani haya matamasha hakuna kwengine pa kufanyika isipokuwa ndani ya ardhi zilizoshtadi kwa Waislamu??!
Tukumbuke kwamba, upofu wetu wa kujifanya hatuoni na kujikinaisha kwamba hakuna athari mbaya utatufikisha pabaya. Na hali iliyopo sasa ni sawa na kuwemo ndani ya shimo la kenge. Shimo ambalo tumelichimba wenyewe na tukajitumbukiza sisi wenyewe.
Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Mtafuata nyendo za wale waliokuja kabla yenu hatua kwa hatua mpaka itafika hadi wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia”. Wakasema (Swahaba): Ee Nabiy! Je, unamaanisha Mayahudi na Manaswara? Akasema: ((Hivyo nani basi mwengine?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Matamasha haya sio lolote si chochote ila ni kulenga kuwapotezea Waislamu muda wao na maadili yao mazuri. Humo ndani ya tamasha hizi, kunauzwa pombe ambayo imepewa jina jengine na kufanywa halali. Wanawake wanatembea utupu huku muziki ukiwarithisha uziwi wa vitendo na kiakili kwa kutosikia maneno ya Muumba hata kama wakikumbushwa kwa sauti iliyo kali hawasikii. Ni pombe ngapi zinazonywiwa humo? Tamasha hizi zinalenga zaidi kugeuza ardhi kuwa ni maeneo ya madanguro pamoja na kupata soko la bidhaa zao kama vile pombe, muziki na biashara haramu za kuuza miili.
Ndio sababu ya wenye akili na elimu sahihi ya Kiislamu wanaendelea kukemea wazi wazi tamasha kama hizi kwani zina hasara tupu. Hatima yake ndio tunaiona hii leo, kila jamii inachokifanya yageuka kuwa ni janga. Ndani ya vitovu vya tamasha hili Muumba hufanywa ni kinyago na hufanywa kila ambalo ni la kumkasirisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Wala zisitafutwe sababu za kuzimika umeme ovyo ovyo kwenye vipindi vya matamasha haya. Zaidi ya hayo, Rabb Atuepushe - tusimtafute "mchawi wetu" pale ardhi itakapotikishwa, bahari ikahamia ardhini na ardhi ikaenda baharini, mbingu zikateremsha mvua za maangamizi na mengi mengineyo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atuhifadhi na athari ya vitimbi vya matamasha haya.
Wazee na vijana wa Kiislamu, ni lazima wawe macho na matamasha kama haya yasiyokuwa na azma njema kwa Waislamu. Tuwazuie wanetu, majirani pamoja na rafiki zetu kushiriki humo. Kuporomoka kwao, ndio hasara kwetu sote. Samaki akioza mmoja, huoza wote.