Wamerithi Shamba Wamelikodisha, Wanatofautiana Namna Ya Kutekeleza Wasia
SWALI:
Assalaam Aleikum.
Sisi tulirithi shamba kutoka kwa mama yetu mzazi. Warithi tulikuwa sisi (watoto saba, wanaume watatu na wanawake 4); baba yetu na bibi yetu (mama wa aliyefariki mama yetu). Tulikuwa karibu sana na bibi yetu kwa hali na mali na akatuusia kuwa, akifariki sehemu ya urathi wake anatuachia sisi. Hayo aliyaeleza kwetu na kwa baadhi ya wajomba zetu kwa njia ya mdomo tu, bila maandishi.
Taratibu tuliyonayo ni kukodisha mazao ya shamba na kugawanya kipato chake kwa warithi kama inavyostahili. Baada ya kufariki bibi yetu; warithi wake (watoto wa kaka yake aliyefariki mapema zaidi); walielezwa kuhusu wasia ule lakini wengine waliupinga kwa vile haukuwa wa maandishi.
1. Jee vipi tunaweza kuutekeleza wasia kama huo?
2. Bibi yetu aliwacha watoto wa kaka yake na dada yake wa kike na kiume; Jee wote hao ni warithi halali?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mirathi ya mama na bibi yenu.
Mwanzo tunaona tuangazie kuhusu urithi wa mama yenu mzazi, ambao ni kama ifuatavyo:
1. Baba yenu – Robo (1/4).
2. Mama yake mama yenu (Bibi) - Sudusi (1/6).
3. Kila binti atapata - 1/24.
4. Kila mtoto wa kiume atapata - nusu ya sudusi (1/12).
Hakika ni kuwa wasiya ni muhimu uandikwe kwani kufanya hivyo kunaondoa utata wowote ule ambao unaweza kutokea kama wenu huo. Ikiwa haukuandikwa ni lazima kuwe na mashahidi watakaotoa ushahidi kuwa kweli wamemsikia aliyefariki kabla ya kuaga kwake dunia akiusia hilo. Ikiwa hao mashahidi kama mnavyosema ni wajomba zenu wanatakiwa waitwe ili kutoa ushahidi kuwa wamemsikia bibi yenu akiusia kama mnavyosema.
Na kisheria mtu anaweza kuusia thuluthi ya mali yake na kiwango hicho ni kingi au kikubwa kama alivyosema Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuusia hilo Sa’ad bin Abi Waqqaasw (Radhiya Allaahu ‘anhu).
Kwa hiyo, ikiwa bibi yenu ameusia kuwa urithi wake mupatiwe nyinyi wote atakuwa amekosea kabisa katika kufanya hilo. Kisha pia mtu anaweza kuusia hiyo thuluthi kwa mtu ambaye hawezi kurithi kisheria, kwani anayerithi hawezi kupewa fungu lingine katika wasiya. Na kufanywa hivo itakuwa ni makosa.
Wasiya huo unaweza kutekelezwa kwa njia ifuatayo:
1. Mashahidi waulizwe kuhusu hayo aliyosema bibi yenu.
2. Wasiya alioutoa usizidi thuluthi ya mali yake.
3. Awe ameutoa kwa hiyari sio kulazimilishwa akiwa na akili timamu na anafahamu analosema.
Ama katika urithi hao mliowataja ndio pekee jamaa za aliyefariki kwani hilo halipo wazi kutoka katika swali lenu. Je, aliyefariki aliacha jamaa wengine? Kwa mfano:
1. Je, mumewe alikuwa hai?
2. Je, alikuwa na watoto? Watoto wenyewe ni wangapi – wa kiume na kike?
3. Je, wazazi wake wako hai, wote au mmoja wao?
Kulingana na sheria ya Kiislamu watoto wa kaka wa aliyefariki hawapati chochote ikiwa kaka yao ameaga kabla ya aliyefariki. Ama kaka na dada wa aliyefariki inategemea kuwepo na warithi wengine wa aliyefariki. Kwa mfano, ikiwa aliyefariki alikuwa na watoto wake hasa wa kiume basi kaka na dada hawatapata chochote. Katika swali lenu mmetaja wajomba zenu, je, hawa ni ndugu za mama yenu na hivyo watoto wa bibi au ni vipi?
Tunaomba mtujulishe kuhusu maswali yetu hapo juu 1-3, ili tupate kuwasaidia kwa njia iliyo nzuri zaidi.
Na Allaah Anajua zaidi